Mabadiliko tabianchi yatishia rasilimali za bahari Zanzibar
Unguja. Mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira vinatishia rasilimali za bahari Zanzibar, huku kiwango cha mmomonyoko wa fukwe na ardhi kinachochangiwa na bahari kikiwa miongoni mwa viwango vya juu zaidi duniani.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Richard Muyungi, usiku wa kuamkia leo Jumanne, Oktoba 27, 2026, wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo kwa vinara wa mazingira iliyofanyika Unguja.
Tuzo hizo zimeandaliwa na Muungano wa Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar (ZACCA), ambapo washindi 20 wametambuliwa katika nyanja mbalimbali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Muyungi amesema maeneo ya Zanzibar, yakiwemo Nungwi, yamekuwa yakikabiliwa na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi ikilinganishwa na maeneo mengine mengi duniani.
“Katika maeneo kama vile Nungwi na maeneo mengine mengi Zanzibar, athari za mabadiliko ya tabianchi zimekuwa kubwa kuliko maeneo mengi duniani,” amesema.
Amesema hali hiyo inatishia utajiri wa rasilimali za bahari zilizopo Zanzibar, ambako kunapatikana asilimia 30 ya viumbe vya baharini na asilimia 60 ya matumbawe yote nchini.
Aidha, amesema Zanzibar ina hekta 45 za miamba ya matumbawe na ni kinara barani Afrika katika kilimo cha mwani.
Dk Muyungi amesema pamoja na mikakati inayotekelezwa na Serikali kukabiliana na changamoto hizo, juhudi zaidi zinahitajika kwa kuwa hatua zilizopo bado hazitoshelezi kukabiliana na ukubwa wa tatizo.
Ametaja baadhi ya hatua zinazochukuliwa kuwa ni ujenzi wa kuta za kuzuia mmomonyoko wa udongo katika Kisiwa cha Panza, Pemba, pamoja na maeneo ya Sikweze na Uusha. Hatua nyingine ni ujenzi wa vivunja mawimbi katika maeneo yaliyoathirika.
Kuhusu fedha za kukabiliana na changamoto hizo, Dk Muyungi amesema Serikali inaelekeza takribani asilimia tano hadi 10 ya bajeti yake katika sekta mbalimbali kwa ajili ya afua za mazingira na mabadiliko ya tabianchi, bila kutaja kiwango halisi cha fedha kinachotengwa.
“Pia, Serikali inajitahidi kutafuta fedha kutoka vyanzo vya kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuanza mchakato wa awamu ya tisa wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF), ambapo miradi mbalimbali kutoka Zanzibar imewasilishwa,” amesema.
Amesema hatua zinazochukuliwa kwa sasa bado haziendani kikamilifu na ukubwa wa tatizo linaloendelea kukua, lakini zinalenga kuweka mwelekeo wa kukabiliana nalo na kuhamasisha taasisi za fedha pamoja na wadau wa maendeleo kuongeza ushirikiano na Serikali.
Vijana na fursa za kiuchumi
Katika hatua nyingine, Dk Muyungi amesema Serikali inatilia mkazo ushirikishwaji wa vijana na wabunifu katika usimamizi wa mazingira.
Amesema kupitia Muungano, vijana wamekuwa wakipewa fursa na kuwezeshwa kushiriki katika mikutano ya kimataifa ya mabadiliko ya tabianchi ili kuongeza uelewa wao na kuimarisha uwakilishi wao katika mijadala inayohusu mazingira.
Pia, ameeleza kuwa biashara ya kaboni na ubunifu wa miradi mbadala ni miongoni mwa fursa zinazoweza kutumiwa na vijana kujipatia kipato huku wakichangia uhifadhi wa mazingira.
“Hekta moja ya mikoko ina uwezo wa kuhifadhi takribani tani 123 za kaboni, na kwa kuwa nchi ina maelfu ya hekta za mikoko, hii ni fursa kubwa ya kiuchumi na kimazingira inayoweza kutumiwa na vijana,” amesema Dk Muyungi.
Naye Mrajisi wa Asasi za Kiraia Zanzibar, Dk Ahmed Khalid Abdullah, ameiomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuziunganisha asasi za kiraia zilizopo Zanzibar na mashirika ya kimataifa ili ziweze kusaidiwa kupata vitendea kazi vya kukabiliana na changamoto za mazingira.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ZACCA, Dk Mahfoud Haji, amesema utoaji wa tuzo hizo unalenga kutambua mchango wa watu binafsi, taasisi na kampuni katika utunzaji wa mazingira, pamoja na kuhamasisha ushiriki zaidi katika juhudi za uhifadhi.
Amesema kongamano lililoandaliwa sambamba na tuzo hizo limewakutanisha wadau wa mazingira kwa lengo la kutoa elimu na kuweka mikakati ya kuimarisha utunzaji wa mazingira.

