Sakata la mashangingi, Bunge labebeshwa zigo, wadau wataka sheria
7 mins read

Sakata la mashangingi, Bunge labebeshwa zigo, wadau wataka sheria

Dar es Salaam. Wadau wa masuala ya sheria na utawala bora wamelitaka Bunge liweke msingi wa kisheria wa kudhibiti ununuzi na matumizi ya magari ya kifahari kwa viongozi wa Serikali, wakisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha uwajibikaji na kuelekeza fedha za umma kwenye huduma za wananchi.

Wito huo umetolewa na wadau waliozungumza na Mwananchi kufuatia maagizo ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu kwa Kamati ya Bunge ya Bajeti, aliyoyatoa bungeni jijini Dodoma, jana.

Spika Zungu aliielekeza kamati hiyo kuwahoji watumishi wa Serikali walionunua magari ya kifahari kinyume na Waraka wa Utumishi wa Umma, akitaka uwajibikaji katika kubana matumizi serikalini.

Alizitaka taasisi za umma kuzingatia miongozo ya ununuzi wa magari na kutafuta njia za kupunguza gharama za uendeshaji, ikiwamo matumizi ya magari ya umeme, gesi na teknolojia mseto (Hybrid).

Katika kuonesha umuhimu wa viongozi kuwa mfano wa kubana matumizi, Zungu alirejea wito wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kupunguza misafara ya magari, akitaka taasisi nyingine za Serikali kuzingatia nidhamu hiyo ya matumizi.

Aprili 8, 2026, akiwaapisha viongozi Ikulu Chamwino, Dodoma, Rais Samia Suluhu Hassan alizitaka taasisi za Serikali kupunguza gharama za matumizi ya magari, ikiwamo mafuta na safari zisizo za lazima.

Ili kuchochea utekelezaji, alianza na ofisi yake, akielekeza watendaji wanaoambatana naye kutumia basi moja badala ya magari tofauti ili kudhibiti gharama za Serikali.

Katika msisitizo wa uwajibikaji, Spika alisema Serikali hutumia Sh558 bilioni kwa mwaka kugharamia magari 15,742, pikipiki 14,047 na mitambo 373 ya Serikali, akiitaka Serikali kudhibiti ununuzi wa magari hayo ya kifahari.

“Gari moja aina ya Toyota Land Cruiser VX-S Special Edition linagharimu zaidi ya Sh300 milioni, fedha zinazoweza kujenga madarasa 17, kununua madawati 2,005 au kujenga zahanati,” alisema Spika.

Kufuatia hatua hiyo, Zungu ameagiza Kamati ya Bunge ya Bajeti kushirikiana na Wizara ya Fedha na Ofisi ya Waziri Mkuu kuchunguza ununuzi wa magari kuanzia mwaka 2013 hadi 2026 na kuwahoji viongozi waliokiuka waraka wa Serikali.

Wakizungumzia kauli hiyo ya Spika Zungu,  leo Jumamosi Oktoba 31, 2026 wachambuzi wa masuala ya siasa, sheria na utawala bora wametaka kutungwa kwa sheria maalumu inayotoa mwongozo wa aina ya magari yanayostahili kwa kila ngazi ya kiongozi.

Wakili na mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala bora, Aloyce Komba amesema agizo la Spika Zungu lina nia njema, lakini utekelezaji wake unaweza kukabiliwa na changamoto kutokana na kutokuwepo kwa sheria inayoweka viwango vya magari kwa ngazi za viongozi.

“Kwa hoja hii, Bunge lina nia njema, lakini utekelezaji wake unaweza kusuasua kutokana na pengo la kisheria kwa kuwa,  hakuna sheria inayotoa mwongozo wa aina ya magari kwa ngazi za viongozi hapa nchini. Ili kufanikisha maelekezo hayo, Bunge liende mbali zaidi, litumie mamlaka yake kutunga sheria kuhusiana na hilo, hapo litapata nguvu ya kisheria,” amesema.

Amesema sheria hiyo inapaswa kuwa rahisi na kutamka wazi aina ya magari yanayopaswa kununuliwa na Serikali kwa ngazi tofauti za viongozi ili kutoa mwongozo na wajibu wa kisheria wa kudhibiti suala hilo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza), Profesa Mohamed Makame amesema uchunguzi wa kamati za Bunge unapaswa kubaini kwa kina michakato ya ununuzi na muda ambao maagizo ya kudhibiti ununuzi wa magari hayo yalitolewa.

“Inaweza kuwa mapema sana kuhukumu kabla ya kupata taarifa zaidi kwa kuwa maagizo yametolewa karibuni, hivyo ni vigumu kuhukumu kuwa ununuzi wa magari haujafuata utaratibu. Hili linatokana na mchakato wa ununuzi wa magari; ulianza lini, ikiwa ulifanyika kabla ya maagizo, hatua zake zitakuwa tofauti,” amesema.

