Magereza kuboresha huduma za afya, yaandaa mpango wa bima kwa wafungwa
4 mins read

Magereza kuboresha huduma za afya, yaandaa mpango wa bima kwa wafungwa

Dodoma. Jeshi la Magereza Tanzania limeanza kuandaa utaratibu wa kutumia bima ya afya kwa wafungwa na mahabusu ili kupunguza gharama za matibabu, madeni yanayotokana na huduma hizo na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya ndani ya vituo vya magereza nchini.

Hatua hiyo inakuja wakati Jeshi hilo likiendelea kuboresha miundombinu ya afya, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, pamoja na kuimarisha rasilimali watu ili kuhakikisha wafungwa, mahabusu na jamii inayozunguka vituo vyake wanapata huduma bora.

Mkuu wa Jeshi la Magereza, Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP), Jeremiah Yoram Katungu, amesema rasimu ya andiko la matumizi ya bima ya afya kwa wafungwa na mahabusu imeandaliwa kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza wakati wa kufunga mkutano wa wataalamu wa afya wa Jeshi la Magereza juzi, Katungu alisema rasimu hiyo ipo katika hatua ya mapitio na maboresho kabla ya hatua zinazofuata.

Alisema mpango huo unalenga kukabiliana na changamoto za kugharamia matibabu ya wafungwa na mahabusu, huku juhudi nyingine zikiendelea kuboresha uwezo wa vituo vya magereza kutoa huduma za afya.

Wataalamu watakiwa kupunguza rufaa

Katungu pia aliwataka wataalamu wa afya wa Jeshi la Magereza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, weledi na uzalendo ili kuboresha huduma kwa wagonjwa na kupunguza rufaa za magonjwa yanayoweza kutibiwa katika vituo vyao.

Alisema kuimarisha huduma za afya ndani ya vituo kutasaidia kupunguza gharama zinazotokana na kupeleka wagonjwa katika hospitali nyingine, hatua inayotarajiwa pia kupunguza madeni ya matibabu.

“Niwatake wataalamu wa afya mkaboreshe utoaji wa huduma. Hiyo itasaidia kupunguza rufaa kwa yale magonjwa ambayo tunaweza kuyatibu katika vituo vyetu na kupunguza madeni ya matibabu ya wafungwa na mahabusu,” alisema Katungu.

Alibainisha kuwa Jeshi la Magereza linaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kutolea huduma, ununuzi wa dawa na vifaa tiba, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa wataalamu wa afya.

Kwa mujibu wa Katungu, Jeshi hilo lina wataalamu wa afya zaidi ya 700 waliopo katika maeneo mbalimbali nchini, ambao wana jukumu muhimu la kuhakikisha huduma zinapatikana kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Katika hatua nyingine, Katungu aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuahidi kusaidia ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Kati ya Jeshi la Magereza jijini Dodoma, pamoja na kuiwezesha kwa vifaa ili ianze kutoa huduma.

Alisema hospitali hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uwezo wa Jeshi la Magereza katika kutoa huduma za afya, huku akiwataka wataalamu kuhakikisha wanatimiza matakwa ya kitaaluma kwa kujisajili katika mabaraza husika na kuhuisha leseni zao.

Pia, alisisitiza umuhimu wa kupanga ununuzi wa dawa na vifaa tiba kwa kuzingatia bajeti iliyopo ili rasilimali zinazotengwa zitumike kwa ufanisi na kukidhi mahitaji ya vituo.

Kwa upande wake, Kamishna wa Fedha na Mipango wa Jeshi la Magereza, CP Chacha Bina Jackson, alieleza kuridhishwa na ongezeko la mapato yanayokusanywa katika zahanati za Jeshi hilo.

Jackson alielekeza kuendelea kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Huduma za Afya (GOTHOMIS) wakati maandalizi yakiendelea kwa ajili ya kuanza rasmi kwa mfumo wa TPS e-Hospital Management, ulioundwa na wataalamu wa teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) wa Jeshi la Magereza.

Alisema matumizi ya mifumo hiyo ni sehemu ya juhudi za kuboresha usimamizi wa huduma za afya na kuimarisha ufanisi katika uendeshaji wa vituo vya matibabu.

Naye Mkuu wa Sehemu ya Afya wa Jeshi la Magereza, SACP Nsajigwa Mwankenja, alisema mkutano huo umewajengea uwezo wataalamu wa afya katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Alisema mafunzo hayo yalihusisha wataalamu zaidi ya 200 kutoka vituo mbalimbali vya Jeshi la Magereza, yakiwa na lengo la kuboresha ujuzi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya.

Juhudi hizo zinaelezwa kuwa sehemu ya mkakati wa Jeshi la Magereza wa kuimarisha huduma za afya kwa wafungwa na mahabusu, huku likiboresha usimamizi wa gharama za matibabu na kuongeza uwezo wa vituo vyake kuhudumia wagonjwa.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *