Polisi Dodoma yawahakikishia usalama wanaofanya biashara usiku
Dodoma. Wakati wafanyabiashara mkoani Dodoma wakihamasika kufanya biashara usiku, Jeshi la Polisi limeahidi kuimarisha usalama huku likiwataka wazingatie sheria, utaratibu na masharti ya leseni zao.
Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera, hivi karibuni, huku akisema wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao usiku wanapaswa kuwa na leseni zinazowaruhusu kufanya biashara hizo na kuzingatia masharti yaliyowekwa.
Jijini Dodoma, leseni za biashara hutolewa na Halmashauri ya Jiji ambazo huwa na masharti ya ukomo wa muda wa kufunga biashara ambao unaelekezwa, mathalani kwenye masoko mwisho ni saa 12 jioni, wakati maeneo ya kuuzia vinywaji muda wa kufunga hufikia hadi saa 5 usiku.
Kamanda Hyera amesema ni muhimu kila mfanyabiashara kuzingatia muda alioruhusiwa kufanya biashara na kutokiuka masharti ya leseni yake aliyokabidhiwa kwani kinyume na hapo ni uvunjifu na ukiukwaji wa misingi ya amani.
“Uzingatiaji wa masharti hayo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha shughuli za kiuchumi zinaendelea kwa utaratibu, huku usalama wa wafanyabiashara na wananchi wengine ukilindwa. Kwa hiyo, hatukatai kufanya biashara usiku, lakini tunahitaji watu wawe na amani kwanza,” amesema Hyera.
Kamanda Hyera ametaja changamoto ambazo mfanyabiashara anaweza kukutana nazo kuwa ni pamoja na uporaji wa mali, uharibifu wa mali, ubakaji na matukio mengine yanayohatarisha usalama wao.
Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara wamesema wanalazimika kufunga biashara mapema ili kujiepusha na vitendo vya uhalifu vinavyoweza kujitokeza wakati wa usiku wanapoendelea na biashara a zao.
Akizungumza na Mwananchi, mfanyabiashara wa matunda kwenye kituo cha mabasi jijini Dodoma, Bahati Mpemba amesema changamoto kubwa inayowakabili wafanyabiashara ni usalama mdogo katika maeneo yao, hali inayowafanya baadhi yao kuishi kwa hofu.
Mpemba amesema wakati mwingine hulazimika kufunga biashara kabla ya muda waliopanga, hata kama bado kuna wateja wanaohitaji huduma zao.
“Wakati mwingine unalazimika kufunga biashara mapema kwa sababu ya hofu ya wizi na vitendo vingine vya kihalifu, licha ya kuwa bado kuna wateja na kama mnavyojua biashara wakati huo huwa imechanganya lakini kwa kweli unaangalia hivi umeme ukizima tutafanyaje,” amesema Mpemba.
Hata hivyo, amekiri kuwa biashara za usiku zina faida kutokana na kuongezeka kwa wateja wanaotoka kazini na kununua matunda kwa ajili ya familia zao, matumizi binafsi au kutengeneza juisi kwa ajili ya biashara.
Kwa upande wake, mfanyabiashara wa vinywaji, Hellena Kojesa amesema muda wa usiku una fursa kubwa na mazingira mazuri ya kibiashara kwa kuwa watu wengi hutembelea maeneo ya burudani baada ya kutoka kazini.
Hellen amesema wateja huongezeka zaidi nyakati ambazo watu wanahitaji kupumzika na kujiburudisha baada ya shughuli za siku nzima.
Kwa upande mwingine, amesema mikusanyiko ya watu, hasa wakati wa mechi za mpira wa miguu, inaweza kusababisha changamoto pale baadhi ya mashabiki wanaposhindwa kudhibiti hisia zao baada ya kupata matokeo mabaya kwa timu wanazoshabikia.
Mfanyabiashara huyo amesema wakati mwingine usiku huchochea ugomvi, uharibifu wa mali na mapigano yanayohusisha chupa za vinywaji, huku wateja wengine wakiibiwa mali zao na ama kukimbia na madeni ya mwenye nyumba
“Biashara huwa nzuri kwa sababu wateja wanaongezeka, lakini changamoto inatokea pale baadhi ya watu wanapokunywa kupita kiasi na kuanza kugombana au kuharibu mali. Wakati mwingine watu waliopo karibu wanaweza kuathirika,” amesema.
Naye, Joseph Mushi, mfanyabiashara katika Stendi ya Mkoa wa Dodoma, amesema ni muhimu kuwepo kwa mikakati ya kuimarisha usalama katika maeneo ya biashara ili kuwawezesha wafanyabiashara kunufaika na fursa hizo bila kuhatarisha maisha na mali zao.

