Baba wa IGP Wambura azikwa Musoma, familia yatakiwa kusherehekea
Musoma. Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi amewaongoza waombolezaji katika mazishi ya Deusdedit Wambura, baba mzazi wa Mkuu wa Polisi Nchini (IGP), Camilius Wambura, huku akiwataka washerehekee maisha yake kwani alikuwa amefikisha umri wa miaka 100.
Wambura aliyefariki dunia Oktoba 26, 2026 jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa zaidi ya miaka 19, amezikwa leo Jumamosi Oktoba 31, 2026 huku ikielezwa kuwa chanzo cha kifo chake kikitajwa kuwa ni tezi dume, figo na moyo, magonjwa yaliyosababisha apate huduma ya matibabu katika hospitali mbalimbali nchini.
Wakitoa salamu za rambirambi, baadhi ya viongozi waliohudhuria kwenye mazishi hayo, wamewaomba ndugu jamaa na marafiki kutohuzunika badala yake washerehekee maisha ya Wambura kutokana na kuishi miaka 100, tofauti na watu wengine.
Akizungumza kwenye shughuli hiyo ya maziko, Katambi amesema familia haipaswi kuwa na majonzi bali washerehekee maisha ya mzee huyo kwani ameishi maisha ya utimilifu.
Amesema maandiko matakatifu yanasema maisha ya binadamu ni miaka 70, hivyo miaka mingine ni ya nyongeza kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Amesema utimilifu wa maisha ya mzee huyo unaendana na mwezi aliozaliwa ambao ni Aprili ambapo kwa imani ya kikatoliki mwezi huo ni wa Ufufuo wa Yesu Kristo, huku akifariki Oktoba ambao ni mwezi wa Rozari.
“Mimi hata miaka 50 sijafika, Mwenyezi Mungu nisaidie, mzee wetu ametupa changamoto kubwa sana hasa katika malezi, amelea watoto wake katika njia nzuri,wapo wacha Mungu, wapo watumishi ni wazalendo na waadilifu,” amesema.
Kwa upande wa Mbunge wa Musoma Mjini (CCM), Mgore Miraji amesema hakuna sababu ya familia kuhuzunika badala yake washerehekee maisha ya baba na babu yao kwani alikuwa ni mbaraka kwao.
Baadhi ya waombolezaji wakiwa kwenye msiba wa baba mzazi wa Mkuu wa Polisi (IGP) Camilius Wambura, mzee Deusdedit Wambura ,mjini Musoma. Picha na Beldina Nyakeke
“Ingawa mzee ameondoka na siku zote kifo kinahuzunisha na hakizoeleki lakini tunapaswa kumshukuru Mungu kwa miaka 100 ya mzee wetu kwani ni wachache wanaofikisha miaka hii,” amesema.
Mbunge wa Serengeti (CCM), Mary Daniel amesema familia inapaswa kumshukuru Mungu kumpa mzee huyo umri mrefu kwani wengi wametamani kufikia umri huo lakini kwa mapenzi ya Mungu haikuwezekana.
“Mimi baba yangu Joseph Surati hakufikisha hata miaka 60, naomba kujiunganisha na baraka za mzee wetu,nami niwe miongoni mwa watu watakaoishi miaka mingi,niwaombe badala ya kuomboleza tusherehekee maisha yake tukimtukuza Mungu,” amesema.
Akiongoza misa ya mazishi katika Kanisa Kuu la Katoliki la Bikira Maria Mama wa Mungu Musoma, Paroko wa Parokia ya Musoma Mjini, Padri Medard Chegere amewataka waombolezeaji wote kutenda mema ili maisha yao yawe na faida kwa jamii,kanisa,umma na Taifa kwa ujumla.
Amesema enzi za uhai wake, marehemu alijitahidi kuishi maisha ya uadilifu na utu na hivyo ameacha kumbukumbu nzuri katika sekta nyingi ikiwamo ya elimu,afya, siasa na uongozi.
“Jumuiko hili ni taswira halisi namna gani Deusdedit aliishi katika jamii,tunapaswa kuwa waadilifu na kuacha alama nzuri , kiongozi yeyote kuanzia ngazi ya jamii ni yule anayeacha alama nzuri kwa watu wake na alama hiyo ni amani, mshikamano,umoja na upendo,” amesema.
Wambura ambaye kitaaluma alikuwa ni mwalimu alishika nyadhifa mbalimbali katika sekta ya elimu ambapo hadi anastaafu utumishi wa umma alikuwa ofisa elimu nafasi ambayo alihudumu katika wilaya mbalimbali nchini.
Mbali na utumishi wa umma, Wambura pia alikuwa mwanasiasa wa chama cha Tanu na kisha CCM ambapo alishika nyadhifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na uongozi kwa nafasi mbalimbali ngazi ya wilaya, mkoa na Taifa.
Marehemu Wambura ameacha watoto wanane, wajukuu 30 na vitukuu 28, amezikwa katika makaburi ya Mwisenge yaliyopo katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Mazishi hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwepo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, Waziri wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Rhimo Nyansaho, Mkuu wa Majeshi (CDF), Jenerali Mkunda.
Wengine ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda, makamanda wa polisi wa mikoa mbalimbali na viongozi wengine wengi wakiwemo wanasiasa.
