Migogoro 21 ya ndoa yaripotiwa ndani ya siku 23 Mwanza
3 mins read

Migogoro 21 ya ndoa yaripotiwa ndani ya siku 23 Mwanza

Mwanza.  Jumla ya migogoro 21 ya ndoa imeripotiwa katika vituo vya polisi mkoani Mwanza kuanzia Oktoba Mosi hadi 23, mwaka huu, huku wivu wa mapenzi, usaliti na changamoto za kiuchumi zikitajwa miongoni mwa sababu zinazochangia migogoro hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema wivu wa mapenzi umekuwa ukitajwa mara kwa mara katika matukio ya mauaji na majeraha yanayotokana na migogoro ya kimahusiano.

Akizungumza na waandishi na Dawati la Habari la Jeshi la Polisi ofisini kwake Oktoba 23, 2024 Mutafungwa amesema baadhi ya sababu zinazochangia migogoro ya ndoa ni pamoja na changamoto za kiuchumi, matatizo ya kijamii, tabia binafsi za wanandoa, usaliti na wivu wa mapenzi.

Akizungumzia takwimu za migogoro ya ndoa katika mwezi huu wa Oktoba, Kamanda Mutafungwa amesema kesi 21 zimeripotiwa katika kipindi cha wiki tatu tangu mwezi huo ulipoanza, hali inayoonesha umuhimu wa kuendelea kutoa elimu na kuchukua hatua za kuzuia migogoro hiyo isizidi.

“Kwa mwezi huu wa 10 ambao haujaisha, tuna jumla ya kesi za migogoro ya ndoa 21 zimeripotiwa kwa hizi wiki tatu tangu mwezi wa 10 umeanza. Ina maana kuna ndoa 21 zipo kwenye hali tete, watu wameona hawawezi kukaa wakatulia, wameamua kuja kwenye madawati,” amesema Mutafungwa.

Ameongeza kuwa takwimu hizo zinahusu matukio yaliyoripotiwa polisi, huku kukiwa na uwezekano wa kuwepo kwa migogoro mingine ambayo bado haijafikishwa kwenye mamlaka husika, akisisitiza kuwa elimu kwa jamii inapaswa kuendelea ili kuwahamasisha wananchi kutafuta msaada mapema.

Katika hatua nyingine, amesema Jeshi la Polisi mkoani Mwanza lina madawati saba yanayoshughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto katika maeneo mbalimbali ya mkoa, yakihudumiwa na askari wenye mafunzo maalumu wanaoshirikiana na taasisi nyingine pamoja na watoa huduma.

Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kushughulikia kesi zinazohusiana na ukatili, kutoa msaada kwa waathirika na kuelimisha jamii kuhusu namna ya kuzuia vitendo hivyo.

Mutafungwa amewataka wanandoa na jamii kwa ujumla kutambua kuwa migogoro ya kifamilia inapozidi inaweza kusababisha madhara makubwa kwa wahusika na watoto, ambao huathirika kisaikolojia na kimakuzi pale wanapokulia katika mazingira yenye migogoro ya mara kwa mara.

“Wanandoa na jamii kwa ujumla watambue kwamba migogoro inapokithiri katika ndoa zao inaleta athari kubwa sana kwa watu wote, hasa watoto,”amesisitiza.

Amewahimiza wananchi kutoa taarifa na kutafuta msaada kutoka kwa mamlaka husika pale migogoro inapoanza kujitokeza, badala ya kusubiri hadi ifikie hatua ya kusababisha majeraha au kupoteza maisha.

Akizungumzia suala hilo, mkazi wa Jiji la Mwanza, Elizabeth Mathias amewashauri wanandoa wanaokabiliwa na migogoro kuripoti katika madawati ya Jinsia na Watoto au kutafuta msaada kutoka kwa mamlaka husika ili kuzuia migogoro hiyo isisababishe madhara makubwa.

Amesema ni muhimu kwa wanandoa kutambua wakati hali ya mahusiano inapokuwa ngumu na kuchukua hatua mapema badala ya kuendelea kuvumilia mazingira yanayohatarisha usalama wao.

“Ni bora kuripoti au kuomba talaka unapoona mambo yamekuwa magumu kuliko kuvumilia hadi mambo makubwa yatokee, kama kupigwa, kuumizwa au kuuawa,”amesema Elizabeth.

Mkazi mwingine wa jiji hilo, Said Salum amesema kutofautiana katika ndoa ni jambo linaloweza kujitokeza, akiwataka wanandoa kuepuka kufanya maamuzi ya haraka yanayoweza kuhatarisha maisha yao au ya wenza wao.

Ameshauri wanandoa kutafuta msaada na ushauri kutoka kwa watu au mamlaka zinazohusika ili kupata suluhisho la migogoro yao kwa njia salama na kuzuia vitendo vya ukatili.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *