Mfanyakazi wa ndani ashikiliwa kwa tuhuma za kumuua mtoto wa mwajiri wake
2 mins read

Mfanyakazi wa ndani ashikiliwa kwa tuhuma za kumuua mtoto wa mwajiri wake

Geita. Jeshi la Polisi mkoani Geita linamshikilia Verediana Levee, mfanyakazi wa ndani, kwa tuhuma za kumuua William Mathayo, mwenye umri wa miaka mitano, aliyekuwa mtoto wa mwajiri wake.

Mtoto huyo alidaiwa kuuawa kwa kunyongwa Oktoba 24, 2026, katika Mtaa wa Ibolelo, Kata ya Nyankumbu, Manispaa ya Geita, wakati wazazi wake wakiwa nje kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Oktoba 26, 2026 na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Safia Jongo, tukio hilo lilitokea saa 4:00 asubuhi, wakati mtoto huyo akiwa amelala kitandani.

Kamanda Jongo amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya kukamilika kwa taratibu.

Amesema chanzo cha tukio hilo kinahusishwa na imani za kishirikina, huku kukiwa na madai kuwa mtuhumiwa alikuwa amepandwa na mapepo wakati akitekeleza kitendo hicho.

“Mtuhumiwa alimvizia mtoto huyo akiwa amelala na kumkaba shingo hadi alipofariki dunia. Wakati tukio linatokea, wazazi wake hawakuwepo nyumbani kwa kuwa walikuwa wamekwenda kwenye shughuli mbalimbali,” amesema Kamanda Jongo.

Ameongeza kuwa mtuhumiwa anadaiwa kuwa katika hali isiyo ya kawaida wakati wa tukio hilo.

Akizungumzia tukio hilo, baba wa mtoto aliyeuawa, Mathayo Valence, amesema familia yake ilikuwa imeishi na mfanyakazi huyo kwa miezi miwili.

Tukio hilo limeibua mjadala kuhusu tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa na waajiri wanapotafuta wafanyakazi wa ndani, huku baadhi ya wananchi wakishauri kufuatilia taarifa na historia za watu wanaoajiriwa.

Matukio matatu ya vifo vya kujinyonga yaripotiwa

Katika hatua nyingine, Kamanda Jongo amesema matukio matatu ya vifo vya watu kujinyonga yameripotiwa mkoani Geita kati ya Oktoba 17 na 26, 2026.

Amesema tukio la kwanza lilitokea Oktoba 17, 2026, likimhusisha Isack Ibrahimu, mwenye umri wa miaka 36, mkazi wa Makurugusi, Wilaya ya Chato, aliyekutwa amefariki dunia baada ya kujijeruhi shingoni na tumboni kwa kutumia kitu chenye ncha kali.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chanzo cha tukio hilo kinadaiwa kuwa msongo wa mawazo unaohusishwa na ugumu wa maisha.

Tukio la pili lilitokea Oktoba 21, 2026, likimhusisha Timotheo Chande, mwenye umri wa miaka 21, aliyekuwa dereva wa bajaji na mkazi wa Mtaa wa Moringe, Kata ya Kalangalala, Manispaa ya Geita.

Chande alikutwa amefariki dunia nyumbani kwao baada ya kujinyonga, huku chanzo cha tukio hilo kikihusishwa na msongo wa mawazo unaotokana na changamoto za mapenzi.

Tukio la tatu liliripotiwa Oktoba 26, 2026, likimhusisha Japhet Ladislaus, mwenye umri wa miaka 19, mkazi wa Mtaa wa Mbabani, Kata ya Mtakuja, ambaye alikutwa amefariki baada ya kujinyonga nje ya nyumba yao.

Kamanda Jongo amesema chanzo cha tukio hilo kinadaiwa kuwa msongo wa mawazo unaohusishwa na changamoto za mahusiano.

Amesema miili ya marehemu ilifanyiwa uchunguzi wa kitaalamu kabla ya kukabidhiwa kwa ndugu zao kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *