Bibi Lotuno, miaka 104 ya maisha vizazi vinne vya familia
Arumeru. Kwa zaidi ya karne moja, Bibi Elisifa Lotuno ameishi kushuhudia mabadiliko ya maisha, ukuaji wa familia yake na kuibuka kwa vizazi vipya, safari oliyoanza Agosti 20, 1922 alipozaliwa na kufikia mwisho Oktoba 22, 2026, alipofariki dunia akiwa na umri wa miaka 104.
Mamia ya wakazi wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha na mji mdogo wa Mirerani, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, wamejitokeza kumuaga katika maziko yaliyofanyika Jumanne, Oktoba 27, 2026, nyumbani kwake katika Kijiji cha Mikungani, Arumeru.
Maisha yake marefu yameacha kumbukumbu ya familia kubwa yenye watoto wanane, wajukuu 100, vitukuu 62 na vilembwe watatu, huku watu waliomfahamu wakimwelezea kama mtu mwenye imani thabiti ya dini, ukarimu na upendo kwa wengine.
Miongoni mwa wajukuu zake ni msanii maarufu, Nakaya Sumary na mlimbwende Nancy Sumary.
Kwa mujibu wa historia ya maisha yake iliyosomwa na mmoja wa wajukuu zake, Jema Lilama, Bibi Lotuno aliyezaliwa Agosti 20, 1922 aliolewa mwaka 1944 akiwa na umri wa miaka 22 na kupata watoto wanane, watano kati yao wakiwa hai na watatu wakitangulia mbele ya haki. Lilama amesema familia inamshukuru Mungu kwa kumpa bibi huyo maisha marefu yaliyomwezesha kuona familia yake ikikua na kuendelea kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
“Tunamshukuru Mungu kwa kumjalia maisha marefu na nafasi ya kushuhudia kukua kwa familia yake kutoka kizazi kimoja hadi kingine,” amesema.
Msanii Nakaya Sumary (kushoto) akiweka shada la maua kwenye kaburi la marehemu bibi Elisifa Lotuno (104), aliyezikwa nyumbani kwake kijiji cha Mikungani wilayani Arumeru mkoani Arusha. Picha na Joseph Lyimo
Safari ya maisha iliyoanzia mwaka 1922
Katika kipindi cha maisha yake, marehemu alijishughulisha na ujasiriamali, ufugaji na kilimo, shughuli zilizokuwa sehemu muhimu ya maisha yake.
Lilama amesema bibi yake alibatizwa mwaka 1954 na aliendelea kushikamana na imani ya dini hadi mwisho wa uhai wake.
Hata hivyo, maisha yake hayakuwa bila changamoto za kiafya. Kwa mujibu wa Lilama, kuanzia mwishoni mwa mwaka 2001, Bibi Lotuno alianza kusumbuliwa na shinikizo la damu, matatizo ya moyo na maumivu ya viungo.
Amesema Bibi Lotuno alipatiwa matibabu katika Hospitali ya Moyo jijini Dar es Salaam na Kituo cha Afya Mirerani kabla ya kufariki dunia Oktoba 22, 2026.
Familia imetoa shukurani kwa madaktari na wahudumu wa Kituo cha Afya Mirerani kwa huduma na matunzo waliyompatia wakati wa matibabu yake.
Baadhi ya watoto wa marehemu bibi Elisifa Lotuno (104), wakiwa kwenye maziko ya mama yao yaliyofanyika kijiji cha Mikungani wilayani Arumeru mkoani Arusha. Picha na Joseph Lyimo
Ukarimu uliomfanya akumbukwe
Zaidi ya idadi ya vizazi alivyoacha, Bibi Lotuno anakumbukwa kwa tabia yake ya kushiriki na wengine kile alichokuwa nacho.
Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Mikungani, Mtaa wa Kairo, Ernest Kisanga, amesema Bibi Lotuno alikuwa mtu mkarimu aliyependa kushiriki chakula na watu wengine.
Amesema alikuwa na desturi ya kuweka chakula nje, chini ya mti, ili ale pamoja na wengine badala ya kujitenga ndani ya nyumba. Kisanga amesema Bibi Lotuno pia alikuwa mtu mwenye imani ya dini, akimwabudu Mungu tangu akiwa na umri mdogo hadi alipofariki.
Kwa upande wake, Mchungaji Msaidizi wa usharika huo, Ernest Mola, amesema Bibi Lotuno alikuwa na moyo wa kusaidia wengine na hakuwa mtu wa kuweka kinyongo.
Naye Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mirerani na Songambele, Sioni Mollel, amewataka waumini kuiga mfano wa maisha ya marehemu, akieleza kuwa aliishi miaka mingi huku akimtukuza Mungu na kuwa baraka kwa watu waliomzunguka.
Mchungaji Ernest Kisanga, akiongoza ibada ya maziko ya marehemu bibi Elisifa Lotuno (104), nyumbani kwake kijiji cha Mikungani wilayani Arumeru mkoani Arusha. Picha na Joseph Lyimo
Kwa majirani, Bibi Lotuno hakuwa tu mzee aliyeishi miaka mingi, bali pia mtu aliyependa kuimba, kucheka na kufurahia ukaribu wa familia yake.
Mmoja wa majirani wa familia hiyo, Orgenes Lekule, amesema Bibi Lotuno alipenda kuimba nyimbo za kumtukuza Mungu, kula vyakula vya asili na kufanya utani na wajukuu zake.
Amesema licha ya umri wake mkubwa, Bibi Lotuno aliendelea kufurahia mazungumzo na utani wa kifamilia.
Lekule amekumbuka tukio la hivi karibuni ambapo mtoto wa familia alimtania kwa kumwambia kuwa anapolala, watu wanamaliza kuku ndani ya nyumba.
“Alikuwa anapenda utani na wajukuu zake. Hivi karibuni alikuwa anataniwa na mtoto wa Lotuno akimwambia, ‘Bibi, wewe umelala watu wanamaliza kuku ndani.’ Anaamka na kukimbizana naye,” amesema.

