Zanzibar inavyoelemewa na mzigo wa taka, yazalisha tani 663 kwa siku
7 mins read

Zanzibar inavyoelemewa na mzigo wa taka, yazalisha tani 663 kwa siku

Unguja. Pamoja na sifa yake kama kisiwa cha utalii duniani, Zanzibar inakabiliwa na janga la kimazingira linalotishia mwonekano wake na mustakabali wa sekta ya utalii.

Takwimu mpya kutoka Mradi wa IslandPlas zinaonyesha kuwa kisiwa cha Unguja pekee kinazalisha takribani tani 663 za taka ngumu kila siku, lakini kati ya hizo, tani 120 pekee ndizo zinazokusanywa na kutupwa kwa utaratibu unaofaa katika dampo la Mtoni na Kibele.

Hii inamaanisha kuwa zaidi ya asilimia 82 ya taka hizo, sawa na tani 543 kwa siku, hazina mfumo rasmi wa ukusanyaji. Taka hizo huishia kwenye mitaro ya maji, mashambani na hatimaye fukwe za bahari, jambo linalohatarisha afya ya jamii na uchumi unaotegemea utalii.

Uchunguzi wa kina unaonyesha kuwa plastiki pekee inachangia asilimia 80 ya taka zote zinazopatikana katika mazingira ya bahari na maeneo yanayozunguka visiwa vya Unguja na Pemba.

Mtaalamu wa afya ya jamii, Mwanajuma Haji, anasema hali hiyo ina athari mbili kubwa ambazo tayari zinaonekana katika jamii.

“Kijamii, taka zinazozagaa ovyo ni chanzo cha magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na homa ya matumbo, hasa wakati wa mvua mitaro inapoziba na maji machafu kuingia majumbani,” anasema Mwanajuma.

Kimazingira, kwa mujibu wa mtaalamu huyo, plastiki zinazozagaa ndizo zinazoua viumbe wa baharini na kuharibu miamba ya matumbawe ambayo ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya watalii.

“Kasa anaweza kula mfuko wa plastiki akidhani ni kiumbe wa baharini. Samaki wanakufa kwa kukabwa na kamba za plastiki. Tukiharibu bahari, tunaua utalii wenyewe,” anaongeza.

Hali hiyo imeilazimu Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (Zema) kukiri kuwa mfumo rasmi wa manispaa na halmashauri pekee hauwezi kumudu mzigo huo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Wakusanyaji Taka Zanzibar, uliofanyika hivi karibuni Unguja, Kaimu Mkurugenzi wa Zema, Haidar Bakari Machano amesema suluhisho linahitaji kuwahusisha watu ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya kazi hiyo kimyakimya.

“Wakusanyaji taka wana nafasi muhimu katika kuokoa vifaa vinavyoweza kutumika tena, hususan plastiki, ambazo zingeweza kuishia kwenye mitaro, fukwe na baharini na kuhatarisha mazingira na afya za wananchi,” amesema Machano.

Ameongeza kuwa kuanzishwa kwa jukwaa hilo ni hatua ya kuwaunganisha wadau hao na kuwapa sauti ya pamoja ya kutetea maslahi yao.

“Kazi wanayoifanya kila siku inaokoa thamani ya vifaa vinavyoweza kutumika tena, inapunguza kiasi cha taka kinachoingia katika mazingira na kusaidia kulinda afya za wananchi wetu,” amesema.

Jukwaa hilo linawaleta pamoja wakusanyaji kutoka mitaani, wanunuzi wa taka na waendeshaji wa vituo vya ukusanyaji kutoka Unguja na Pemba. Kwa miaka mingi, kundi hilo limekuwa likifanya kazi bila kutambuliwa, vifaa vya kujikinga wala mikataba.

Katika jukwaa hilo, wakusanyaji walipata nafasi ya kueleza changamoto zao. Mmoja wao ni Salma Khamis, mkusanyaji kutoka Fuoni, ambaye kwa miaka minne amekuwa akiamka saa 10 alfajiri kusaka plastiki.

“Kila siku natembea zaidi ya kilomita 10 na gunia mgongoni, nakusanya chupa za maji na mifuko ya plastiki. Watu wakiona gunia langu wananicheka, wanasema nimechoka,” amesema na kuongeza:

“Lakini kwa kazi hii nalisha watoto wangu wawili. Shida ni bei ndogo, kilo moja ya chupa ngumu ni Sh300 tu, na hakuna glavu. Tunachomwa mikono na chupa zilizokatika.”

Ameomba Serikali na wadau kuwapatia vifaa vya kujikinga kama glavu, buti na barakoa, pamoja na mikokoteni ya kisasa ili waweze kukusanya taka nyingi zaidi kwa usalama.

Kwa upande wa wanunuzi, Hadija Mohammed Ali, mmiliki wa kituo cha kuhifadhi na kukandamiza taka katika eneo la Mtoni, alisema licha ya kuwa kiungo muhimu kati ya wakusanyaji na soko, wanakabiliwa na changamoto ya mtaji na ukosefu wa soko la uhakika.

