Kabudi aagiza watumishi waachie majengo ya kupanga, waende Mtumba
Dodoma. Serikali imeagiza watumishi wa Serikali ambao walikuwa wamepanga kwenye majengo mengine ya umma kuyaachia na kurudi katika majengo yao yaliyopo mji wa Serikali Mtumba.
Agizo hilo limetolewa leo Jumanne na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi wakati akitoa taarifa ya uzinduzi rasmi wa Mji wa Serikali Oktoba 30,2026.
Waziri Profesa Kabudi amesema mara baada ya tangazo la Serikali kuhamia Dodoma, baadhi ya taasisi zake zililazimika kupanga katika majengo mengine ikiwemo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambapo sasa majengo yao yamekamilika na wanatakiwa kuanza kuyatumia.
Rais Samia Suluhu Hassan atazindua mji huo ambao tamko lake lilitolewa na Rais wa awamu ya kwanza Mwalimu Nyerere mwaka 1973 na Serikali imekuwa ikihamia kwa awamu, lakini ilipofika awamu ya tano kasi ya kuhamia Dodoma ikawa kubwa na ndipo ikatungwa sheria rasmi ya kuitambua Dodoma kama makao makuu ya nchi.
“Lilipotolewa agizo na shughuli za ujenzi wa awamu ya kwanza zilianza Novemba 28,2018 ambapo Jumla ya Sh39.39 bilioni zilitumika, leo majengo yamefikia zaidi ya asilimia 99 baada ya kutumia zaidi ya Sh940.8 bilioni kwenye awamu ya pili, sasa ni muda muafaka watumishi kuachia majengo yale na kwenda Mtumba,” amesema Profesa Kabudi.
Waziri amesema uzinduzi wa majengo majengo 37 yaliyopo Mtumba unakwenda sambamba na majengo mengine 35 yaliyojengwa nje ya mji wa Serikali lakini na barabara zenye urefu wa kilomita 57.1 ambazo zimegharimu zaidi ya Sh110.5 bilioni zote zikiwa ndani ya Mji wa Serikali.
Amesema uwekezaji mkubwa uliofanyika ndani ya mji wa Serikali unaweza kutosheleza zaidi ya miaka 30 ijayo na kwamba itakapobidi kufanya upanuzi bado kuna maeneo ambayo yamewekwa kwa akiba yatasaidia.
Hata hivyo Waziri amesema Serikali inakusudia kuchukua maeneo mengine kwa kuwalipa wananchi ili kuweka akiba ya baadaye katika upanuzi wa mji huo wakati ambapo idadi ya watu inaongezeka na kutarajia kuongeza miundombinu.