Profesa Makame amesema nia ya Spika Zungu ni njema na sahihi kwa mhimili wa Bunge kusimamia matumizi ya Serikali.

“Kwa hoja hiyo ya Spika, Bunge limesimamia masilahi ya umma, limeona matumizi ya fedha kupita kiasi kwenye jambo linalomfurahisha mtu mmoja mmoja, hivyo linataka udhibiti ili zielekezwe katika kuwanufaisha wananchi,” amesema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Conrad Masabo amesema Spika wa Bunge ana mamlaka ya Kikatiba na kisheria ya kuisimamia na kuiwajibisha Serikali, lakini utekelezaji wa azma hiyo unaweza kuwa mgumu ikiwa Bunge lenyewe halitasimamia kikamilifu mifumo ya matumizi ya fedha za umma.

Amesema Bunge haliwezi kuiacha Serikali pekee kubeba lawama za ununuzi wa magari ya kifahari, kwa kuwa ndicho chombo chenye mamlaka ya kujadili na kupitisha bajeti zinazowezesha ununuzi huo.

“Bunge lina mamlaka ya kupitisha bajeti. Kama bajeti inaruhusu magari makubwa kununuliwa na mamlaka mbalimbali za Serikali, chanzo cha fedha hizo ni Bunge lenyewe kwani hakuna mamlaka ya Serikali inayotenga fedha na kununua magari bila kupitisha bajeti yake bungeni.

“Kwa hiyo, kama kuna magari ya kifahari yananunuliwa, chanzo ni Bunge lenyewe. Ili kudhibiti haya, Bunge linatakiwa kuacha kupitisha bajeti za hovyo,” amesema.

Dk Masabo ameongeza kuwa Spika anaweza kukabiliwa na shinikizo kutoka ndani ya chama chake, jambo linaloweza kuathiri uhuru wake wa kufanya uamuzi katika kuwawajibisha viongozi wa Serikali.

Amesema hata kama kamati husika ya Bunge itawasilisha ripoti ya uchunguzi, uamuzi ya mwisho yanaweza kuathiriwa na mijadala na misimamo ya chama, hivyo kupunguza ufanisi wa hatua zinazokusudiwa kuchukuliwa.

Amesisitiza kuwa Spika Zungu anapaswa kuanza kwa kutumia mamlaka ya Bunge kudhibiti bajeti za ununuzi ya magari, kwa kuhakikisha mawaziri wanaowasilisha bajeti hizo wanatoa maelezo ya kina kuhusu mahitaji halisi, idadi ya magari yaliyopo, upungufu uliopo na aina ya magari yanayohitajika kabla ya kuidhinisha fedha.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim, Dennis Konga amesema uwajibikaji kuhusu ununuzi wa magari ya Serikali haupaswi kuishia kwenye taasisi za Serikali, bali uanze pia ndani ya Bunge ambalo lina mamlaka ya kisheria ya kujadili, kutathmini na kupitisha bajeti za ununuzi.

Amesema Spika anapaswa kutumia nafasi yake kusimamia udhibiti huo tangu hatua ya kuidhinisha bajeti badala ya kusubiri ununuzi ufanyike ndipo kuanzisha uchunguzi.

“Kama bajeti imepita bungeni, halafu anakuja kufuatilia huku nje na anaiagiza kamati kuwahoji walionunua, maana yake tatizo lilianzia kwake. Kama kuna tatizo, anatakiwa kulisimamia huko huko bungeni.

“Kazi yake ya kwanza ni kudhibiti bajeti za ovyo zisipite na kufanya tathmini wanapowasilisha bajeti za ununuzi wa magari, kujiridhisha magari yaliyopo ni mangapi, upungufu ni mangapi na wanataka kununua mangapi,” amesema.

Hata hivyo, Dk Konga amesema suala la magari ya Serikali halipaswi kuamuliwa kwa kuangalia gharama pekee, bali mahitaji ya kazi na mazingira ya maeneo husika.

Ametoa mfano wa mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye mazingira ya barabara za mjini yanaweza yasihitaji gari lenye uwezo mkubwa wa kupita maeneo magumu, tofauti na mkuu wa Mkoa wa Njombe ambaye majukumu yake yanaweza kumlazimu kutumia gari linaloweza kupita kwenye barabara za milima, mabonde na maeneo yenye matope.

“Kwa hiyo, hatuwezi kuacha kununua magari ya kifahari kwa sababu tunabana matumizi. Tununue magari kulingana na mahitaji na maeneo husika,” amesema.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *