Jiji la Arusha lachunguza kifo cha mgonjwa Kaloleni
Arusha. Halmashauri ya Jiji la Arusha imeunda timu maalumu ya kuchunguza tuhuma za uzembe wa wahudumu wa afya katika Hospitali ya Kaloleni, zinazohusishwa na kifo cha Esther Mrema, mkazi wa Njiro jijini humo.
Mrema alifariki dunia Oktoba 27, 2026, baada ya kulazwa katika hospitali hiyo tangu Oktoba 20, mwaka huu, akisumbuliwa na nimonia kali.
Familia ya marehemu inadai kuwa kuchelewa kubadilishwa kwa mtungi wa oksijeni hali ya mgonjwa ilipozidi kuwa mbaya kulichangia kifo chake.
Kutokana na tuhuma hizo, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo ameunda timu ya kuchunguza mazingira ya tukio hilo.
Katika taarifa iliyotolewa jana Oktoba 28, 2026, Halmashauri ya Jiji la Arusha ilieleza imeanza kuchunguza tukio hilo kufuatia taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha mgonjwa huyo.
“Kwa kuwa taarifa mbalimbali zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha marehemu E.M. katika Hospitali ya Kaloleni, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha ameunda timu ya uchunguzi kufuatilia suala hilo,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Halmashauri hiyo pia iliwataka wananchi kutumia njia rasmi kuwasilisha changamoto zao, huku ikitoa pole kwa familia ya marehemu.
Hospitali yakanusha uzembe
Awali, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kaloleni, Dk Anna Kimaro alisema Mrema alilazwa akiwa na nimonia kali iliyohusishwa na maambukizi ya fangasi aina ya Pneumocystis pneumonia(PCP), pamoja na kifua kikuu cha mapafu.
Dk Kimaro alisema mgonjwa huyo alipatiwa huduma za kitabibu, ikiwemo oksijeni, kwa siku zote saba alizokaa hospitalini hapo, akisisitiza kuwa hakuna uzembe uliofanyika katika kumhudumia.
“Mgonjwa alipatiwa huduma za kitabibu, ikiwemo oksijeni, kwa siku zote saba alizokuwa hapa, na kwamba wakati wa kifo chake alikuwa na mtungi wa oksijeni, tena akihudumiwa na wauguzi, hivyo hakuna uzembe wowote uliofanywa,” amesema.
Dada wa marehemu asimulia kilichotokea
Akisimulia mazingira ya tukio hilo leo Alhamisi Oktoba 29, 2026 alipozungumza na Mwananchi, dada wa marehemu, Elizabeth Mrema, amesema alikuwa akifuatilia hali ya mgonjwa ndipo alipoona kiwango cha oksijeni kwenye mtungi kikianza kupungua.
Elizabeth amesema alimjulisha daktari kuhusu hali hiyo, lakini hakukuwa na hatua za haraka za kuandaa mtungi mwingine, licha ya kumweleza mara kadhaa kuwa oksijeni ilikuwa ikipungua.
“Nilimweleza daktari kuwa oksijeni ilikuwa inapungua. Alikuja kumwangalia mgonjwa na kuniambia nisubiri hadi iishe kabisa. Baadaye nilipomfuata tena, alikiri kuwa ilikuwa inakaribia kuisha na kusema angeenda kufanya maandalizi,” amesema.
Amesema aliendelea kumwangalia dada yake, lakini baadaye aliona hali yake ikizidi kuwa mbaya, hivyo alimfuata tena mhudumu wa afya kumweleza kuwa oksijeni ilikuwa imeisha na mgonjwa alihitaji msaada wa haraka.
Kwa mujibu wa Elizabeth, mhudumu huyo alimwambia angeleta mtungi mwingine, lakini ilichukua muda kabla ya mtungi huo kufikishwa na kuunganishwa kwa mgonjwa.
“Hata hivyo, wakati mtungi ulipofikishwa, hali ya mgonjwa ilikuwa tayari imekuwa mbaya. Mhudumu aliondoka kumwita daktari, lakini alipofika, dada yangu alikuwa amefariki,” amesema.
Elizabeth amedai kuwa kama mtungi mwingine ungeandaliwa mapema au daktari angeitwa kwa wakati, huenda hali hiyo isingefikia hatua ya kifo.
Amesisitiza umuhimu wa wahudumu wa afya kuwajibika na kuchukua hatua kwa wakati, hasa pale mgonjwa anapohitaji huduma ya haraka.
Uchunguzi ulioanzishwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha unatarajiwa kufuatilia tuhuma hizo ili kubaini mazingira ya tukio hilo.
