Rais Samia amteua Dk Mabula, amtengua Malisa
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, ametengua uteuzi wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Beno Malisa, huku akimteua Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula, kushika wadhifa huo.
Malisa, hadi anatenguliwa leo Jumatano, Oktoba 28, 2026 ameuongoza Mkoa wa Tabora kwa miezi miwili. Alihamishiwa hapo Agosti 27, mwaka huu akitokea Mkoa wa Mbeya.
Taarifa ya utenguzi wa Malisa na uteuzi wa viongozi wengine wanne imetolewa leo Oktoba 28,2026 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka na kutiwa saini na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Shaaban Kissu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Dk Mabula ameteuliwa kumrithi Malisa. Dk Mabula alikuwa Mbunge wa Ilemela hadi mwaka 2025, kabla ya hapo amewahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Dk Mabula aliukosa ubunge baada ya kutemwa katika mchujo wa ndani wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2025.
Wengine walioteuliwa kwa mujibu wa taarifa hiyo ni Dunford Mpelumbe kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Kabla ya uteuzi huo, Mpelumbe alikuwa Wakili wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na anachukua nafasi ya Jaji mstaafu, Mathew Mwaimu ambaye amemaliza muda wake.
Mwingine aliyeteuliwa ni Omar Ali Omar kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Kabla ya uteuzi huo, Omar alikuwa Mkuu wa Idara ya Utawala, Mipango na Fedha, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Karume, Zanzibar.
Omar anachukua nafasi ya Mohamed Khamis Hamad ambaye amemaliza muda wake.
“Uapisho wa viongozi wateule utafanyika kwa tarehe itakayopangwa baadaye,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

