Anayedaiwa kumuua mkewe kwa risasi kuendelea kusota rumande
Dar es Salaam. Laurence Kweka (48), anayekabiliwa na shtaka la kumuua mkewe, Jane Urassa, kwa kumpiga risasi, ataendelea kusota rumande hadi Novemba 10, 2026, baada ya upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.
Kweka, mkazi wa Bunju A, anadaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 1, 2026, eneo la Bunju A, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Leo Alhamisi, Oktoba 29, 2026, Wakili wa Serikali, Harrison Lukosi, ameiambia Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea.
Lukosi ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kemilembe Josiah, wakati kesi hiyo ya mauaji namba PI 23407 ya mwaka 2026 ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
“Kesi imeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado unaendelea. Kwa sababu hiyo, Mheshimiwa Hakimu, upande wa Jamhuri tunaomba utupangie tarehe nyingine,” amedai Lukosi.
Kutokana na maelezo hayo, Hakimu Josiah amekubaliana na ombi la upande wa Jamhuri na kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 10, 2026, kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo, Kweka hakupelekwa mahakamani, badala yake kesi hiyo iliendeshwa kwa njia ya mtandao huku mshtakiwa akiwa mahabusu.
Kwa mara ya kwanza, Kweka alifikishwa katika mahakama hiyo Oktoba 15, 2026, na kusomewa shtaka la mauaji.
Siku hiyo, upande wa Jamhuri ulidai kuwa mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Kwa mujibu wa shtaka hilo, Kweka anadaiwa Oktoba 1, 2026, eneo la Bunju A, Wilaya ya Kinondoni, kumuua Jane Maloo Urassa kwa kumpiga risasi.
Wakati wa kufikishwa mahakamani hapo, Kweka alikuwa amevalia fulana yenye mistari myekundu na suruali ya jinzi ya rangi ya kijivu.
Hakimu Josiah alimweleza mshtakiwa kuwa hahitajiki kujibu shtaka hilo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
Shtaka la mauaji linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo ataendelea kusalia rumande wakati upelelezi ukiendelea.

