Mama na baba lishe waomba eneo maalumu Mji wa Serikali Dodoma
Dodoma. Mama na baba lishe mkoani Dodoma wameiomba Serikali kuwatengea eneo maalumu la kufanyia biashara ya chakula katika Mji wa Serikali Mtumba, wakisema hatua hiyo itawawezesha kunufaika na fursa za kiuchumi zitakazotokana na uwepo wa watumishi, viongozi na wageni.
Ombi hilo linakuja wakati Rais Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuzindua majengo ya wizara, taasisi za Serikali na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba kesho Ijumaa, Oktoba 30, 2026.
Wakizungumza baada ya kutembelea mji huo leo Alhamisi, Oktoba 29, 2026, siku moja kabla ya uzinduzi, wamesema uwekezaji uliofanyika katika ujenzi wa majengo ya Serikali unaweza kufungua fursa kwa wajasiriamali wa sekta ya chakula, iwapo watapewa nafasi ya kuwahudumia watu watakaofika kwa shughuli mbalimbali.
Mwenyekiti wa mama na baba lishe Tanzania, Vijo Mali, amesema ziara hiyo imewawezesha kujionea maendeleo ya ujenzi wa majengo ya Serikali na kubaini fursa zinazoweza kuwasaidia kukuza shughuli zao za kiuchumi.
“Mradi huu ni mkubwa, ofisi ni pana na nzuri. Sisi mama lishe tunaona kuna fursa ambapo tunaweza kupata nafasi ya kuwauzia viongozi chakula, na sisi tukapata kipato,” amesema.
Mali ameiomba Serikali iwajengee au iwatengee eneo maalumu la kufanyia biashara ili mama na baba lishe wa Dodoma waweze kuuza vyakula na kunufaika na shughuli za kiuchumi zitakazochochewa na uwepo wa Mji wa Serikali.
Pia, ameiomba Serikali kuhakikisha maeneo yatakayotengwa yanakuwa na huduma muhimu, ikiwemo maji ili kuwawezesha kuandaa chakula katika mazingira yanayozingatia usafi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa baba lishe, Yahaya Hassan, amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa kwao kwa kuwa wamepata fursa ya kutembelea Mji wa Serikali na kushiriki semina iliyowapa elimu kuhusu namna ya kuandaa vyakula vya asili.
Amesema elimu hiyo itawasaidia kuboresha maandalizi ya vyakula na kuongeza ujuzi katika utoaji wa huduma kwa wateja, wakiwemo wageni wanaofika kupata huduma katika mji huo.
“Tumeambiwa tutawekewa maeneo ya kuuza chakula kwa baba na mama lishe. Tumefaidika kwa kutembelea Mji wa Serikali, lakini tumetoka kwenye semina iliyotufundisha namna ya kupika vyakula vya asili,” amesema Yahaya.
Amesema wanatarajia kutumia fursa hiyo kukuza shughuli zao na kuongeza kipato, huku wakichangia kutangaza vyakula vya asili vinavyopatikana nchini.
Kwa mujibu wa viongozi hao, kutengwa kwa maeneo maalumu kutawawezesha kutumia ujuzi walioupata na kuboresha huduma zao za chakula katika Mji wa Serikali Mtumba.

