Mangapwani kuwa kitovu cha mapato ya forodha
2 mins read

Mangapwani kuwa kitovu cha mapato ya forodha

Unguja. Waziri wa Fedha wa Tanzania, Khamis Mussa Omar amesema Bandari Jumuishi ya Mangapwani inatarajiwa kuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa nchi baada ya kukamilika kwa ujenzi wake.

Kutokana na matarajio hayo, amezitaka taasisi zinazohusika na utoaji huduma bandarini, ikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), kuanza maandalizi mapema kwa kuhakikisha vifaa muhimu kama skana vinapatikana na watumishi wanaandaliwa ili huduma zianze kutolewa kwa ufanisi bila kuchelewa.

Omar ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Oktoba 26, 2026, alipotembelea bandari hiyo iliyopo Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja, kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo.

Amesema ili bandari hiyo ifanye kazi kwa ufanisi, ni lazima watoa huduma wawe wamejiandaa kabla ya kukamilika kwa miundombinu yake.

“Bandari hii inatazamiwa kuwa kituo muhimu sana kwa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania na chanzo kikubwa cha mapato ya forodha punde mradi huo utakapokamilika,” amesema.

Amesisitiza kuwa, maandalizi ya vifaa na watumishi hayapaswi kusubiri hadi ujenzi utakapokamilika, akizitaka taasisi husika kuhakikisha kila kitu kinakuwa tayari kwa wakati.

“Ni muhimu kwa watoa huduma wote kuwa tayari. Isifike wakati miundombinu imekamilika ndipo waanze kutafuta vifaa na watumishi. Jiandaeni mapema ili kuwa tayari,” amesema.

Amesema TRA na ZPC zinapaswa kupanga ratiba ya pamoja ili kuratibu uwekezaji unaohitajika na kuhakikisha huduma bandarini zinatolewa kwa ufanisi baada ya mradi kukamilika.

Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya taasisi hizo ni muhimu katika kuweka mipango madhubuti itakayowezesha utoaji wa huduma bora kwa wakati na bila kusuasua.

Mkurugenzi Mkuu wa ZPC, Akif Ali Khamis amesema ujenzi wa bandari hiyo umefikia asilimia 20 na unatarajiwa kukamilika Septemba 2028, kabla ya kukabidhiwa kwa Serikali.

Akif ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Tanzania kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi huo, akisema unatarajiwa kuifanya bandari hiyo kuwa kitovu cha biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Amesema katika awamu ya kwanza, bandari hiyo inatarajiwa kuhudumia kontena 250,000 kwa mwaka, zinazopimwa kwa kipimo cha TEUs, pamoja na tani milioni moja za mizigo kwa mwaka. Pia itakuwa na uwezo wa kupokea meli kubwa.

Bandari Jumuishi ya Mangapwani ni mradi wa kimkakati wenye thamani ya Dola 300 milioni za Marekani, uliozinduliwa na Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi, Machi 2026.

Mradi huo unatarajiwa kupunguza msongamano katika Bandari ya Malindi, ambayo ilianza kutumika mwaka 1920, na kuongeza uwezo wa Zanzibar kuhudumia shughuli za biashara na usafirishaji wa mizigo.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *