Mchengerwa: Ubora wa dawa hautashushwa kwa ajili ya uwekezaji
Arusha. Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesema Tanzania haitakubali viwango vya dawa kuhatarishwa kwa sababu ya kutafuta wawekezaji wa viwanda vya kuzalisha dawa na vifaatiba nchini, akisisitiza kuwa mwekezaji lazima azingatie viwango vinavyotakiwa, ikiwamo vile vya Shirika la Afya Duniani (WHO).
Amesema sekta ya afya ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayobeba usalama wa Taifa kwa kuwa mamilioni ya Watanzania hutegemea dawa na huduma zinazotolewa katika vituo vya afya na hospitali nchini.
Mchengerwa amesema hayo leo Jumanne Oktoba 27,2026 akizungumza Arusha katika kongamano la kisanyasi na mkutano mkuu wa 27 wa Chama cha Wanateknolojia Dawa Tanzania (Taphata), unaoongozwa na kauli mbiu “Kukuza viwanda vya dawa Tanzania kwa ajili ya afya bora,ajira endelevu na uchumi imara”.
Waziri huyo amesema Tanzania inaendelea kusukuma ajenda ya kuongeza uzalishaji wa dawa na bidhaa za afya ndani ya nchi, lakini amesisitiza kuwa hatua hiyo lazima iende sambamba na uadilifu, ubora na usalama wa dawa zinazozalishwa.
Amesema uwekezaji katika viwanda vya dawa unahitaji wataalamu wenye uwezo katika uzalishaji, uhakiki wa ubora, usimamizi wa mnyororo wa ugavi, utafiti na ubunifu na kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha uliopita Watanzania milioni 43 walipata huduma katika vituo vya afya na hospitali mbalimbali nchini, hivyo ubora na usalama wa dawa ni suala lisilopaswa kuathiriwa na maslahi ya uwekezaji.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, akizungumza leo Jumanne, Oktoba 27, 2026, jijini Arusha katika kongamano la kisayansi na mkutano mkuu wa 27 wa Chama cha Wanateknolojia ya Dawa Tanzania (TAPHATA).
“Sasa ukiwa na mmomonyoko wowote wa uadilifu kwenu ninyi vijana, maana yake kazi tutakayokuwa tumewatuma katika viwanda hivi vitavyojengwa leo, ninyi mtashindwa kwenda kuitekeleza ipasavyo kwa sababu mtakuwa mme-compromise.”
“Na sisi tumesema, hata akija nani kuwekeza hapa nchini, viwango vya uwekezaji unaotakiwa kwa mujibu wa taratibu za WHO kamwe hatuwezi kuruhusu vi-compromise, hata kama mwekezaji atakuja na shilingi ngapi,” amesema na kuongeza;
“Kwa hiyo, yako mambo ya msingi ambayo mimi na wewe ni lazima tuyazingatie. Hata kama tutakuwa tunahitaji pesa kiasi gani, haya ya msingi katika Taifa kamwe tusiruhusu mmomonyoko wa maadili kwenu vijana wa famasia ambao tutawategemea kwenda kusimamia viwanda hivi uingie katika fikra za vichwa vyenu, fikra za mioyo yenu, lakini fikra za utendaji katika viwanda hivi tunavyovizungumza,” amesema.
Amewataka vijana wanaojiandaa kushiriki katika ujenzi na usimamizi wa viwanda hivyo kujenga msingi imara wa maadili, akisema mmomonyoko wa maadili unaweza kuhatarisha utekelezaji wa majukumu yao.
“Ukiwa na mmomonyoko wowote wa maadili kwenu vijana ambao tutawategemea kwenda kusimamia viwanda hivi, kazi tutakayowatuma mtaishindwa kuitekeleza ipasavyo,” amesema.
Amesema Tanzania inaweza kujifunza kutoka mataifa yaliyopiga hatua katika uzalishaji wa dawa, akitaja India, Bangladesh, China, Misri na Algeria.
