Iringa, Njombe waonywa miundombinu ya umeme kuibwa, kuchomwa moto
Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeripoti kuchomwa kwa nguzo za umeme na kuibiwa kwa transfoma katika mikoa ya Njombe na Iringa, likionya kuwa vitendo hivyo vinasababisha kukatika kwa huduma na hasara kwa shirika hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Tanesco leo Jumatano, Oktoba 28, 2026, uharibifu huo umesababisha hasara kwa shirika pamoja na kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi za wananchi.
Hadi sasa jumla ya nguzo 66 zimeungua ambapo katika Mkoa wa Njombe, nguzo 39, Mgala 13, Utengule 3, Iboya 2, Image 2, Igoma 2, Utalingolo 4, Yakobi 13. Makete jumla nguzo 27, Ikonda 16, Ilela 5, Ipelele 3 na Lupila 3. Aidha, transfoma moja imeibwa katika eneo la Mafinga, Wilaya ya Wanging’ombe.
Nguzo ya umeme ikiwa imeanguka kutokana na uharibifu wa moto katika Mkoa wa Njombe.
Kwa upande wa Mkoa wa Iringa, Wilaya ya Kilolo, nyaya zimeharibika na transfoma moja yenye uwezo wa kVA 100 imebiwa. Katika Wilaya ya Mafinga, nguzo nyingine tano zimeungua, huku transfoma mbili zenye uwezo wa kVA 50 kila moja zikiibwa.
Kutokana na hali hiyo, Tanesco imekemea vitendo vya hujuma na wizi wa miundombinu ya umeme, ikiwataka wanaohusika kuacha mara moja vitendo hivyo.
Pia, imewataka wananchi kuchukua tahadhari wanapochoma moto kwa shughuli za kilimo na kusafisha mashamba, ili kuzuia moto kusambaa na kuharibu nguzo na vifaa vingine vya umeme.
Nguzo ya umeme ikiwa imeanguka kutokana na uharibifu wa moto katika Mkoa wa Njombe.
Aidha, shirika hilo limewataka wananchi kushirikiana na mamlaka husika kwa kutoa taarifa kuhusu matukio ya wizi, uchomaji wa makusudi na uharibifu wa miundombinu ya umeme.
Tanesco imeelekeza taarifa hizo zitolewe kwa Jeshi la Polisi au kupitia namba yake ya huduma kwa wateja ya 180, ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Shirika hilo limesisitiza kulinda miundombinu ya umeme ni jukumu la kila mwananchi, likisema ushirikiano wa jamii ni muhimu katika kukomesha vitendo hivyo na kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana kwa uhakika na endelevu.

