Mtoto wa nje ya ndoa kurithishwa mali kwazua mjadala
Dar es Salaam. Siku moja baada ya Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainabu Katimba, kueleza kuwa mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa ana haki ya kurithi mali, kumekuwa na mapokeo tofauti, baadhi wakitaka atafutiwe mali zake ili kuepusha migogoro ndani ya familia.
Jana Oktoba 27, 2026, Zainabu alilisema hilo bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge Tina Andrew Chenge, aliyehoji umuhimu wa Serikali kufanya marekebisho ya sheria za mirathi ili kuhakikisha watoto waliozaliwa nje ya ndoa hawabaguliwi katika ugawaji wa mali za marehemu.
Akifafanua msimamo wa Serikali, Katimba alisema haki za mtoto zimepewa kipaumbele na kwamba mtoto anapaswa kurithi kutoka kwa mzazi wake bila kujali kama alizaliwa ndani au nje ya ndoa.
Alisema Serikali itaendelea kuhakikisha haki za watoto, wanawake na Watanzania kwa ujumla zinazingatiwa katika masuala ya mirathi kwa kufuata sheria zilizotungwa na Bunge.
Akizungumza leo Jumatano Oktoba 28, 2026, Wakili Mwandamizi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), William Maduhu amesema kabla ya mwaka 2009, mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa hakuwa na haki ya kurithi mali za baba yake pale baba huyo alipofariki dunia.
Amesema hali hiyo ilionekana kuwa na changamoto kwa sababu mtoto alikuwa akiathirika kutokana na maamuzi ya wazazi wake, licha ya kutokuwa na kosa lolote katika mazingira ya kuzaliwa kwake.
Maduhu amesema mwaka 2009 Serikali ilitunga Sheria ya Mtoto, namba 21 ya mwaka huo, iliyoweka msingi wa kutambua usawa wa watoto mbele ya sheria na kuondoa ubaguzi unaotokana na mazingira ya kuzaliwa kwao.
“Sheria ya Mtoto imesema kwa uwazi kuwa pale penye mgogoro wa tafsiri kati ya sheria hiyo na sheria nyingine yoyote, Sheria ya Mtoto inachukua nafasi yake, mradi jambo husika linamhusu mtoto,” amefafanua.
Ameongeza kuwa Tanzania haina mfumo wa mahakama za kidini katika kushughulikia mashauri ya mirathi, hivyo migogoro hiyo huamuliwa katika mahakama za kiraia kwa kuzingatia sheria zinazotumika nchini.
Kwa mujibu wa Maduhu, mahakama zinapopokea kesi zinazohusu watoto, huzingatia ushahidi unaoweza kuthibitisha uhusiano kati ya mtoto na baba anayedaiwa kuwa mzazi wake.
Ushahidi huo unaweza kujumuisha cheti cha kuzaliwa, vipimo vya vinasaba (DNA), risiti za malipo ya ada na mawasiliano mbalimbali kati ya mtoto na baba yake.
Akielezea uzoefu wake, Maduhu amesema zaidi ya asilimia 95 ya watoto wanaohusika katika migogoro ya aina hiyo wanapopelekwa kwa familia za baba zao hukataliwa, hasa wale ambao hawakuwahi kutambulishwa katika familia hizo, hali inayosababisha wengi kuishia kutafuta haki kupitia mahakama.
“Ili kuondokana na migogoro hiyo, ni kuendelea kutoa elimu kuhusu watoto kuwa sawa mbele ya sheria. Wanaume wanapaswa kuhakikisha wanawatambulisha watoto wao mapema katika familia zao,” amesema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Tike Mwambipile, amesema mtoto anapozaliwa, anakuwa ametokana na wazazi wawili, baba na mama, hivyo mazingira ya uhusiano wao hayapaswi kuwa sababu ya kumnyima haki.
Amesema kinachopaswa kuangaliwa ni kama mtoto huyo ni wa mwanaume anayehusika, badala ya kujikita katika kujadili kama wazazi walikuwa ndani au nje ya ndoa.
“Sheria inachotaka kuangalia ni kama huyo mtoto ni wa huyu bwana,” alisema Tike, akisisitiza kuwa maelezo yaliyotolewa na Naibu Waziri yanaendana na msingi wa sheria inayolinda haki za watoto.
Kuhusu hatua za kupunguza migogoro ya mirathi, Tike amewashauri watu kuzingatia maadili na kuwa na mwenza mmoja ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza katika familia.
Amesema sheria hiyo haipaswi kutafsiriwa kuwa inalenga kumpendelea mwanamke, mwanaume au mtoto fulani, bali kulinda haki za mtoto.
Akizungumzia mgawanyo wa mali, amesema mali inayogawiwa kama urithi ni sehemu inayomilikiwa na marehemu, ambayo hugawanywa kwa warithi halali kwa kuzingatia sheria husika.
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka, amesema mwongozo wa mirathi katika Uislamu hautambui mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa kama mrithi wa baba kwa utaratibu wa kawaida wa mirathi ya Kiislamu.
Hata hivyo, alisema mwenye mali anaweza kumsaidia mtoto huyo kwa kumpa sehemu ya mali zake kupitia wosia, kwa kuzingatia utaratibu wa Kiislamu unaoruhusu kutenga hadi theluthi moja ya mali kwa watu wasiokuwa warithi.
“Kwa hiyo, mwenye mali anayo nafasi ya kumsaidia mtoto huyo kupitia theluthi ya mali zake na utaratibu ni lazima awe ameandika wosia. Mali nyingine zilizobaki zitagawanywa kwa wale wanaotambulika kisheria,” amesema Mataka.
Kwa upande wake Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mchungaji Daniel Mgogo, Daniel Mgogo amesema mtoto akishatokea duniani haki zake zote anapaswa kupata kwa baba aliyemleta.
“Ndio maana hata ukisoma Biblia mtu mmoja wa imani anaitwa Ibrahim, alipokosa mtoto kutoka kwa mke wake Sara, waliamua kupata mtoto kutoka kwa mfanyakazi wake.
‘Hata hivyo alipozaliwa yule mtoto baadaye Mungu akabariki Sara naye akapata mtoto ambapo naye wivu ukaja na akawa hamtaki tena yule mtoto pale. Lakini, Biblia inasema Ibarhim hakumwondoa yule mtoto (Ismail) mikono mitupu na badala yake alipata sehemu ya urithi ambayo aliondoka nayo,” amesema Mgogo ambaye pia ni muhubiri maarufu.
“Hivyo kusema mtoto wa nje ya ndoa hana sehemu ya urithi wakati hana baba mwingine, baba ni wewe na anapaswa apate haki zake zote kutoka kwako,”amesema Mchungaji huyo.
Katika maoni ya wananchi mtandaoni, Annarose Manyanga, amesema sheria hiyo inapaswa kufanyiwa marekebisho ili kuhimiza watu kuzaa ndani ya ndoa, kupunguza migogoro ya kifamilia na kudumisha misingi bora ya jamii.
Kwa upande wake, Unique Qnnie amesema anaunga mkono juhudi za kutetea haki za watoto waliozaliwa nje ya ndoa, akieleza kuwa hawakuchagua mazingira ya kuzaliwa kwao.
Hata hivyo, Tz_Masega amesema suala hilo linaweza kumwathiri mwanamke aliyeshirikiana na mumewe kutafuta na kujenga mali, lakini baadaye akakabiliwa na madai ya urithi kutoka kwa mtoto ambaye hakumfahamu.