Amesema uzoefu wa nchi hizo unaonyesha kuwa kujenga sekta imara ya dawa hakutegemei viwanda pekee, bali pia uwekezaji katika elimu, sheria, wataalamu na mifumo madhubuti ya udhibiti.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, wakati akipewa maelekezo leo Jumanne, Oktoba 27, 2026, jijini Arusha kabla ya kuzungumza katika kongamano la kisayansi na mkutano mkuu wa 27 wa Chama cha Wanateknolojia ya Dawa Tanzania (TAPHATA).
Amesema Tanzania ina soko kubwa la ndani pamoja na fursa katika masoko ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, hivyo vijana wanapaswa kuona fursa zaidi ya kuajiriwa na kuelekea katika ubunifu na uanzishaji wa viwanda vya dawa na kuwa itasaidia kutimiza lengo la Serikali kuhakikisha ifikapo 2030 inazalisha dawa kwa asilimia 80.
Amesema utekelezaji wa ajenda hiyo unahitaji pia wataalamu wenye maadili kwa sababu sekta ya dawa haiwezi kuvumilia uzembe, rushwa au ukiukwaji wa taratibu unaoweza kuhatarisha maisha ya wananchi.
Awali Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya nchini Tanzania anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Emmanuel Tayari, amesema Tanzania ina uwezo wa kujenga na kuendeleza viwanda vya dawa nchini.
Amesema hayo huku akitumia mifano ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya benki na madini kuonyesha namna wataalamu na kampuni za Kitanzania zilivyoweza kuimarika baada ya Serikali kufanya mageuzi.
“Wakati Tanzania inapozungumzia kujenga viwanda vya dawa na kufanya mabadiliko katika sekta hiyo, baadhi ya watu wanaweza kujiuliza kama nchi ina uwezo wa kufanya hivyo, lakini historia inaonyesha kuwa Tanzania imewahi kufanya mambo makubwa na kufanikiwa,” amesema
Ametoa mfano wa mageuzi yaliyofanyika katika sekta ya benki, akisema baada ya soko kufunguliwa kulikuwa na mashaka kuhusu uwezo wa Watanzania kuendesha sekta hiyo, lakini baadaye wataalamu na taasisi za ndani walionyesha uwezo mkubwa.
“Watu wengi walikuwa na maoni mbalimbali kwamba je, hawa Watanzania wataweza? Lakini leo ni mwaka 2026, benki zetu za Watanzania zinaongoza kwa faida Afrika Mashariki,” amesema.
Kuhusu sekta ya madini, amesema Tanzania imeweza kujenga utaalamu katika sekta hiyo na sasa wataalamu waliopata uzoefu nchini wamekuwa wakifanya kazi katika migodi mikubwa ndani na nje ya Tanzania.
Amesema mafanikio hayo yanapaswa kuwa sehemu ya somo kwa sekta ya dawa, hasa katika kujenga viwanda, kukuza wataalamu na kuongeza uwezo wa ndani wa kuzalisha bidhaa muhimu za afya.
Awali, Rais wa Taphata, Thabit Milandu, ameomba Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji katika uzalishaji wa dawa nchini ili kuongeza upatikanaji wa dawa salama na zenye ubora, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kuongeza ajira.
Amesema uzalishaji huo ni muhimu katika kuimarisha mfumo wa afya na uwezo wa nchi kukabiliana na milipuko ya magonjwa na kuwa vinapaswa kupewa kipaumbele, kwa kuwa vina nafasi ya kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wakati na kwa gharama zinazolingana na uwezo wa wananchi.
Amesema, kuongeza uzalishaji wa dawa nchini kutasaidia pia kuchochea tafiti, ubunifu wa teknolojia, uwekezaji, kuongeza thamani ya malighafi, kufungua masoko ya ndani na kimataifa pamoja na kuongeza ajira katika kada mbalimbali.

