Utafiti mpya waibua matumaini ya kudhibiti VVU bila ARV
Dar es Salaam. Utafiti mpya wa kisayansi umeibua matumaini katika mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), baada ya kubaini kuwa kingamwili maalumu zinaweza kuchelewesha kwa kiasi kikubwa kurejea kwa virusi mwilini baada ya mtu kusitisha kwa muda matumizi ya dawa za kufubaza virusi hivyo (ARV).
Matokeo hayo yanaashiria uwezekano wa siku zijazo wa baadhi ya watu wanaoishi na VVU kudhibiti maambukizi kwa muda mrefu bila kutegemea matumizi ya ARV kila siku, ingawa watafiti wanasisitiza kuwa bado hakuna uthibitisho wa tiba inayoweza kuondoa kabisa virusi mwilini.
Utafiti huo wa awamu ya pili, unaojulikana kama RIO, ulichapishwa katika jarida la kimataifa la Nature Medicine mwaka 2026 na ulihusisha wanaume 68 wanaoishi na VVU, wengi wao wakiwa walianza kutumia ARV katika hatua za awali za maambukizi.
Utafiti huo uliongozwa na Marcílio J. Fumagalli kutoka Maabara ya Utafiti wa Kinga ya Mwili katika Ngazi ya Molekuli, Chuo Kikuu cha Rockefeller, kilichopo New York, Marekani, pamoja na watafiti wenzake.
Watafiti walichunguza uwezo wa kingamwili mbili maalumu zinazojulikana kama 3BNC117-LS na 10-1074-LS katika kudhibiti VVU.
Washiriki waligawanywa katika makundi mawili. Kundi la kwanza lililokuwa na watu 34 lilipatiwa kingamwili hizo mbili, huku kundi la pili lenye idadi sawa likipewa dawa bandia (placebo).
Baada ya kupokea matibabu hayo, washiriki walisitisha matumizi ya ARV kwa muda chini ya uangalizi wa karibu wa watafiti ili kuchunguza uwezo wa kingamwili hizo kudhibiti virusi bila msaada wa dawa za kawaida.
Matokeo yalionyesha kuwa kundi lililopokea kingamwili lilifanikiwa kuchelewesha kurejea kwa virusi kwa kiwango kikubwa zaidi ikilinganishwa na kundi lililopokea placebo.
Katika kipindi cha wiki 20 baada ya kusitisha ARV, washiriki wanane pekee kati ya 34 katika kundi lililopokea kingamwili walipata kurejea kwa virusi, ikilinganishwa na washiriki 30 kati ya 34 katika kundi lililopokea placebo.
Aidha, muda wa wastani kabla ya washiriki kuhitaji kuanza tena ARV ulikuwa wiki 45.4 kwa kundi lililopokea kingamwili, ikilinganishwa na wiki 4.6 kwa kundi lililopokea placebo.
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa kingamwili hizo zinaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuongeza muda ambao baadhi ya watu wanaweza kudhibiti VVU bila kutumia ARV. Hata hivyo, hazijaonyesha uwezo wa kuondoa kabisa virusi mwilini.
Mtafiti aeleza hatua inayofuata
Akieleza mwelekeo wa tafiti zaidi kuhusu kingamwili hizo, Fumagalli amesema hatua inayofuata ni kuchunguza namna seli za kinga zinavyobadilika na kuongeza uwezo wake wa kupambana na VVU wakati wa matibabu.
“Hatua inayofuata tunayotaka kuchunguza ni aina ya vitu vinavyozalishwa na seli hizi kabla na baada ya matibabu, na iwapo seli hizo zinakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kupambana na virusi wakati wa matibabu yanayotumia kingamwili,” amesema Fumagalli.
Kauli hiyo inaonyesha kuwa pamoja na kuchunguza uwezo wa kingamwili kuzuia virusi kuongezeka, watafiti wanataka kuelewa zaidi namna zinavyoshirikiana na mfumo wa kinga ya mwili katika kudhibiti maambukizi.
Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Elisha Osati, amesema utafiti huo ni hatua muhimu katika kutafuta mbinu mpya za kudhibiti VVU, hasa kwa kuwa unachunguza uwezekano wa kutumia kingamwili maalumu kuongeza muda ambao mtu anaweza kudhibiti virusi bila kutegemea ARV.
“Ni hatua nzuri. Hata sindano za Lenacapavir ambazo zimeshaanza kutumika duniani zilianza na utafiti. Hata hivyo, matokeo yanapaswa kutafsiriwa kwa tahadhari kwa sababu utafiti ulihusisha wanaume 68 pekee na haujathibitisha kuwa kingamwili hizo zinaweza kuponya VVU. Bado kuna safari ndefu,” amesema Osati.
Wakati utafiti huo ukiibua matumaini ya mbinu mpya za kudhibiti VVU, dunia pia imepiga hatua katika matumizi ya dawa za muda mrefu za kukabiliana na maambukizi hayo kupitia Lenacapavir.
Dawa hiyo ya sindano, inayotolewa mara mbili kwa mwaka, ilipendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2025 kama njia nyingine ya kujikinga na maambukizi ya VVU (PrEP) kwa watu ambao hawajaambukizwa.
Utafiti wa RIO ni miongoni mwa tafiti zaidi ya 30 zinazoendelea duniani kutafuta njia za kuondoa VVU vilivyojificha ndani ya seli za mwili au kuvidhibiti bila kutumia dawa kila siku.
Mwakilishi wa mtandao wa watu wanaoishi na VVU nchini Tanzania, Janeth Lyimo, amesema ni muhimu watafiti na wadau wa afya kutoa elimu sahihi ili watu wasitafsiri matokeo hayo kuwa tayari kuna tiba na kuamua kuacha kutumia dawa zao.
“Pia, tafiti zijazo zinapaswa kuwajumuisha wanawake na makundi mbalimbali ya watu wanaoishi na VVU ili kuhakikisha matokeo yanawanufaisha watu wengi,” amesema Janeth.
Hifadhi ya VVU mwilini bado ni changamoto
Utafiti huo pia umechunguza hifadhi ya virusi vya VVU inayobaki ndani ya seli za kinga za mwili hata mtu anapotumia ARV na kuwa na kiwango kisichogundulika cha virusi kwenye damu.
Hifadhi hiyo, inayojulikana kitaalamu kama HIV reservoir, ni mojawapo ya changamoto kubwa zinazofanya iwe vigumu kuondoa kabisa VVU mwilini.
Ingawa ARV huzuia virusi kuzaliana na kuenea, haziwezi kuondoa kikamilifu virusi vilivyojificha ndani ya seli za mwili. Hali hiyo ndiyo inayoweza kusababisha virusi kurejea mtu anapoacha kutumia dawa hizo.
Watafiti walitumia vipimo vya kisayansi kuchunguza ukubwa wa hifadhi hiyo kabla ya kuanza kwa utafiti.
Walibaini kuwa washiriki walikuwa na kiwango kidogo cha virusi vilivyokuwa na uwezo wa kuzaliana, hali iliyohusishwa na ukweli kwamba wengi wao walianza matibabu mapema baada ya kupata maambukizi.
Virusi vyabaini dalili za usugu
Licha ya mafanikio yaliyobainika, utafiti huo pia umeonyesha changamoto inayohitaji kufanyiwa uchunguzi zaidi.
Virusi vilivyoanza kurejea kwa baadhi ya washiriki waliopokea kingamwili vilionyesha dalili za kujenga usugu dhidi ya kingamwili ya 10-1074-LS, lakini si kwa kiwango sawa dhidi ya 3BNC117-LS.
Watafiti pia walibaini uhusiano kati ya uwezo wa kingamwili za asili zilizokuwapo mwilini mwa mshiriki kupambana na VVU na muda ambao virusi vilichukua kurejea baada ya kusitisha ARV.
Matokeo hayo yanaashiria kuwa kinga ya asili ya mtu inaweza kuwa na mchango katika mafanikio ya matibabu yanayotumia kingamwili maalumu.
Kwa ujumla, utafiti wa RIO unaongeza ushahidi wa kisayansi katika juhudi za kutafuta mbinu mpya za kudhibiti VVU, ikiwamo uwezekano wa kutumia kingamwili maalumu kuongeza muda wa udhibiti wa virusi bila kutegemea matumizi endelevu ya ARV.
