Copra yatumia teknolojia kuunganisha wakulima, masoko
3 mins read

Copra yatumia teknolojia kuunganisha wakulima, masoko

Kibaha. Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (Copra) imeimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali kuwaunganisha wakulima na masoko ya ndani na nje ya nchi, huku ikihimiza ubunifu katika matumizi ya mazao yanayoharibika baada ya kuvunwa ili kupunguza upotevu na kuongeza thamani ya kilimo.

Hatua hizo ni sehemu ya juhudi za mamlaka hiyo kuboresha biashara ya mazao, kupanua fursa za masoko na kuhakikisha wakulima wananufaika zaidi na uzalishaji wao.

Mkurugenzi Mkuu wa Copra, Irene Mlola amesema hayo leo Jumatano Oktoba 28, 2026, katika maadhimisho ya miaka mitatu ya kuanzishwa kwa mamlaka hiyo yaliyofanyika kwa siku tatu kuanzia Oktoba 26, Kibaha mkoani Pwani.

Mlola amesema mifumo ya kidijitali iliyoanzishwa na mamlaka hiyo imewawezesha wakulima kuuza mazao yao kupitia maghala na kuwasiliana moja kwa moja na wanunuzi wa nje ya nchi kwa kutumia mitandao.

“Copra ilianzisha mifumo ya kidijitali ili kuwafikia wakulima walioweza kuuza mazao yao kwenye maghala moja kwa moja nje ya nchi kupitia mitandao,” amesema.

Amesema mamlaka hiyo pia ina maofisa masoko wanaofuatilia mwenendo wa masoko ya ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujenga uhusiano kati ya wakulima na wafanyabiashara.

Mlola amesema katika kutekeleza jukumu hilo, Copra imeanzisha mfumo wa kidijitali wa Copramis unaolenga kuwatambua na kuwahudumia wakulima kidijitali bila kujali walipo.

Aidha, amesema mamlaka hiyo hufuatilia bei za sokoni na kusimamia bei za mnadani ili kulinda thamani ya mazao ya wakulima na kuongeza ushindani katika biashara ya mazao.

Akizungumzia mafanikio ya huduma za Copra kwa wakulima, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, amesema mamlaka hiyo imesaidia kufungua masoko 15 katika nchi mbalimbali, zikiwemo India na China.

Amesema mfumo wa ushindani katika biashara ya mazao umewawezesha wakulima kupata fursa zaidi za kuuza mazao yao, akibainisha kuwa juhudi hizo ni muhimu katika kuimarisha kilimo biashara na kuongeza kipato cha wakulima nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communication, Rosalynn Mworia, akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) Irene Mlola (kulia), kuhusu miaka mitatu ya Mamlaka hiyo, kando ya mkutano mkuu wa Mamlaka hiyo Kibaha mkoani Pwani ulifanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia Jumatatu Oktoba 26, 2026. Picha na Said Powa

Copra yataka ubunifu kuongeza thamani ya mazao

Pamoja na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali kufungua fursa za masoko, Copra imesisitiza umuhimu wa kubuni matumizi mbadala ya mazao yanayoharibika baada ya kuvunwa ili kupunguza upotevu na kuongeza thamani yake kiuchumi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Copra, Profesa Sifuni Mchome amesema sekta ya kilimo ina fursa nyingi zinazoweza kutumiwa kupitia uchakataji na ubunifu, hata kwa mazao yanayoonekana kutofaa tena kwa matumizi yake ya awali.

“Kwenye kilimo hakuna kitu ambacho hakifai, hata parachichi ambalo unaona limeoza linaweza kutoa mafuta, linaweza kuwa chakula cha mifugo likatumika,” amesema.

Amesema mfano huo unaonesha namna mazao yanayoharibika yanavyoweza kuchakatwa na kutengeneza bidhaa nyingine, zikiwemo mafuta na chakula cha mifugo, badala ya kutupwa bila kuleta manufaa ya kiuchumi.

Mchome amesema upotevu wa mazao unaweza pia kuashiria uwepo wa changamoto katika mnyororo wa thamani wa kilimo zinazopaswa kutatuliwa ili wakulima na wadau wengine wanufaike zaidi.

“Mafanikio katika kilimo yanategemea uwekezaji unaofanywa. Ukiona mazao ya kilimo yanatupwa, hapo kutakuwa na tatizo jingine,” amesisitiza.

Kwa kuunganisha wakulima na masoko kupitia teknolojia, kufuatilia mwenendo wa bei na kuhimiza matumizi mbadala ya mazao yanayoharibika, Copra inalenga kupanua fursa za biashara na kuongeza manufaa ya kiuchumi kwa wakulima na wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa kilimo nchini.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *