Mwanafunzi aliyetoroshwa Mvomero apatikana | Mwananchi
Morogoro. Hatimaye mwanafunzi wa kidato cha nne, aliyetoroshwa kwa nia ya kwenda kuozeshwa, amepatikana na kurejea kwa wazazi wake waishio Kijiji cha Sokoine, Kata ya Dakawa, Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.
Awali, taarifa iliyotolewa jana Oktoba 30, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Andrew Kantimbo, ilieleza kuwa binti huyo kutoka jamii ya kimaasai (jina limehifadhiwa), anasoma Shule ya Sekondari Sokoine Memorial, iliyopo Dakawa na alidaiwa kutoroshwa na vijana watatu wa kiume wa jamii hiyo Oktoba 26, 2026 mchana.
Kufuatia tukio hilo, vijana watatu wa jamii ya kimaasai pamoja na mama mzazi wa kijana anayetuhumiwa kumchukua binti huyo, walikamatwa na Polisi mkoani humo huku mmoja akiendelea kusakwa.
Akieleza taarifa za kupatikana kwa binti huyo, Kumbuni Twaro amesema tayari amepatikana jana jioni na taratibu nyingine za kipolisi ikiwa ni pamoja na kupima afya yake zinaendelea.
“Binti ametueleza kuwa baada ya kutoroshwa alipelekwa sehemu ambayo haifahamu na huko alikuwa amefungiwa ndani hadi jana, ndipo alipopakiwa kwenye basi, hata hivyo walitunza tiketi ambayo inaonyesha alipandia eneo la Kibaigwa mkoani Dodoma. Kuhusu afya yake, Polisi na vyombo vingine vya Serikali vinafuatulia,” amesema Twaro.
Twaro ameeleza kuwa Jumapili iliyopita, kijana huyo na jamaa zake, walifika nyumbani kwake na kutaka kutoa posa kwa ajili ya kumchumbia binti huyo, hata hivyo, yeye pamoja na binti mwenyewe walikataa jambo hilo.
“Nilikataa kwa sababu binti yangu anasoma na Serikali haitaki mambo ya kuozesha mabinti wakiwa wanasoma. Pia, binti mwenyewe kwa sasa hataki kuolewa, anataka kuendelea na masomo ya kidato cha tano kama atafaulu na hata asipofaulu nitamsomesha shule binafsi au ufundi,” amesema Twaro.
Ameongeza kuwa: “Mimi mwenyewe nimesoma hadi kidato cha nne, nafahamu umuhimu wa elimu na nimekuwa nikijitahidi kumsomesha binti yangu kwa gharama zozote na hata maendeleo yake ya kitaaluma ni mazuri na ni binti aliyetulia na hana tabia mbovu.”
Akieleza mila na tamaduni za kimaasai kwenye suala ya kuozesha vijana wao, Twaro amesema miaka ya nyumba kabla ya elimu kupewa msisitizo na Serikali, binti alikuwa anaweza kuchumbiwa hata akiwa mchanga na wazazi walikuwa wakikubali kupokea posa, lakini kwa sasa mila hiyo haina nafasi tena.
Diwani wa Kata ya Dakawa ambaye anatoka kwenye jamii ya kimaasai, Joshua Lugaso amesema Serikali kupitia mtendaji kata na maofisa ustawi wa jamii, wamejipanga kuhakikisha binti anakuwa salama wakati wote.
Kuhusu vipimo, Lugaso amesema baada ya kurudi, jana ileile alipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mvomero na kufanyiwa vipimo mbalimbali na majibu ya vipimo hivyo yamehifadhiwa.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Dk Philipina Philipo amesema katika wilaya hiyo kuna changamoto ya mabinti kuzaa katika umri mdogo na takwimu zinazoonyesha hali halisi ya changamoto hiyo.
Akieleza madhara yanayoweza kupatikana kutokana na mimba za utotoni, Dk Philipo amesema binti anaweza kupata uchungu pingamizi, kushindwa kuzaa kwa njia ya kawaida kutokana na via vya uzazi kutokomaa vizuri na pia kupoteza damu nyingi wakati wa kujifungua.
“Madhara mengine ni ya kisaikolojia hasa pale binti atakapopata changamoto za ujauzito na mabadiliko ya homoni, kushindwa kuhimili changamoto za ujauzito na uzazi, kushindwa kulea mtoto wake kwa sababu ya kutokomaa kiakili,” amesema Dk Philipo.
Wakati huohuo, kiongozi wa dini wa kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Mchungaji Petro Karaita amesema ndoa hizo za utotoni mara nyingi zimekuwa zikifungwa kwa taratibu za kimila na sio dini.
“Bado baadhi ya wazazi kwenye jamii ya kimaasai zinaendelea na kuozesha mabinti wakiwa shule na wengine na umri mdogo na baya zaidi wamekuwa wakichukua mahali ya ng’ombe ambao hawalingani na thamani ya mabinti hao.”
Amesema yeye kama kiongozi wa dini amekuwa akijitahidi kutoa elimu Kwa jamii yake kuhusu madhara ya kuwaozesha mabinti wakiwa na umri mdogo lakini pia madhara ya kuwakatisha masomo.

