Wawili wajitokeza kusalimisha silaha zao Mbeya
2 mins read

Wawili wajitokeza kusalimisha silaha zao Mbeya

Mbeya. Wakati kampeni ya kusalimisha silaha kwa hiari zinazomilikiwa kinyume cha sheria ikihitimishwa leo Oktoba 31, 2026 watu wawili wakazi wa Mkoa wa Mbeya wamejitokeza kukabidhi silaha mbili na risasi 22 katika kituo kikuu cha polisi.

Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi alilolitoa Septemba Mosi, 2026, akiwataka wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha ndani ya kipindi cha miezi miwili.

Akizungumza leo Oktoba 31, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, amesema watu hao wamekabidhi silaha hizo kwa hiari katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Mbeya.

“Leo Oktoba 31, 2026 ni siku ya mwisho ya kampeni ya kusalimisha silaha haramu kupitia ofisi za serikali za mitaa, vijiji au kwa watendaji wa kata. Watu wawili wamejitokeza na kusalimisha silaha mbili kwa hiari yao,” amesema.

Amesema sababu zilizowafanya wamiliki hao kuamua kurejesha silaha hizo ni pamoja na umri mkubwa, hali iliyowafanya washindwe kuendelea kumudu kuzimiliki na kuziendesha.

Amezitaja silaha hizo kuwa ni bunduki aina ya Long Rifle 22 iliyokuwa na risasi tatu na bastola aina ya Revolver 38 Webley iliyokuwa na risasi 19.

Kuzaga amesema kampeni hiyo ilizinduliwa na Waziri Katambi Septemba Mosi mwaka huu, huku akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuchukua hatua dhidi ya watakaobainika kumiliki silaha kinyume cha sheria na kushindwa kuzisalimisha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga akionyesha silaha zilizo salimishwa na watu wawili  kufuatia kampeni ya kuwataka wamiliki wanaomiliki kinyume cha sheria kusalimisha kwa hiari.

Amesisitiza kuwa wananchi wanaomiliki silaha hizo wanapaswa kuzifikisha katika ofisi za serikali za mitaa, vijiji au kwa watendaji wa kata ili kuepuka kukabiliwa na hatua za kisheria.

Akizungumzia suala hilo, mkazi wa Ilemi jijini Mbeya, Sikitu Amos ameshauri Jeshi la Polisi kuweka utaratibu wa kuwakutanisha wamiliki wa silaha kuwapa elimu kuhusu matumizi salama ya silaha hizo, badala ya kuwa vitisho kwenye kumbi za starehe.

Amesema elimu hiyo itasaidia kudhibiti matumizi holela ya silaha, hususani katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu.

Pia, ameshauri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuanzisha programu ya upimaji wa afya ya akili kwa wamiliki wa silaha, hususani kwa wanandoa ili kusaidia kuzuia matukio ya mauaji yanayoweza kuepukika.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *