Treni za mwendokasi zagongana Hispania, 64 wafariki 80 wajeruhiwa
1 min read

Treni za mwendokasi zagongana Hispania, 64 wafariki 80 wajeruhiwa

Dar es Salaam. Watu 64 wamefariki dunia na wengine 80 kujeruhiwa baada ya treni mbili za mwendo kasi kugongana katika Mkoa wa Toledo, katikati mwa Hispania. Ajali hiyo ilitokea asubuhi ya leo Jumatano, Oktoba 28, 2026.

Taarifa zilizoripotiwa na Al Jazeera kwa kunukuu Shirika la Habari la Reuters zimeeleza kuwa watu 50 wamejeruhiwa vibaya, huku 15 kati yao wakiwa katika hali mahututi. Mamlaka za usalama za nchi hiyo zimeeleza kuwa  idadi ya vifo inaweza kuongezeka kutokana na hali ya baadhi ya majeruhi.

Ajali hiyo imetokea karibu na eneo la Urda, kwenye reli ya mwendo kasi inayounganisha mji mkuu Madrid na Seville, kusini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, ajali hiyo ilihusisha treni ya AVE inayoendeshwa na kampuni ya reli ya serikali ya Renfe na treni nyingine ya kampuni binafsi ya Iryo.

Treni ya Renfe ilikuwa ikielekea Seville kutoka Madrid, huku treni ya Iryo ikiwa kwenye njia hiyo hiyo. Taarifa za awali zinaeleza treni moja iliigonga nyingine kwa nyuma wakati ikiwa imesimama, hali iliyosababisha mabehewa mawili kutoka kwenye reli na kuanguka kwenye mteremko.

Sababu kamili ya ajali hiyo bado inachunguzwa, huku mamlaka zikifanya kazi ya kubaini mazingira yaliyopelekea treni hizo kugongana.

Mamlaka, wahudumu wa afya na vikosi vya ulinzi wa raia wametumwa eneo la tukio kuwasaidia majeruhi na kuwahamisha hospitalini. Pia, kituo maalumu cha huduma za matibabu kimeandaliwa karibu na eneo la ajali ili kuwahudumia waathirika kabla ya kupelekwa hospitalini.

Ajali hiyo imesababisha kusimamishwa kwa huduma za treni za mwendo kasi kati ya Madrid, Ciudad Real na maeneo ya Andalusia, kwa mujibu wa kampuni ya Renfe. Hatua hiyo imeathiri usafiri wa abiria katika njia hiyo muhimu ya reli.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *