Jiwe la kihistoria lililotumika kuficha ng’ombe za Wapare dhidi ya wavamizi wa mifugo
4 mins read

Jiwe la kihistoria lililotumika kuficha ng’ombe za Wapare dhidi ya wavamizi wa mifugo

Mwanga. Katika kitongoji cha Kwaanjili, Kijiji cha Mbambua, Kata ya Lembeni, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, lipo jiwe kubwa lenye pango lililotumika miaka ya 1800’s kama maficho ya mifugo ya Wapare dhidi ya wavamizi waliokuwa wakitaka kuiba mifugo yao.

Jiwe hilo, ambalo limebaki kuwa alama ya historia ya jamii ya Wapare, linatajwa kuwa sehemu muhimu iliyotumiwa na wazee wa zamani kuhifadhi mifugo yao na kujilinda dhidi ya uvamizi, hasa kutoka kwa watu waliotajwa katika simulizi za wenyeji kuwa Wamasai.

Akizungumza  na Mwananchi  kuhusu historia ya jiwe hilo lenye uwezo wa kuhifadhi ng’ombe 60 kwa wakati mmoja,  mmoja wa wazee wa kijiji hicho, Mkumba Mvungi,  amesema wakati wa miaka hiyo mifugo ilikuwa rasilimali muhimu kwa jamii, hivyo Wapare walilazimika kutumia mbinu mbalimbali kuilinda dhidi ya wavamizi.

Anasema pango hilo lilikuwa miongoni mwa maeneo yaliyowasaidia kuhifadhi mifugo yao wakati wa mashambulizi, huku wao wakitumia nafasi ya juu ya jiwe kufuatilia mienendo ya watu waliokuwa wakikaribia eneo hilo.

Mmoja wa wazee wa kijiji cha Mbambua, Mkumba Mvungi, akionyesha jiwe lenye lango lenye uwezo wa kihifadhi ngombe zaidi ya 60.

“Zamani vita zilipoanza na watu wakija kuchukua ng’ombe wa Wapare, wenyeji walikuwa wakikimbilia hapa na kuingiza mifugo yao ndani ya pango hili. Walifunga kwa mawe ili kuzuia mifugo isionekane wala kuchukuliwa,” anasema mzee  Mvungi

Anaeleza kuwa,  baada ya kuficha mifugo ndani ya pango, baadhi ya watu walipanda juu ya jiwe hilo ili kuwaona wavamizi walipokuwa wakikaribia na kujipanga kukabiliana nao.

Anasema nafasi ya juu ya jiwe iliwapa wenyeji faida ya kuwaona waliokuwa chini, huku wavamizi wakipata ugumu wa kuwafikia kutokana na mazingira ya eneo hilo.

Kwa mujibu wa Mvungi, pango hilo lilikuwa na uwezo wa kuhifadhi takribani ng’ombe 60 kwa wakati mmoja, jambo linaloonyesha umuhimu wake katika kulinda mifugo iliyokuwa sehemu ya maisha na uchumi wa jamii hiyo.

Anasema wakati huo familia nyingi zilikuwa na mifugo mingi, hivyo eneo hilo lilikuwa msaada mkubwa kwa wazee waliotafuta namna ya kuokoa mali zao wakati wa hatari.

Amesema kwa sasa, pango hilo limebaki kuwa sehemu ya urithi wa kihistoria inayokumbusha maisha ya Wapare wa zamani, mbinu walizotumia kujilinda na namna walivyothamini mifugo yao.

Mmoja wa wazee wa kijiji cha Mbambua, Mkumba Mvungi, akionyesha jiwe lenye lango lenye uwezo wa kihifadhi ngombe zaidi ya 60.

Mzee mwingine, Yohana Mcharo, anasema jiwe hilo lilikuwa sehemu muhimu ya kujisitiri wakati wa uvamizi, kwani lilitoa nafasi kwa wenyeji kuficha mifugo yao na kufuatilia mienendo ya watu waliokuwa wakikaribia eneo hilo.

Anasema wazee wa wakati huo walikuwa wakitumia maarifa ya mazingira yao kujilinda, hasa kutokana na hofu ya kuporwa mifugo iliyokuwa tegemeo la maisha yao.

Anasema pango hilo lilikuwa na nafasi ya kutosha kuhifadhi mifugo mingi kwa wakati mmoja, hali iliyowasaidia wenyeji kupata mahali pa kujisitiri wakati wa hatari.

Anasema simulizi za matumizi ya pango hilo zimeendelea kuhifadhiwa na wenyeji kutoka kizazi kimoja hadi kingine, zikikumbusha namna wazee wa eneo hilo walivyotumia pango hilo kusitiri mifugo yao.

Mwonekano wa nje wa jiwe kubwa lenye pango lililotumika miaka ya 1800’s kama maficho ya mifugo ya Wapare dhidi ya wavamizi waliokuwa wakitaka kuiba mifugo yao.

Mtunza Makumbusho ya Wapare, Elia Mgaya, anasema makumbusho hayo yana jukumu la kuhifadhi historia inayofafanua maisha ya jamii hiyo, mila zake na shughuli mbalimbali zilizokuwa zikifanyika katika vipindi tofauti.

Anasema makumbusho hayo yana vifaa na zana mbalimbali zilizotumiwa na Wapare katika shughuli za kilimo na maisha ya kila siku, pamoja na vifaa vilivyohusika katika shughuli zao za kijamii.

Kwa mujibu wa Mgaya, kuhifadhi historia ni njia ya kuwakumbusha watu maisha waliyoishi wazee wao, kuelewa mbinu walizotumia kukabiliana na changamoto na kuenzi mambo mazuri yaliyofanyika katika vizazi vilivyotangulia.

Anasema maeneo ya kihistoria kama pango hilo yana umuhimu kwa sababu yanaunganisha jamii ya sasa na simulizi za maisha ya zamani, hivyo yanastahili kutambuliwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Amesema, pango hilo linabaki kuwa ushahidi wa simulizi za wenyeji kuhusu namna Wapare walivyotumia mazingira yaliyowazunguka kulinda mifugo yao, wakati ambapo mifugo ilikuwa miongoni mwa alama muhimu za utajiri na ustawi wa familia.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *