Chadema yadai kushambuliwa na Polisi, Msajili
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimedai kuwa kinapitia mashambulizi kutoka Jeshi la Polisi na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ili kipoteze mwelekeo wa ajenda ya kuwatetea maslahi ya Watanzania.
Kwa mujibu wa Chadema, mashambulizi hayo yanajumuisha kukamatwa na kuachiwa kwa baadhi ya viongozi wake kwa nyakati tofauti, pamoja na madai ya viongozi wengine wa wilaya na mikoa kupigiwa simu na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa utaratibu ambao chama hicho kinauona si sahihi.
Pamoja na mashambulizi hayo, Chadema kimesisitiza hakitatoka nje ya mstari katika harakati za kupigania na kutetea maslahi ya Watanzania. Kimesema hali hiyo inazidi kuwaimarisha.
Mwananchi limeutafuta uongozi wa Jeshi la Polisi kuzungumzia madai hayo ya Chadema, lakini siyo msemaji wake, David Misime wala Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Jumanne Muliro aliyepokea simu ua kujibu ujumbe mfupi aliotumiwa.
Hata hivyo, wakati Chadema ikieleza hayo, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza amesema taasisi hiyo inawapigia simu hao kwa lengo la kuhakiki uongozi kwa ngazi ya wilaya na mikoa.
Akizungumza na Mwananchi leo Oktoba 24, 2026, Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, John Heche amesema hadi sasa viongozi wao watatu wanadaiwa kushikiliwa na polisi katika vituo tofauti.
Kwa mujibu wa Heche, viongozi hao ni Grace Shio (Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa), Colleta Ntidiyicha (Katibu wa Baraza la Vijana la Chadema – Bavicha Mkoa wa Kigoma) na Mwenyekiti wa Bavicha Kanda ya Victoria, Edson Mlinyinga.
Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zakaria Obadi ni miongoni mwa viongozi walishikiliwa na polisi Mkoa wa Shinyanga kwa saa 10 kisha kuachiwa kwa dhamana Oktoba 21, 2026 wilayani Kahama.
“Ni mwendelezo wa kamatakamata viongozi wetu ili kukivunja nguvu Chadema, maana hakuna sababu za msingi lengo kuvuruga jitihada zetu.
“Kwa taarifa nilizonazo hata mimi nawindwa pia, huenda wakanikamata, lakini siwezi kukimbia nchi. Hatua iliyofikiwa kwa sasa lazima mabadiliko yafanyike, ili kukomesha haya mashambulizi,” amesema Heche.
Heche amesema si polisi pekee wanaoiandama Chadema, bali hadi Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo imekuwa ikishuka hadi ngazi ya chini kuwapigia simu viongozi wao badala ya kupitia ofisi ya katibu mkuu wa chama hicho.
“Imesha wapigia simu viongozi wetu wa mikoa mitatu inawaambia njoeni tuzungumze tutawapa posho, hiki kitu sijawahi kukisikia.Kama Ofisi ya Msajili ina jambo maalumu na viongozi wa Chadema inamwambia katibu mkuu anayeshusha maelekezo chini.
“Sasa Ofisi ya Msajili inatoa wapi namba na kuwapigia viongozi wetu moja kwa moja wa ngazi ya wilaya na majimbo. Kuna namna ambayo kuna jambo linaandaliwa ili kuleta mpasuko ndani ya chama,” amedai Heche.
Amesema hilo likitokea litakifanya chama hicho kitoke nje ya mstari na kusababisha viongozi wake kuangaika polisi na korido za Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kushughulikia masuala yanayowakabili.
“Nilimpigia Msajili, akaniambia wanavyofanya eti katika maeneo yenye uchaguzi wa kata na majimbo, lakini kuna sehemu zingine hakuna uchaguzi, nilimueleza hivyo. Pia, kwanini asipitie kwa Katibu Mkuu.
“Ukiangalia kwa haraka haraka ni haya haya mashambulizi yanayoratibiwa kutoka Ofisi ya Msajili na Polisi, ili watu wetu wawe ‘busy’ kwa Msajili na Polisi,” amedai Heche.
Ufafanuzi Ofisi ya Msajili
Akizungumza madai hayo ya Heche, Nyahoza amekanusha akisema kinachofanyika ni uhakiki viongozi wa vyama vya siasa katika maeneo yenye uchaguzi, wakilenga kutambua viongozi halali, si kuwanyanyasa, kama inavyodhaniwa.
Kwa mujibu wa Nyahoza, Ofisi ya Msajili imeviandikia vyama vyote vya siasa barua na kuviwasilisha mpango kazi wa uhakiki, hivyo inahitaji ushirikiano wao ili kufanikisha utekelezaji wake.
Amesema kwa sasa uhakiki huo unafanyika katika wilaya zenye kata 11 zinazotarajiwa kufanya uchaguzi, kwa lengo la kuthibitisha viongozi wa mikoa na wilaya wa vyama vya siasa katika maeneo hayo.
Amefafanua kuwa kwa mujibu wa sheria, vyama vya siasa vinapaswa kuwa na rejesta ya viongozi wake wa mikoa na wilaya, hivyo ni muhimu kwa Ofisi ya Msajili kuwa na taarifa sahihi za viongozi hao.
“Ni kutambuana tu ili tujue nani kiongozi halisi. Tusipokuwa na taarifa kamili, tunaweza kuwa na watu wasio halali wanaojifanya viongozi wa vyama fulani,” amesema Nyahoza.
Amesema shughuli hiyo inahusisha vyama vyote 19 vya siasa na kwamba baadhi ya vyama vimeshirikiana na ofisi hiyo bila kulalamika kama Chadema kinavyofanya.
“Tumeshaviandikia vyama vyote na kuvipelekea mpango kazi. Mbona wenzao wanashirikiana? Hatufanyi kwa chama kimoja, tunafanya kwa vyama vyote,” amesema.
Nyahoza amesema ofisi hiyo, pia, hutoa elimu kuhusu gharama na taratibu za uchaguzi, hivyo inahitaji kufanya kazi na viongozi halali wanaotambulika katika maeneo husika.
Amesisitiza kuwa ushirikiano wa vyama ni muhimu katika kuhakikisha taarifa za viongozi zinakuwa sahihi na kuzuia watu wasiotambulika kujifanya viongozi wa vyama vya siasa.
Nyahoza amekanusha madai ya Chadema kuwa hatua hiyo inalenga kukinyanyasa chama hicho bali kutambua viongozi halali na kuhakikisha vyama vyote vinashirikishwa katika utekelezaji wake.

