Zanzibar kuingiza dagaa kwenye lishe shuleni
2 mins read

Zanzibar kuingiza dagaa kwenye lishe shuleni

Unguja. Mfumo wa sasa wa chakula katika shule nyingi kisiwani Zanzibar umetajwa kukabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa virutubisho vidogo vinavyohitajika kwa ukuaji na afya ya wanafunzi.

Shule nyingi zimekuwa zikitoa chakula chenye wanga pekee, kama vile uji wa mahindi au ulezi, ambao unatoa nishati na nguvu pekee, lakini hauna virutubisho vya kutosha.

Ili kukabiliana na changamoto hii, shirika la utafiti la WorldFish, kwa kushirikiana na wadau wa Zanzibar, limeanzisha mkakati wa kuhamasisha uingizaji wa vyakula vya baharini na viumbe vya majini katika programu za lishe shuleni.

Akizungumza katika mkutano wa wadau wa kujadiliana mpango huo leo Oktoba 26, 2027, Mwanasayansi Mwandamizi kutoka Worldfish, Netsoyi Mudege amesema mkakati huu unalenga kuanza kwa kujumuisha protini za samaki kwenye uji na milo ya wanafunzi ili kuongeza thamani ya lishe na kupambana na udumavu.

Amesema utafiti uliofanywa Juni na Julai ulihusisha mahojiano katika shule 29 zilizofanyiwa utafiti, pamoja na wasindikaji wa samaki 380, wauzaji vyakula, walimu, na maofisa wa serikali.

“Matokeo ya utafiti huo yalionyesha kuwa ni shule mbili tu kati ya 29 zilizokuwa zikiwapa wanafunzi chakula chenye samaki,” amesema.

Licha ya kuwa karibu shule zote zilionyesha nia ya kutoa samaki, utoaji huo unakabiliwa na changamoto za wasiwasi kuhusu usalama wa chakula, mzio na ukosefu wa majokofu ya kuhifadhia samaki wabichi.

Kutokana na changamoto hizo, utafiti ulibaini kuwa matumizi ya dagaa waliokaushwa au unga wa dagaa ndiyo suluhu sahihi na rahisi zaidi kujumuishwa mashuleni.

“Unga wa dagaa unaweza kuchanganywa moja kwa moja kwenye uji wa shule kupitia mapishi maalumu yaliyobuniwa ili kuwa yenye lishe na ladha inayowavutia watoto,” amesema

Tofauti na samaki wakubwa, dagaa huliwa wakiwa wakamilifu pamoja na mifupa na viungo vya ndani, na hivyo kutoa virutubisho vingi kama vile vitamini A, kalsiamu, iodini, na Omega- vinavyosaidia ujenzi wa ubongo na afya ya akili.

Katika kuunga mkono jitihada hizi, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Maandalizi na Msingi, Fatma Mode Ramadhani alieleza kuwa Serikali inasimamia mradi wa chakula na lishe katika shule za maandalizi zaidi ya 322 zinazopata uji.

Katika shule hizo, shule 55 zinaendeshwa kupitia mradi maalum ambapo watoto wanapatiwa uji uliochanganywa na viazi lishe na mboga mboga, na sasa jitihada zinafanyika kuingiza dagaa.

“Serikali ipo katika mpango wa kuongeza shule zingine 15 ili kufikia shule 70 zilizopo maeneo ya mbali yenye changamoto kubwa za lishe na mahudhurio,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Maliasili za Baharini Zanzibar (Zafiri), Dk Zakaria Ali Khamis alibainisha kuwa Mzanzibari anakula wastani wa kilo 29 hadi 30 za samaki kwa mwaka, na zaidi ya asilimia 80 ya protini ya wanyama inatoka baharini.

Zakaria aliongeza kuwa tafiti zinaonyesha watoto wengi kati ya miaka mitatu na 14 wanakabiliwa na ukosefu wa virutubisho mwilini unaoweza kuathiri ufaulu wao wa masomo ya sayansi na hisabati.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *