Kibano watoa huduma za elimu ya fedha mtandaoni
4 mins read

Kibano watoa huduma za elimu ya fedha mtandaoni

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezindua mwongozo wa utekelezaji wa programu ya elimu ya fedha kwa waelimishaji wenye ujuzi maalumu (CFEs), ukiwa na lengo la kuimarisha usahihi wa taarifa, maadili ya kitaaluma na kulinda wananchi dhidi ya upotoshaji kuhusu huduma za kifedha na uwekezaji.

Mwongozo huo unakuja wakati Tanzania ikishuhudia ongezeko la watu wanaopenda kuwekeza katika masoko ya mitaji, hali iliyofungua fursa kwa watoa elimu ya fedha kuwaelekeza wananchi kuhusu bidhaa mbalimbali za uwekezaji.

Hata hivyo, baadhi ya waelimishaji wamekuwa wakitoa taarifa zisizo sahihi kuhusu uwekezaji katika mifuko mbalimbali, ikiwamo maelezo yanayoweza kuwafanya wananchi kuwa na matarajio yasiyo halisi kuhusu faida watakazopata.

Hatua hiyo pia imefuatia kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, aliyewataka wadau wa soko la mitaji kuepuka kuwajengea Watanzania dhana kwamba uwekezaji katika soko la hisa ni njia ya kupata utajiri wa haraka.

Amesema mtazamo huo unaweza kuwapotosha wawekezaji na kuwaweka katika hatari ya kupoteza fedha zao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mwongozo huo leo, Oktoba 29, 2026, Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi wa Watumiaji wa Huduma za Kifedha wa BoT, Dk Khadija Kishimba, amesema mwongozo huo umeandaliwa kutokana na uzoefu wa takribani miaka mitatu ya utekelezaji wa programu hiyo, ambao umebaini changamoto zinazohitaji utaratibu wa pamoja.

Amesema baadhi ya waelimishaji wamekuwa wakitoa taarifa zisizo sahihi, hali inayoweza kuathiri ubora wa elimu ya fedha na uelewa wa wananchi kuhusu maamuzi ya kifedha.

Mwongozo huo umeandaliwa kwa kushirikisha wadau mbalimbali, wakiwemo Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira), vyuo vilivyoidhinishwa na BoT pamoja na wawakilishi wa waelimishaji.

Tayari mwongozo huo umesainiwa na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, katika nafasi yake ya Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Ujumuishi wa Fedha.

Unalenga kuweka mfumo wa pamoja wa utekelezaji wa programu hiyo, kuimarisha uwajibikaji na kuboresha ubora wa elimu ya fedha inayotolewa nchini.

Kishimba amesema waelimishaji wanapaswa kuzingatia ukweli katika taarifa wanazotoa, kuheshimu mipaka ya majukumu yao na kulinda taarifa binafsi za washiriki wa programu hiyo.

“Kazi mnayofanya ni kubwa, lakini waelimishaji mnapaswa kutoa taarifa sahihi zinazojengwa katika misingi ya ukweli, kuheshimu mipaka ya majukumu yenu, kulinda taarifa binafsi za washiriki na kuepuka vitendo vinavyoweza kupotosha umma,” amesema.

 “Benki Kuu haina macho nchi nzima. Sisi tuliopo ni wachache, nyinyi ni wengi. Naomba tutumie nafasi hiyo kuweza kusaidiana,” amesema, akiwahimiza waelimishaji kushirikiana kufuatilia ubora wa elimu inayotolewa kwa wananchi.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha katika Wizara ya Fedha, Fred Ilomo, amesema mwongozo huo utaweka utaratibu wa namna waelimishaji wanavyopaswa kutekeleza majukumu yao, huku ukisaidia kulinda masilahi ya wananchi wanaopokea elimu hiyo.

Amesema licha ya matokeo chanya yaliyopatikana kupitia programu hiyo, bado kuna haja ya kuweka viwango vitakavyohakikisha walengwa wanapata taarifa sahihi na zinazoeleweka.

Naye Mshauri wa Masuala ya Fedha wa BoT, Fanuel Kajoji, amesema mwongozo huo unakuja wakati baadhi ya wakufunzi wa elimu ya fedha wamekuwa wakiwaahidi wananchi faida za uwekezaji ambazo haziwezi kuhakikishwa.

Amesema hali hiyo inaweza kuwafanya wananchi kufanya maamuzi ya kifedha kwa kutegemea matarajio yasiyo na uhakika badala ya kutathmini taarifa na hatari zinazohusiana na bidhaa wanazotaka kuwekeza.

“Jukumu la wakufunzi ni kuwawezesha wananchi kuelewa namna huduma hizo zinavyofanya kazi, manufaa yake na hatari zinazoweza kuambatana nazo ili waweze kufanya maamuzi kwa uelewa.

“Hivyo, hawapaswi kukataa au kuikashifu huduma fulani kwa ujumla, bali kutoa taarifa sahihi zinazomsaidia mtumiaji kutathmini chaguo alizonazo,” amesema.

Kajoji amesema faida ya uwekezaji inaweza kukadiriwa kwa kuchambua taarifa za mwenendo wa awali, lakini makadirio hayo hayapaswi kuchukuliwa kuwa dhamana ya matokeo ya baadaye.

“Baadhi ya bidhaa, kama dhamana za Serikali, zina masharti yanayomwezesha mwekezaji kufahamu marejesho yanayotarajiwa, lakini kwa bidhaa nyingine kiwango cha faida kinaweza kubadilika kulingana na mwenendo wa soko,” amesema.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *