Miaka mitatu ya COPRA na safari ya kufungua fursa za mazao
Kibaha. Miaka mitatu tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023, Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (Copra) imeweka msingi wa kuratibu biashara ya mazao 129, ikilenga kuunganisha wakulima na masoko na kuongeza mchango wa kilimo katika uchumi wa Tanzania.
Katika mahojiano maalumu yaliyoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Rosalynn Mndolwa-Mworia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, Mwenyekiti wa Bodi ya Copra, Profesa Sifuni Mchome na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Irene Mlola, wameeleza safari ya miaka mitatu ya taasisi hiyo na fursa zilizofunguliwa kwa sekta ya mazao.
“Baada ya kutatua changamoto za kilimo biashara, tukatambua tunakosa mfumo wa kuratibu. Copra inasimamia mazao 129,” amesema Katibu Mkuu, akifafanua sababu ya kuanzishwa kwa mamlaka hiyo.
Masoko ya kimataifa yalivyofunguliwa
Katika kipindi hicho, Serikali imesema Copra imefungua masoko 15 katika nchi mbalimbali, zikiwemo India na China, hatua inayopanua fursa za wakulima na wafanyabiashara wa mazao ya Tanzania.
“Pia tunahamasisha wale wenye uwezo waweze kulima na kuuza moja kwa moja nje ya nchi, na tayari tumeshafungua masoko 15 katika nchi mbalimbali, zikiwemo India na China,” amesema Katibu Mkuu.
Ametaja ndizi zinazouzwa Afrika Kusini na mauzo ya parachichi yaliyofikia tani 30,000 kuwa miongoni mwa mifano ya fursa zinazojitokeza. Mahindi nayo yameuzwa kwa zaidi ya tani 15,000.
“Ndizi za wakulima wetu wanauza sana Afrika Kusini kwa sasa. Kwa hiyo, kazi ya COPRA ni kuweka mifumo ili kuwawezesha wakulima wetu kupata fursa stahiki,” amesema.
Serikali pia inalenga kuwezesha mauzo ya mahindi kupitia mtandao, yakiwemo mauzo kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ili kurahisisha upatikanaji wa wanunuzi na kupanua biashara.
“Mkakari wetu wa sasa tunataka kufikia mwakani tuweze kuuza mahindi Congo na kwingine kwa njia ya mtandao,” amesema Katibu Mkuu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communication, Rosalynn Mworia, akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) Irene Mlola (kulia), kuhusu miaka mitatu ya Mamlaka hiyo, kando ya mkutano mkuu wa Mamlaka hiyo Kibaha mkoani Pwani ulifanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia Jumatatu Oktoba 26, 2026. Picha na Said Powa
Ujenzi mifumo ya taasisi na biashara
Katika mahojiano hayo,Mwenyekiti wa Bodi ya COPRA, Profesa Sifuni Mchome, amesema hatua za mwanzo zilihusu kuweka taratibu za kuendesha taasisi na kuhakikisha inakuwa na watumishi wenye uwezo wa kutekeleza majukumu yake.
“Jambo la kwanza ambalo tulilifanya kama Bodi ni kutengeneza mifumo, kuweka miongozo na kanuni na taratibu ambazo zingewezesha mambo yaende,” amesema.
Ameongeza kuwa bodi imejikita katika kuwashirikisha wakulima, wafanyabiashara, taasisi na wadau wa kimataifa ili kuunganisha uzalishaji, uchakataji na matumizi ya mazao.
“Hiki ndicho kinawezesha usalama wa chakula na hii mikondo mitatu isipoongea unapata changamoto, lakini kwa sasa ndani ya COPRA mifumo hii inaongea vizuri ndiyo maana tumefika hapa,” amesema.
Kwa mujibu wa Mchome, ushirikiano huo unasaidia kuunganisha mahitaji ya wakulima na wanunuzi, huku mifumo na kanuni zikiweka msingi wa biashara inayozingatia mahitaji ya soko.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao na Ubora wa COPRA, Pendo Migambo, akizungumza katika mkutano wa watumishi wa Mamlaka hiyo katika kuadhimisha miaka mitatu ya kuanzishwa kwake, Kibaha mkoani Pwani, uliofanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia Oktoba 26, 2026. Picha na Said Powa.
Teknolojia kuongeza ufanisi
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Irene Mlola, amesema alipoanza kazi Oktoba 1, 2023, alikuta taasisi ikihitaji kuimarishwa ili kukidhi matarajio yaliyokuwapo, akieleza ugumu aliokutana nai na kazi aliyoifanya.
“Nilipewa sheria ya Usalama wa Chakula iliyotungwa mwaka 2009, nikapewa Oktoba 1, 2023 nianze utekelezaji huku jamii ikiwa na matarajio makubwa, hili lilikuwa jambo lililohitaji umakini mkubwa,” amesema.
Amesema ushirikiano na Serikali, taasisi nyingine, Bodi na sekta binafsi ulisaidia kuijenga taasisi hiyo.
“Sikuwa peke yangu, nilikuwa na Serikali na taasisi nyingine pamoja na sekta binafsi, hatua hiyo ndiyo iliyotuwezesha kujenga taasisi hii,” amesema.
Mlola amesema COPRA ilianza kutengeneza mifumo maalumu kwa mazao sita, yakiwemo mbaazi, ufuta, dengu na soya. Baadaye COPRA ilianzisha mfumo wa kidijitali wa COPRA MIS ambao amesema unasaidia kusajili maghala, kufuatilia ubora na kutambua shehena za mazao.
“Ili kufikia huko, ilibidi mfumo huo uweze kufundishwa kwa wenye maghala wote, ili kuratibu na kuendesha biashara ya mazao na mnyororo wake,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communication, Rosalynn Mworia, akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) Irene Mlola (kulia), kuhusu miaka mitatu ya Mamlaka hiyo, kando ya mkutano mkuu wa Mamlaka hiyo Kibaha mkoani Pwani ulifanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia Jumatatu Oktoba 26, 2026. Picha na Said Powa
Fursa kwa wakulima zaimarika
Mlola amesema mamlaka inafuatilia bei za sokoni na kusimamia bei za mnadani ili kulinda thamani ya mazao ya wakulima, huku mpango wake wa miaka mitano ukilenga kuongeza uzalishaji na matumizi ya mbegu bora, mbolea na pembejeo.
Katika mafanikio hayo, Katibu Mkuu amesema wakulima wanahitaji kupata pembejeo kwa wakati na huduma muhimu ili kuongeza uzalishaji na kunufaika na fursa zinazofunguliwa.
“Wakulima ni watu wanaofanya kazi sana. Watanzania si wavivu, wanahitaji kuwezeshwa tu kupata mbolea, mbegu kwa wakati ili waweze kuzalisha,” amesema.
Serikali pia inataka mazao yanayosimamiwa na COPRA yawe sehemu ya juhudi za kufikia uchumi wa kipato cha kati cha juu ifikapo mwaka 2050, huku ikitaja lengo la kufikisha mauzo ya mazao kwenye Dola za Marekani 5 bilioni, sawa na zaidi ya Sh13.2 trilioni ifikapo 2030.
Ili kuhakikisha wakulima wote wananufaika na safari hiyo, Mlola amewataka wadau na wakulima kuitazama COPRA kama mshirika muhimu wa kukuza biashara zao kupitia kanuni na miongozo inayowezesha sekta kukua.
“Rai yangu kwa wadau, Mamlaka ya COPRA kazi yake ni kufanya udhibiti wa mazao ili kufikia Ajenda 2030 na Dira 2030 kwa kuweka miongozo na misingi ya kutufikisha hapo kwa manufaa ya pande zote na kwa uendelevu. Waache tafsiri hasi katia tafsiri ya udhibiti” amesema.
Mlola amesisitiza kuwa COPRA ni daraja muhimu katika kuchochea fursa kwa wakulima na wadau wote katika mnyororo wa thamani ili kuimarisha upatikanaji wa pembejeo, masoko na huduma muhimu za uzalishaji, uhifadhi, usafirishaji na biashara ya mazao ndani na nje ya nchi.

