Wadau: Wazazi, walezi wawasikilize watoto badala ya kuwahukumu
Dar es Salaam.Wadau wa elimu, saikolojia na malezi wamependekeza mambo matatu ya kupata suluhu dhidi ya watoto wenye changamoto za kimaadili ikiwemo kufanya mazungumzo kati yao na wazazi badala ya kuwahukumu wanapoonekana katika video zinazosambaa mitandaoni.
Mbali na hilo, kuimarisha ushauri nasaha shuleni na kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na kuwapa mkazo na msingi wa elimu ya maadili kuanzia wanapozaliwa hadi wanapofikisha miaka 12.
Wakichangia mjadala wa Mwananchi Space ulioandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL), Oktoba 28, 2026, wenye mada ‘Sherehe za kuhitimu shule zinapogeuka tatizo la maadili: Tatizo liko wapi na nini suluhisho?.
Wamesema kukabiliana na hali hiyo kunahitaji ushirikiano wa familia, shule na jamii katika kuwajengea watoto uwezo wa kufanya uamuzi sahihi, kuelewa athari za matendo yao na kukabiliana na shinikizo la marafiki, huku wakisema kuwashambulia au kuwahukumu hadharani kunaweza kuongeza changamoto badala ya kuwasaidia kubadilika.
Mhadhiri wa Idara ya Saikolojia na Mratibu wa Kitengo cha Ushauri na Unasihi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kampasi ya Mkwawa mkoani Iringa, Dk Nabwera Rashid, amesema hata watoto wanaoonekana katika video mitandaoni wanapaswa kuzungumzishwa na kusaidiwa kuelewa athari za matendo yao badala ya kuhukumiwa.
Amesema baadhi ya watoto hao huenda tayari wameathirika kisaikolojia kutokana na kusambaa kwa video hizo, hivyo ni muhimu jamii kuanza kwa kuwapa nafasi ya kueleza wanachopitia kabla ya kuchukua hatua nyingine.
“Baada ya kukaa nao pamoja, watoto hao na wengine wajengewe uwezo kwamba hawapaswi kuiga marafiki kwa kila wanachowaambia. Tuwafundishe kutambua faida na hasara za kutafuta umaarufu,” amesema.
Dk Rashid amesema watoto wanapaswa kuelewa kuwa kuhitimu elimu ya msingi au sekondari si mwisho wa maisha, hivyo ni muhimu kuzingatia uamuzi wanaofanya namna unavyoweza kuathiri maisha yao ya baadaye.
Amesema elimu ya maadili inapaswa kuwasaidia kutambua madhara ya vitendo vyao, ikiwamo kuchapisha maudhui kwenye mitandao ya kijamii bila kufikiria matokeo yake.
Amesema njia ya kuwasaidia watoto si kuishia katika kuwapa adhabu, bali ni kuwajengea uwezo wa kutofautisha yaliyo sahihi na yasiyo sahihi na kuwajibika kwa uamuzi wao. Kwa upande wake, mtafiti wa masuala ya elimu nchini, Dk Muhanyi Nkoronko, amesema kuongezeka kwa matumizi ya vifaa vya kidijitali bila usimamizi wa kutosha kunachangia baadhi ya wanafunzi kushiriki au kusambaza maudhui yasiyofaa kwenye mitandao ya kijamii.
Amesema watoto wanapokuwa katika umri wa kujaribu mambo mapya, wanaweza kushawishika kufanya vitendo fulani kutokana na shinikizo la marafiki au kutaka kupata umaarufu bila kuzingatia athari zake.
Dk Nkoronko amewashauri wazazi kufuatilia matumizi ya vifaa vya kidijitali kwa watoto wao na kuwapa elimu kuhusu namna ya kutumia mitandao ya kijamii kwa usalama na uwajibikaji.
Amesema usimamizi huo unapaswa kuambatana na mazungumzo yanayowawezesha watoto kuelewa sababu za kuwekwa kwa mipaka, badala ya kuwataka watii bila kuelewa madhara ya wanachokifanya.
Naye mshauri wa elimu, Mwalimu Magoda, amesema changamoto za maadili kwa watoto haziwezi kutatuliwa kwa kuelekeza lawama shuleni pekee, kwa kuwa malezi ya mtoto huathiriwa pia na familia na mazingira ya jamii anayoishi.
Amesema baadhi ya tabia zinazoonekana kwa wanafunzi zinaweza kuchochewa na mifano wanayoiona katika jamii, maudhui ya mitandaoni na watu wanaowavutia.
“Hawa watoto hivi vitu wanatoka navyo kwenye jamii. Ni ngumu sana kukuta shuleni wanapiga muziki au walimu wanatamka mambo yasiyofaa,” amesema.
Magoda ameshauri shule kuimarisha mifumo ya malezi, nidhamu na ushauri nasaha ili kuwasaidia wanafunzi kujenga misingi bora ya tabia kabla ya kujitokeza kwa changamoto.
Amesema walimu na wazazi wanapaswa kushirikiana katika kuwajenga watoto, huku wazazi wakitakiwa kuwa mifano bora kwa watoto wao kwa kuzingatia kuwa malezi hayaishii katika kuwapatia mahitaji ya msingi pekee.
Kwa upande wake, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka, amesema kuna tofauti kati ya kulea na kufuga watoto, akiwataka wazazi kutathmini namna wanavyotekeleza wajibu wao wa malezi.
Katika andiko lake lililowasilishwa kwenye mjadala huo, amesema malezi yanahusisha kumwongoza mtoto na kuandaa makuzi yake kisaikolojia, kijamii na kibaiolojia ili aweze kuwajibika katika jamii. Amesema kuwapatia watoto mahitaji ya msingi pekee hakutoshi, bali wazazi wanapaswa kushiriki katika kuwaongoza, kuwafuatilia na kuwasaidia kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo wanapokua.
Naye mhadhiri wa saikolojia katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Christian Bwaya, amesema elimu haipaswi kuishia katika kujenga uwezo wa kitaaluma, bali inapaswa pia kuimarisha maadili na ukuaji wa kihisia wa mwanafunzi.
Amesema somo la historia ya Tanzania na maadili lililoingizwa katika mtaala ulioboreshwa lina umuhimu katika kuwasaidia wanafunzi kutofautisha mema na mabaya, lakini linahitaji kuendelezwa ili liweze kujenga uwezo wa watoto kufanya maamuzi yanayowajibika.
“Ukimpa mtu A bila kuelimisha moyo wake, ajue mema na mabaya, bado hujamuelimisha,” amesema Bwaya.
Amesema umuhimu wa kujumuisha elimu ya kijamii na kihisia (social-emotional learning) katika ufundishaji ili kuwasaidia watoto kujitambua, kuelewa hisia za wengine na kufanya maamuzi yenye kuzingatia athari kwao na kwa jamii.
Bwaya amesema walimu wanahitaji maandalizi zaidi kuhusu masuala ya malezi, huku wazazi wakitakiwa kutenga muda wa kuzungumza na watoto, kuwasikiliza na kuelewa changamoto wanazopitia.
Amesema mfumo wa elimu unapaswa kuzingatia kwa pamoja maarifa, maadili na ukuaji wa kihisia ili kuwasaidia wanafunzi kuwa watu wanaoweza kuwajibika katika jamii.

