Chalamila ataka Ilala Kota ipangwe upya
4 mins read

Chalamila ataka Ilala Kota ipangwe upya

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema majengo chakavu katika eneo la Ilala Kota, Kata ya Mchikichini, yanapaswa kuondolewa na eneo hilo kupangwa upya ili kujenga miundombinu ya kisasa inayoendana na ukuaji wa jiji.

Amesema mpango huo unapaswa kuzingatia makazi bora, maeneo ya biashara, maegesho ya magari na huduma nyingine muhimu, badala ya kuendelea kujenga majengo kwa mtindo wa zamani unaochangia msongamano na matumizi yasiyofaa ya ardhi.

Chalamila ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, Oktoba 23, 2026, wakati wa ziara ya kutembelea maeneo yanayomilikiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), yakiwamo Manyanya kwa Kota, Mtaa wa Msolomi, Kata ya Mwananyamala, Wilaya ya Kinondoni, na Ilala Kota, Mchikichini, Ilala.

Amesema ukuaji wa Dar es Salaam unahitaji mabadiliko katika upangaji na uendelezaji wa maeneo, ili majengo mapya yazingatie mahitaji ya wakazi wa sasa na wa baadaye.

“Ukienda Daraja la Kigogo, ambalo zamani lilikuwa kama uchochoro na uswahilini, leo panapendeza sana. Lakini ukitazama upande mwingine, kuna vijumba ambavyo havina sifa tena ya kuwa katikati ya mji.

“Hivyo vinatakiwa vitoke ili eneo lipangwe upya na kujengwa kwa namna itakayolingana na taswira ya kisasa ya jiji,” amesema.

Amesema Dar es Salaam inaendelea kukua kutokana na shughuli za kiuchumi, biashara, bandari, elimu na uwekezaji, hali inayoongeza mahitaji ya makazi na miundombinu bora.

Kwa mujibu wa Chalamila, jiji hilo lina ukubwa wa takribani kilomita za mraba 1,500 na wakazi zaidi ya milioni sita. Makadirio yanaonyesha kuwa idadi hiyo inaweza kufikia milioni 10 kati ya mwaka 2030 na 2035.

Amesisitiza kuwa ongezeko hilo linapaswa kuendana na mipango miji inayozingatia matumizi bora ya ardhi, maegesho, huduma za kijamii na mifumo ya majitaka.

Akizungumzia Ilala Kota, amesema eneo hilo linaweza kuendelezwa kuwa mradi mkubwa wenye majengo ya biashara, makazi, maeneo ya michezo, kumbi za mikutano na maegesho ya magari ya chini ya ardhi.

Amesema fursa hiyo inapaswa kutumika badala ya kuendelea kujenga majengo madogo bila mpango wa pamoja.

“Leo Kariakoo karibu kila eneo limejengwa, lakini majengo mengi hayana maegesho ya kutosha. Tunapopata eneo kubwa kama Mchikichini, tunapaswa kufikiria maegesho ya chini ya ardhi na huduma nyingine zitakazosaidia kupunguza msongamano,” amesema.

Chalamila amesema Serikali inahitaji kushirikiana na sekta binafsi kuharakisha uendelezaji wa maeneo ya umma, akieleza kuwa ushirikiano huo unaweza kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kugawana gharama na hatari za uwekezaji.

Amesema TBA inapaswa kutumia uzoefu wake wa kujenga na kusimamia majengo ya Serikali kuvutia wawekezaji binafsi kwa ajili ya miradi ya makazi na biashara.

TBA yatathmini hali ya majengo

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TBA, Saidi Mdeme, amesema wakala huo unaendelea kutathmini hali ya majengo na maeneo yake ili kubaini namna bora ya kuyaendeleza kwa kuzingatia mahitaji ya jiji na usalama wa wananchi.

Akizungumzia Manyanya kwa Kota, amesema awali kulikuwa na mpango wa kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa nyumba zilizopo, lakini tathmini ya wataalamu ilibaini kuwa hali ya majengo hayo hairuhusu kuendelea na mpango huo kama ulivyokusudiwa.

Amesema matokeo hayo yameonyesha umuhimu wa kutathmini upya matumizi ya eneo hilo badala ya kuwekeza fedha katika kukarabati majengo ambayo hayastahili kuendelea kutumika katika hali yake ya sasa.

Mdeme amesema eneo la Manyanya kwa Kota lina ukubwa wa takribani ekari 4.7, huku TBA ikiendelea kutathmini maeneo yake kwa ajili ya kuandaa mipango ya maendeleo inayozingatia matumizi bora ya ardhi.

Amesema TBA inasimamia nyumba 6,629 nchini, zikiwemo 1,080 Dar es Salaam. Wakala huo pia unaendelea na ujenzi wa nyumba 80 Magomeni Kota na maandalizi ya mradi wa nyumba 144 Temeke Kota.

Aidha, Mdeme amesema TBA inaandaa mipango ya kuendeleza Ilala Kota, Mchikichini, lenye ukubwa wa ekari 44.5.

Ameongeza kuwa wakala huo unaimarisha usimamizi wa maeneo yake kwa kuweka mipaka na mabango yanayoonyesha umiliki wa Serikali, huku ukiendelea kutafuta fursa za kushirikiana na sekta binafsi katika miradi ya maendeleo.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *