Vyama vya kijamii vyawa mkombozi wa wananchi
3 mins read

Vyama vya kijamii vyawa mkombozi wa wananchi

Dodoma. Mikopo isiyo na riba, msaada wa matibabu na kugharamia misiba ni miongoni mwa huduma zinazowasaidia baadhi ya wananchi kukabiliana na changamoto za kifedha kupitia vyama vya kijamii vinavyoanzishwa mitaani.

Kupitia michango ya kila mwezi na mifumo ya kuweka akiba na kukopa, vyama hivyo vimekuwa njia ya kusaidiana wakati wa dharura, ikiwemo magonjwa, vifo na shughuli za kifamilia zinazohitaji fedha nyingi.

Wakizungumza na Mwananchi jijini Dodoma leo Oktoba 28, 2026, wakazi waliojiunga na vyama hivyo wamesema ushirikiano huo umepunguza mzigo wa kifedha na kuwasaidia kupata fedha ambazo zingeweza kuwa vigumu kuzipata kwa njia nyingine.

Mwenyekiti wa Chama cha Matula Family, Benny Matula, amesema kikundi hicho kimekuwa mkombozi kwa wanachama ambao awali walilazimika kutafuta michango kwa ndugu na marafiki kila walipokumbwa na matatizo.

Amesema mwanachama anapougua hupata msaada wa hadi Sh400, 000, huku huduma hiyo ikiwahusu pia wategemezi wake wakiwemo mwenzi, watoto na wazazi kwa mujibu wa katiba ya chama.

Pia, chama hicho husaidia kugharamia huduma za msiba wa mwanachama, zikiwemo viti, magari, maturubai, muziki, wapambaji na waongozaji wa shughuli hizo.

“Tunatoa pia kiasi cha fedha kisichozidi Sh1.5 milioni kwa ajili ya msiba wa mwanachama au mtegemezi wake anayehusika kwa mujibu wa katiba yetu,” amesema.

Kwa mujibu wa Matula, huduma hizo zinagharamiwa na michango ya Sh10, 000 kwa mwezi kutoka kwa kila mwanachama.

Amesema chama hicho pia hutoa Sh400, 000 kumsaidia mwanachama kufanikisha sherehe, huku mfuko wa kuweka na kukopa ukiwawezesha wanachama kupata mikopo kulingana na akiba zao kwa ajili ya biashara, ujenzi wa nyumba na ununuzi wa vifaa vya kazi.

Ameongeza kuwa utaratibu huo umejenga utamaduni wa kuweka akiba na kuwasaidia baadhi ya wanachama kuepuka mikopo yenye masharti magumu.

Naye Katibu wa Muungano Chedego Group kilichopo Kata ya Dodoma Makulu, Brighton Msafiri, amesema kikundi hicho kilianzishwa baada ya familia ya Chedego kubaini changamoto zilizokuwa zikiwakabili wanafamilia waliokuwa wakiomba michango ya dharura wanapougua au kufiwa.

Amesema awali, familia hiyo ililazimika kuomba Sh5,000 kutoka nyumba moja hadi nyingine kila mwanafamilia alipohitaji fedha za matibabu.

“Changamoto hiyo ilitusababisha kuanzisha kikundi cha kusaidiana ndani ya familia, lakini sasa tumekipanua na hata watu ambao si wa familia wamejiunga nasi,” amesema.

Msafiri amesema kikundi hicho kina wanachama 150, kila mmoja akichangia Sh15, 000 kwa mwezi. Mwanachama au mtegemezi wake anapougua hupata Sh700, 000, huku anapofiwa akipata Sh1 milioni, inayojumuisha Sh500,000 za gharama za msiba na Sh500,000 za mkono wa pole.

Amesema kikundi hicho kimeweka faini na adhabu kwa wanachama wasiotoa ushirikiano wenzao wanapopatwa na matatizo ili kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake.

Ameongeza kuwa mfumo huo husaidia pia kupata watu wa kushirikiana katika majukumu ya msiba na kuwafariji wafiwa.

Kwa upande wake, mkazi wa Dodoma, Charles Njole, amesema kikundi anachoshiriki kimemsaidia kupata mkopo wa Sh1.5 milioni uliomwezesha kukamilisha ujenzi wa nyumba yake iliyoharibiwa na mvua mwaka jana katika eneo la Nzuguni.

“Bila kuwa mwanachama wa kikundi hicho, nisingeweza kupata mkopo huo bila riba,” amesema.

Naye Grace John amesema vyama hivyo ni muhimu kwa kuwa huwakutanisha watu wanaoweza kusaidiana kifedha na kijamii, hasa wanapokabiliwa na matukio ambayo hawakuwa wamejipanga kuyakabili.

Amesema mshikamano huo huonekana zaidi wakati wa misiba, ambapo wanachama hushirikiana kutekeleza majukumu mbalimbali na kuwafariji wafiwa.

Kwa mujibu wa wakazi hao, kuimarisha vyama vya kijamii na utamaduni wa kuweka akiba kunaweza kuongeza uwezo wa wananchi kukabiliana na dharura za kifedha na kujenga mshikamano katika jamii.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *