PPRA yaunganisha mifumo kudhibiti mikataba ya Serikali
4 mins read

PPRA yaunganisha mifumo kudhibiti mikataba ya Serikali

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeunganisha mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma (NeST) na mfumo wa usimamizi wa mikataba wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hatua inayolenga kuimarisha ufuatiliaji wa mikataba ya Serikali kuanzia maandalizi hadi utekelezaji.

Hatua hiyo inakuja wakati takribani asilimia 70 ya bajeti ya Serikali inapotumika kupitia ununuzi wa umma, unaotoa fursa kwa kampuni za ndani na nje kushiriki katika zabuni za miradi na huduma za Serikali.

Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba, alisema hayo leo Alhamisi, Oktoba 29, 2026, katika mkutano wa wahariri na waandishi wa habari ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Amesema ununuzi wa umma unapaswa kuzingatia thamani halisi ya fedha, ushindani, uwazi, uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali za Serikali ili kuhakikisha fedha zinazotumika zinaleta matokeo yaliyokusudiwa. “Mfumo huo unatoa fursa kwa wazabuni wa ndani na nje ya nchi kushiriki katika utekelezaji wa miradi na utoaji wa huduma za Serikali, lakini wanapaswa kutambua kuwa wanapopewa mikataba, wanatekeleza majukumu kwa masilahi ya Taifa,” amesema Simba.

Ametaja ufuatiliaji wa mikataba ya Serikali, ucheleweshaji wa malipo kwa makandarasi na changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa kazi kuwa miongoni mwa maeneo yanayohitaji usimamizi imara ili kulinda masilahi ya taasisi nunuzi na watoa huduma.

Simba amesema kuunganishwa kwa mifumo hiyo kutarahisisha ufuatiliaji wa mikataba na kuimarisha usimamizi wa mchakato wa ununuzi wa umma.

“Tumekamilisha kuunganisha mfumo wetu wa NeST na mfumo wa usimamizi wa mikataba chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” amesema.

Amesema Serikali imetoa maelekezo kuwa mikataba ya ununuzi wa umma inayotambuliwa ni ile iliyopitia katika mfumo rasmi wa ununuzi wa umma.

Ameongeza kuwa NeST ilianza kutumika rasmi Septemba 2023 na kwa sasa imeunganishwa na mifumo mingine zaidi ya 30, ikiwemo ya benki, malipo, leseni na uhakiki wa mikataba.

NeST yaokoa Sh27.64 bilioni

Mbali na kuimarisha usimamizi wa mikataba, matumizi ya mfumo wa NeST yamewezesha kuzuia uchapishaji wa zaidi ya kurasa milioni 288.57 za nyaraka za zabuni, sawa na kuokoa takribani Sh27.64 bilioni.

Matumizi ya mfumo huo wa kielektroniki yanawezesha mchakato wa ununuzi wa umma kufanyika kwa njia inayopunguza utegemezi wa nyaraka za karatasi.

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuboresha usimamizi wa ununuzi wa umma, ambao unahusisha kiasi kikubwa cha fedha za Serikali na kutoa fursa kwa wazabuni kushiriki katika miradi mbalimbali.

Makundi maalumu yapata zabuni Sh82.34 bilioni

Katika hatua nyingine, Simba alisema sheria imezielekeza taasisi za umma kutenga asilimia 30 ya bajeti za ununuzi kwa ajili ya makundi maalumu, yakiwemo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.

Alisema hadi sasa makundi maalumu 33,659 yamesajiliwa katika mfumo wa NeST na kupata zabuni zenye thamani ya Sh82.34 bilioni.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, vijana ni 16,133, wanawake 16,070, wazee 767 na watu wenye ulemavu 689.

Simba amesema lengo ni kuongeza idadi ya makundi yenye uwezo wa kushiriki katika zabuni ili kuendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema matarajio ni kuwa na takribani makundi 300,000 yenye uwezo wa kushiriki katika zabuni, huku kundi maalumu likiruhusiwa kupata zabuni moja yenye thamani ya hadi Sh500 milioni.

Zabuni zavyobadili maisha

Kwa upande wa wanufaika, Katibu wa kikundi cha Shamba Queens, Faith Mkasela, amesema kikundi hicho kimepata zabuni za kufanya usafi wa barabara na mitaro kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), zenye thamani ya Sh30 milioni, na nyingine kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads), zenye thamani ya Sh200 milioni.

Amesema kuungana kama vijana kumewasaidia kujitengenezea fursa za kiuchumi badala ya kutegemea ajira pekee.

“Tuliona hatupaswi kutegemea kusubiri ajira, tukaungana sisi kama vijana ili tuweze kujitafutia fursa wenyewe. Mfumo wa NeST kupitia PPRA umetusaidia kupata zabuni mbalimbali na kujikwamua kiuchumi,” amesema Mkasela.

Naye Mwenyekiti wa kikundi cha Nyota Bora, kinachojishughulisha na kubeba mizigo katika Stendi ya Mbezi, Goodwill Munishi, amesema mafunzo na mwongozo waliopata kutoka PPRA vimemsaidia kuelewa namna ya kutumia mfumo wa NeST kutafuta fursa za ununuzi wa umma.

Amesema maarifa hayo yamewasaidia kutambua fursa zilizopo katika mfumo rasmi wa zabuni za Serikali na kuboresha maisha yao.

“Kwa kweli tunashukuru PPRA wamekuwa walimu na walezi wazuri kwa makundi maalumu. Mifumo tunayoelekezwa na Serikali imerahisisha maisha yetu,” amesema Munishi.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *