Naibu Waziri aonya ubadilishaji holela wa maeneo ya wazi
3 mins read

Naibu Waziri aonya ubadilishaji holela wa maeneo ya wazi

Arusha. Serikali imeonya ubadilishaji holela wa matumizi ya maeneo ya wazi yaliyotengwa kwa huduma za umma, ikisema hali  hiyo inachochea uvamizi wa ardhi na migogoro.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya, amesema maeneo yaliyotengwa kwa matumizi ya umma yanapaswa kulindwa na kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa, badala ya kuruhusu watu kuyavamia na kujenga nyumba au kuanzisha biashara bila kufuata taratibu.

Akizungumza jijini Arusha leo Oktoba 28, 2026, katika mkutano mkuu wa 11 wa mwaka wa wataalamu wa mipango miji nchini ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji (TPRB), Mmuya amesema hakuna mamlaka inayopaswa kuruhusu mabadiliko ya matumizi ya ardhi bila kufuata taratibu za kisheria.

Amesema kumekuwa na tabia isiyokubalika ya baadhi ya watu kuvamia maeneo ya wazi, maeneo ya umma na maeneo hatarishi, hali inayoweza kuathiri utekelezaji wa mipango ya miji na matumizi bora ya ardhi.

“Msimamo wa Wizara ni kwamba maeneo ya wazi ndani ya nchi lazima yatumiwe kwa matumizi yaliyopangwa. Hatuwezi kupanga eneo kuwa la wazi leo, kesho mtu akaenda kujenga nyumba, baa au biashara nyingine kwa sababu tu anaona eneo hilo halina matumizi,” amesema.

Mmuya amesema endapo kutakuwa na sababu ya msingi ya kubadili matumizi ya eneo lililopangwa, mchakato huo lazima uanze katika halmashauri husika, wataalamu watoe ushauri na ombi lifuate taratibu zilizowekwa.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

 “Naomba tusitengeneze migogoro isiyokuwa na sababu. Serikali inatupa fedha tupange nchi yetu na wataalamu tunao wajibu wa kusimamia maendeleo yanayotokana na mipango tuliyopanga,” amesema.

Mmuya amezitaka mamlaka za upangaji, kuanzia vijiji hadi serikali za mitaa na wilaya, kuhakikisha maeneo hatarishi yakiwamo mabonde, kando ya mito, yaliyokumbwa na mafuriko hayatolewi kwa ajili ya makazi ya wananchi.

Amesema Tanzania inaendelea kukua kwa kasi na idadi ya watu wanaohamia mijini inatarajiwa kuongezeka, hivyo mipango ya miji inapaswa kuzingatia matumizi bora ya ardhi na ujenzi wa nyumba za ghorofa badala ya kuendelea kupanua miji kwa utaratibu wa nyumba moja moja bila kuzingatia mpango mpana wa maendeleo.

Pia, amewakemea watu wanaodaiwa kununua ardhi vijijini, kuchora viwanja na kuviuza kwa wananchi wakidai michoro hiyo imeidhinishwa na Wizara ya Ardhi, akisema vitendo hivyo vinapotosha wananchi na kuhatarisha juhudi za kupanga matumizi bora ya ardhi.

Awali, Kaimu Msajili wa TPRB, Martha Mkupasi, amesema bodi imeanza kuchukua hatua dhidi ya watu wasio na taaluma wanaojihusisha na kazi za mipango miji kinyume cha sheria, maarufu kama “vishoka”.

Mkupasi amesema hatua ya awali ni kuwatambua na kuwaelimisha watu hao kuhusu sheria na taratibu za taaluma, kabla ya kuchukua hatua zaidi kwa watakaokaidi.

Amesema kufikia lengo la kuwa na miji endelevu, jumuishi na shindani kunahitaji ubunifu, uwekezaji katika mifumo ya kidijitali na ushirikiano baina ya taasisi.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratias Kalimenze, amesema Tanzania ina upungufu wa zaidi ya asilimia 75 ya maofisa mipango miji wanaohitajika, hali inayoongeza mzigo wa kazi kwa waliopo.

Amesema kwa sasa ofisa mmoja wa mipango miji anahudumia zaidi ya watu 100,000, hivyo matumizi ya teknolojia yanaweza kusaidia kuongeza ufanisi wa huduma.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, amesema Mkoa wa Arusha unatambua mchango wa wataalamu wa mipango miji katika kuhakikisha ardhi inapangwa na kutumika kwa mujibu wa sheria.

Amewataka viongozi wa vijiji na mitaa kusimamia matumizi sahihi ya ardhi badala ya kutumia madaraka yao kujinufaisha.

 “Tupambane na wale watu maarufu wa 20 kwa 20, na naamini kwa kufanya hivyo sisi Arusha tutaendelea kuwa Geneva ya Afrika, kwa sababu maeneo yetu yatakuwa yamepangwa na matumizi ya ardhi yataendana na mipango tuliyoweka,” amesema.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *