AI, data kubwa kuimarisha usimamizi wa maji
Arusha. Matumizi ya Akili Unde (AI) na uchambuzi wa taarifa nyingi yanaweza kusaidia kutabiri ukame na mafuriko, kufuatilia ubora wa maji na kuboresha usimamizi wa rasilimali hiyo, wataalamu wamesema.
Wamesisitiza kuwa teknolojia hizo zinapaswa kuunganishwa na uwekezaji katika miundombinu, uhifadhi wa vyanzo vya maji na mifumo ya kidijitali ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akisoma hotuba ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, katika kongamano la 27 la WaterNet, WAFSA na GWP-SA lililofanyika jijini Arusha leo Oktoba 28, 2026, Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dk Toba Nguvila, amesema teknolojia za kisasa zina nafasi muhimu katika kuboresha usimamizi wa maji.
Washiriki wa kongamano la kimataifa la 27 kujadili matumizi ya Akili Unde katika usimamizi wa huduma za maji uliofanyika jijini Arusha leo,kongamano hilo limeandaliwa na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) Picha na Filbert Rweyemamu
Amesema maji ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda, nishati na utalii, hivyo usimamizi wake unahitaji taarifa sahihi na maamuzi yanayozingatia ushahidi.
Dk Nguvila amesema usimamizi usiofaa wa maji unaweza kusababisha uharibifu wa mazingira, hasara za kiuchumi, matatizo ya kiafya na migogoro kati ya watumiaji.
“Mabadiliko ya tabianchi yameongeza changamoto katika upatikanaji wa maji kutokana na mabadiliko ya mvua, ukame, mafuriko na kupanda kwa joto. Teknolojia inaweza kusaidia kutabiri majanga hayo na kuwezesha mamlaka kupanga hatua za kukabiliana nayo,” amesema.
Ameongeza kuwa matumizi yenye tija ya teknolojia hizo yanahitaji taarifa za kuaminika, wataalamu wenye ujuzi na mifumo imara ya kidijitali.
Kwa upande wake, mwakilishi wa WaterNet, Nnenesi Kgabi, amesema wakati umefika wa kuondoka kwenye mijadala na kuelekea katika utekelezaji wa suluhisho za changamoto za maji.
Amesema tafiti za kisayansi zinapaswa kutumika katika kutunga sera na kufanya maamuzi, huku nchi za Afrika Mashariki na Kusini zikishirikiana kubadilishana maarifa na teknolojia.
Ameeleza kuwa ushirikiano wa kikanda ni muhimu kwa kuwa baadhi ya rasilimali za maji, ikiwemo mito na maziwa, zinashirikishwa na nchi zaidi ya moja.
Amesema matumizi ya taarifa zinazolingana na tafiti za pamoja yanaweza kusaidia kupanga ugawaji wa maji kwa haki, kupunguza migogoro na kuboresha uhifadhi wa rasilimali hizo.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST), Profesa Aloys Mvuma, amesema Akili Unde na uchambuzi wa taarifa nyingi vinaweza kuwasaidia wataalamu kuchambua taarifa za mvua, mito na maji ya chini ya ardhi ili kubaini mabadiliko na kupanga matumizi bora.
Amesema kongamano hilo ni fursa kwa wataalamu, watafiti na taasisi mbalimbali kujadili suluhisho zinazoweza kutekelezwa kukabiliana na changamoto za maji na mabadiliko ya tabianchi.
Kongamano hilo limehudhuriwa na washiriki wapatao 350 kutoka nchi 30, ikiwa ni mara ya kwanza kwa MUST kuwa mwenyeji wa mkutano huo.
Mwenyekiti wa Baraza la MUST, Dk Zakhia Meghji, amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wanawake katika usimamizi wa rasilimali za maji.
Amesema wanawake wana nafasi kubwa katika shughuli zinazohusiana na maji katika kaya na jamii, hivyo uzoefu na maarifa yao yanapaswa kuzingatiwa katika tafiti na maamuzi.
Dk Meghji, ambaye amewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, amesema wanawake hawapaswi kuonekana kama watumiaji wa maji pekee, bali pia washirikishwe kama viongozi, watafiti, wahandisi, wataalamu wa data na wafanya maamuzi.
Amesema ushiriki wao unaweza kusaidia kubuni suluhisho yanayozingatia mahitaji halisi ya jamii na kuhakikisha manufaa ya teknolojia yanawafikia watu wote.
Ameongeza kuwa ukosefu wa taarifa sahihi na uaminifu miongoni mwa watumiaji unaweza kuchangia migogoro ya maji, huku mifumo ya kidijitali na taarifa zilizo wazi zikiweza kuongeza uwajibikaji na kupunguza kutokuelewana.
Makamu Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Profesa Maulilio Kipanyula, amesema tafiti za vyuo vikuu zinapaswa kufanywa kwa kushirikiana na jamii na sekta ya viwanda ili kuhakikisha matokeo yake yanatumika kutatua changamoto halisi.
Amesema ushirikiano huo unaweza kusaidia kubuni teknolojia zinazofaa na kuongeza tija katika sekta mbalimbali, ikiwemo usimamizi wa maji.