“Ninanunua maelfu ya kilo kwa wiki kutoka kwa wakusanyaji, lakini changamoto kubwa ni kwamba Zanzibar hakuna kiwanda kikubwa cha kuzirejeleza. Gharama ya usafiri inakula faida yote. Tukipata mkopo nafuu na mashine ya kusaga hapa Zanzibar, tutaweza kuwalipa wakusanyaji bei nzuri na kuchochea vijana wengi kuingia kwenye kazi hii,” amesema Hadija.

Meneja wa Mpango wa Ustahimilivu wa Pwani na Bahari wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) Tanzania, Joseph Olila, anasema lengo la jukwaa hilo ni kubadilisha mtazamo wa dhihaka dhidi ya wakusanyaji taka na kuwafanya watambulike kama mabingwa wa mazingira.

“Kila siku wanakusanya plastiki ambazo vinginevyo zingeishia kwenye mitaro yetu, fukwe na baharini. Ni wakati wa kuwatambua kama wafanyakazi wa mazingira, si wachafu,” anasema Olila.

Kwa upande wake, Ofisa wa Kitaifa wa Mradi wa IslandPlas, Genoveva Feksi, anasema bado kuna changamoto kubwa ya kimazingira na matokeo ya utafiti yaliyoonyesha uzalishaji wa tani 663 za taka kwa siku ndiyo yamechochea juhudi za kuwawezesha wakusanyaji na kuimarisha ushirikiano katika sekta ya urejelezaji.

“Tunataka kuondoka kwenye dhana ya ‘tupa na sahau’ kwenda kwenye ‘kusanya na pata kipato’. Ndiyo maana tunasukuma dhana ya uchumi wa mzunguko,” anasema Genoveva.

Naye, ofisa kutoka Baraza la Taifa la Biashara Zanzibar (ZNCC), Mussa Issa Ramadhan, anasema baraza hilo sasa linawatambua rasmi wakusanyaji na wafanyabiashara wa taka kama sehemu muhimu ya sekta binafsi na injini ya uchumi wa kijani.

“Si tena kazi ya maskini, ni biashara inayoweza kuajiri maelfu ya vijana wa Unguja na Pemba ikiwa itawezeshwa kwa sera rafiki,” anasema Mussa.

Wadau wa mazingira wanaamini kuwa jukwaa hilo likiwezeshwa kupata vifaa vya kujikinga, mitaji midogo na bei elekezi ya plastiki, linaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa tani 543 za taka zinazoishia hovyo na kugeuza janga la plastiki kuwa fursa ya ajira.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Wizara ya Fedha tayari imekabidhi magari 26 ya usafirishaji na usimamizi wa taka ngumu kwa Wizara ya Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ.

Magari hayo yamenunuliwa kupitia Mradi wa Ukuzaji Uchumi wa Zanzibar (Big Z), ambao ulitiwa saini mwaka 2021 kwa mkopo wa Dola za Marekani milioni 150 kutoka Benki ya Dunia (WB), kupitia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri wa Fedha Zanzibar, Dk Juma Malik Akil, anasema mradi wa Big Z una vipengele vingi, vikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, masoko na maeneo ya vivutio vya utalii, huku usimamizi wa taka ngumu ukiwa miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele.

“Tumenunua magari lakini watumiaji sasa ni Wizara ya Serikali za Mitaa, mikoa, wilaya na halmashauri zote. Tunataka kuona Zanzibar inakuwa safi,” anasema Dk Akil.

Magari hayo yanajumuisha magari 11 ya kukandamiza taka (compactor), yenye uwezo wa kubeba tani 18 kila moja, pamoja na magari 15 ya tipa yenye uwezo wa kubeba tani nane kila moja. Jumla ya thamani yake ni Sh7.123 bilioni.

Anaongeza kuwa utunzaji mzuri wa magari hayo ni muhimu kwa sababu Benki ya Dunia na Serikali ya Muungano zinafuatilia thamani na matumizi ya mkopo huo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma endelevu ya usimamizi wa taka ngumu.

Kwa upande wake, Waziri wa Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Idrisa Kitwana Mustafa, anasema usafi wa mazingira ndio msingi mkuu wa maendeleo na kuvutia uwekezaji nchini.

“Maendeleo yote tunayoyataja, msingi wake ni usafi. Tunapozungumza kuhusu taka ngumu, naamini kesho na kesho kutwa Serikali ndiyo itakayokuwa na jukumu hilo. Tunajua namna ya kufikiri zaidi kadiri tutakavyoona nyumbani panavyokuwa safi,” alisema Kitwana.

Kwa mujibu wa Kitwana, juhudi za kuondoa taka zinaendelea na anaamini kuwa hali itabadilika katika muda mfupi ujao na huduma ya uzoaji taka itakuwa ya kuridhisha. Alisema changamoto kubwa ilikuwa ukosefu wa vitendea kazi, ambavyo sasa vimepatikana, huku jitihada nyingine zikiendelea.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *