Umeme wa upepo wafungua fursa za biashara Mufindi
Iringa. Shughuli za kusaga mahindi na biashara nyingine zinazotegemea umeme ni miongoni mwa fursa zinazofunguka kwa wananchi wa Usokami na vijiji vinavyozunguka mradi wa umeme wa upepo unaotekelezwa Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa.
Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh50 bilioni, unaotekelezwa na Kampuni ya Mwenge Hydro Power Limited, una uwezo wa kuzalisha megawati 3.9 na unatajwa kunufaisha wananchi zaidi ya 9,000 katika vijiji 32 vilivyopo kwenye kata sita za Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.
Kwa wananchi, upatikanaji wa umeme karibu na makazi yao unaongeza uwezekano wa kuanzisha shughuli za uzalishaji na biashara zilizokuwa zikikwamishwa na changamoto ya nishati hiyo.
Akizungumza Oktoba 28, 2026, wakati wa ziara ya kutembelea viwanda mkoani Iringa, Mkuu wa Mkoa, Kheri James, amewataka viongozi wa vijiji vinavyozunguka mradi huo kuhamasisha wananchi kulinda miundombinu yake ili huduma iendelee kupatikana.
“Uwekezaji huu una manufaa kwa jamii na nawaomba wananchi kutumia fursa hii ya upatikanaji wa umeme ili kuimarisha shughuli zenu za kiuchumi na kujikwamua kimaisha,” amesema James.
Amesisitiza kuwa utunzaji wa miundombinu ni muhimu katika kuhakikisha mradi unaendelea kutoa huduma na kuchochea uzalishaji, biashara na maendeleo ya jamii zinazozunguka eneo hilo.
Meneja wa Mwenge Hydro Power Limited, Deogratius Massawe, amesema kampuni hiyo inalenga kuwapatia wananchi huduma ya umeme iliyo ya uhakika na gharama nafuu.
“Upatikanaji wa umeme unaweza kuongeza fursa za kiuchumi, kuimarisha shughuli za uzalishaji na biashara pamoja na kuchochea maendeleo ya jamii zinazozunguka mradi huu,” amesema Massawe.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wanufaika, Michael Mahenge amesema upatikanaji wa umeme umeanza kurahisisha shughuli za kiuchumi ambazo hapo awali zilikuwa ngumu kutekelezwa kutokana na changamoto ya nishati hiyo.
“Kwa kweli uwepo wa umeme huu umetuwezesha wananchi kuanza kufanya shughuli ndogo ndogo za uzalishaji ndani ya kijiji, ikiwemo kusaga mahindi,” amesema Mahenge.
