Vocal Africa yafungua shauri kudai Mwaipaya apatikane
Dar es Salaam. Shirika la Vocal Africa limefungua shauri mahakamani nchini Kenya, likitaka Serikali ya nchi hiyo iwajibishwe kumtafuta na kumfikisha, Twaha Mwaipaya mbele ya Mahakama, akiwa hai au amefariki.
Uamuzi wa shirika hilo, unakuja siku nne baada ya mwanaharakati huyo, kudaiwa kutekwa na watu wasiojulikana akiwa nchini Kenya. Hadi sasa bado haijajulikana wapi alipo, huku mamlaka nchini Kenya na Tanzania zikiahidi kufuatilia.
Juzi Oktoba 26, 2026, Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk Bernard Kibesse, alithibitisha kuwa mamlaka za ubalozi zinafuatilia kwa kina suala hilo ili kupata ukweli wa mazingira ya kutoweka kwa Mwaipaya.
Kwa upande wa Serikali ya Kenya, kupitia msemaji wake, Charles Owino, ilisema inafuatilia madai hayo, ingawa haikuwa imepokea taarifa rasmi kutoka kwa taasisi yoyote kuhusu tukio hilo.
Uamuzi wa kufunguliwa kwa kesi hiyo, ulielezwa jana, na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Hussein Khalid, alipozungumza na waandishi nje ya Mahakama ya Milimani nchini Kenya.
Alisema hatua hiyo inalenga kuishurutisha Serikali ya Kenya kueleza alipo kada huyo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anayedaiwa kutekwa.
Khalid alieleza wanaamini Mwaipaya bado yuko nchini Kenya, hivyo Serikali inapaswa kuhakikisha usalama wake na kueleza alipo.
Alisema kila mtu aliyeko nchini humo, bila kujali uraia wake, ana haki ya kulindwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za Kenya.
“Tunataka kusema kwa sauti moja kwamba Serikali ya Kenya ina jukumu la kuhakikisha usalama wa Wakenya na watu wengine wote walioko nchini humo,” alisema Khalid.
“Twaha Mwaipaya, ambaye ni Mtanzania, ana haki kama watu wengine wote ya kulindwa na kuhakikishiwa usalama wake.”
Khalid, alisema hatua ya kwenda mahakamani imechukuliwa ili Serikali itekeleze wajibu wake wa kisheria na kuhakikisha Mwaipaya anapatikana, huku ikieleza mazingira ya kutoweka kwake.
Alisema Kenya imekuwa ikikabiliwa na lawama kuhusu madai ya watu kutekwa na kuvushwa mipaka ya nchi kinyume cha sheria, hali inayozua hofu kuhusu usalama wa wanaotafuta hifadhi.
Khalid alitaja tukio la Novemba 2024, ambapo kiongozi wa upinzani wa Uganda, Dk Kizza Besigye, alidaiwa kutekwa jijini Nairobi na kupelekwa Uganda kwa nguvu.
Pia, alitaja jaribio la kumteka mwanaharakati wa Tanzania, Maria Sarungi, Januari 2025, ambaye baadaye aliachiwa baada ya malalamiko kutoka kwa umma.
Khalid, alisema Wakenya hawataki nchi yao itumike kuwakamata na kuwaondoa watu kutoka mataifa mengine wanaokwenda kutafuta usalama kutokana na madai ya manyanyaso.
Alisema Kenya inapaswa kuwa mahali salama kwa watu wanaokimbia maonevu, wakiwamo Watanzania na Waganda, badala ya kuwa sehemu ya vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha yao.
Khalid alieleza kuwa msimamo huo unaungwa mkono na mashirika ya haki za binadamu na ya wanasheria, yakiwemo Amnesty International, Pan-African Lawyers Union, East Africa Law Society na Law Society of Kenya.
Mashirika mengine yaliyotajwa ni Uganda Law Society, Katiba Institute na Kenya Human Rights Commission, ambayo yanataka serikali iheshimu sheria na kulinda watu wote walioko nchini humo.

