Machinga Kariakoo watangaziwa ahueni | Mwananchi
Dar es Salaam. Wafanyabiashara wadogo, maarufu wamachinga waliopo Kariakoo, jijini Dar es Salaam, wanatarajiwa kuendelea na shughuli zao katika maeneo waliyoruhusiwa kukaa hadi soko lao linalopangwa kujengwa Jangwani litakapokamilika.
Mwenyekiti wa Wamachinga Kariakoo, Steven Lusinde, amesema hayo leo Jumatano, Oktoba 21, 2026, alipokutana na wafanyabiashara hao kuwapa mrejesho wa mazungumzo yao na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe, yaliyofanyika siku mbili zilizopita kuhusu suala la kuondoka Kariakoo na eneo watakalohamia.
Hatua hiyo inawahusu wafanyabiashara waliokuwa katika maeneo ambayo Serikali iliwapa ruhusa ya kufanya biashara, wakiwemo waliopo katika mitaa ya Narung’ombe, Congo, Mchikichini, Nyamwezi, Agrey, Sikukuu na Swahili.
Septemba 24, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, aliwapa wamachinga mwezi mmoja, hadi Oktoba 24, 2026 kuondoka katika maeneo yasiyo rasmi ili kupisha barabara na kuwezesha shughuli za usafirishaji na biashara kufanyika kwa utaratibu.
Chalamila alisema hakuna mfanyabiashara anayefukuzwa Kariakoo, bali wanatakiwa kuondoka barabarani na kutafuta maeneo rasmi ya kufanyia biashara.
“Tungependa mtumie kipindi hiki cha mwezi mmoja kupisha barabara hizo wenyewe. Kariakoo hii fremu nyingi zinajengwa, tafuteni maeneo katika fremu hizo. Serikali pia imetumia takribani Sh28 bilioni kujenga na kukarabati Soko Kuu la Kariakoo, hivyo lazima njia za kuingia na kuingiza mizigo soko hilo zipitike wakati wote,” alisema Chalamila.
Maamuzi hayo yalitokana pia na kampeni ya usafi na agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuboresha usafi wa Jiji la Dar es Salaam, akieleza kutoridhishwa na hali ya usafi, ikiwemo wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika maeneo yasiyo rasmi.
Wakati wafanyabiashara katika baadhi ya maeneo mengine tayari wameondolewa, wamachinga wa Kariakoo walipewa muda wa mwezi mmoja kujiandaa.
Wafanyabiashara wadogo, maarufu wamachinga wakiwa Kariakoo jijini Dar es Salaam leo Octoba 21, 2026, wakifutilia Mkutano uliotishwa na viongozi wa wafanyabiashara hao kuhusu kuruhusiwa kuendelea na biashara Katika eneo hilo hadi ujenzi wa soko lao utakapo kamilika, eneo la Jangwani. Picha na Said Powa
Lusinde: Tumezungumza na Serikali
Akizungumza na wafanyabiashara hao, Lusinde amesema katika mazungumzo yao na Profesa Shemdoe, Waziri huyo aliwaonyesha eneo ambalo soko lao litajengwa. Eneo hilo lipo karibu na Soko la Kigogo Sambusa, Jangwani.
“Hivyo mkutano huu wa leo ni kuja kuwapa taarifa wenzetu kile tulichozungumza na Waziri na namna Serikali ilivyoweza kulishughulikia suala hili,” alisema Lusinde.
Alipoulizwa kama hilo ndilo soko ambalo Serikali iliahidi kulijenga Jangwani, ikiwemo wakati Rais Samia alipofungua Soko la Kariakoo, Lusinde alithibitisha kuwa ndio hilo.
Alisema soko hilo likikamilika, litaweza kuchukua wafanyabiashara zaidi ya 10,000 kwa wakati mmoja.
Kuhusu malalamiko ya wamachinga kwamba hawashirikishwi katika ujenzi wa masoko ya Serikali, Lusinde alisema safari hii wameshirikishwa na wameeleza aina ya soko wanalohitaji.
“Kwa kweli kwa soko hili niseme tumeshirikishwa na kwa safari hii tumewasisitiza hatutaki jengo la ghorofa, hivyo soko letu litakuwa la chini kwa kuwa ndiyo biashara yetu inavyotaka,” alisema.
Lusinde amesema wamachinga hawataki kutumia mfumo wa mtandaoni wa Tausi kupata maeneo katika soko jipya, akitaka Serikali itumie kanzidata zao kuwapangia maeneo.
Alisema mfumo huo unaweza kuwanufaisha watu wasiohusika, ambao baadaye hukodisha maeneo kwa wafanyabiashara wengine kwa bei kubwa.
“Sisi Tausi katika soko letu hili jipya tutataka ndiyo itufuate kwa kuwa ni mfumo ambao wengi wetu hatuujui kutumia na mwisho wa siku wasiohusika ndiyo wanafaidika nao na maeneo hayo ambayo huyachukua kwa lengo la kuja kuyakodisha kwa wengine kwa bei kubwa,” alisema.
Mmoja wa wafanyabiashara wadogo, maarufu wamachinga akizungumza leo Octoba 21, 2026, Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Machinga waunga mkono uamuzi
Baadhi ya wamachinga wameeleza kuunga mkono hatua hiyo, wakisema walikuwa na wasiwasi kuhusu mahali pa kwenda baada ya muda waliopangiwa kuondoka Kariakoo kukamilika.
Pius Deo alisema wamepokea maelezo hayo kwa mikono miwili, akisisitiza kuwa biashara zao zinategemewa na familia nyingi.
“Jamii inapaswa kuelewa sisi uwepo wetu barabarani kuna familia nyuma zinatutegemea kupitia kazi hii na si kwamba ni watu wahuni,” alisema.
Aliongeza kuwa kuwaondoa bila kuwapatia eneo mbadala kunaweza kuathiri familia zinazotegemea kipato chao, ikiwemo watoto wanaosomeshwa kupitia biashara hizo.
Naye Aibu Sangoba alisema wako tayari kuondoka Kariakoo hata kesho ikiwa wataelezwa kuwa soko lao limekamilika na liko tayari kutumika.
Alisema tamko la Chalamila lilisababisha taharuki miongoni mwa wafanyabiashara hao, kila mmoja akijiuliza atakwenda wapi.
Kuhusu madai kwamba wamachinga hawalipi ushuru, Rehema Mnukwa alisema madai hayo si ya kweli, akieleza kuwa utaratibu wa kuwapanga kwenye meza ungeweza kurahisisha ukusanyaji wa ushuru iwapo ungeandaliwa vizuri.
Eneo la Jangwani Katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam ambalo soko la Wafanyabiashara wadogo, maarufu wamachinga, linarajiwa kujengwa hivi karibuni. Picha na Said Powa
Soko kukamilika ndani ya miezi sita
Akizungumzia mpango wa ujenzi wa soko hilo, Profesa Shemdoe alisema Serikali inalenga kulikamilisha ndani ya miezi sita ili kupunguza msongamano wa wafanyabiashara Kariakoo.
Alisema mpango huo ulitangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan Januari 30, 2025, na ujenzi utatekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Ilala.
“Lengo la Serikali ni kupunguza msongamano uliopo Kariakoo. Ujenzi wa tuta katika eneo la Kigogo Sambusa unaanza mara moja na ukikamilika, Halmashauri ya Jiji la Ilala itaanza ujenzi wa soko. Tunataka eneo hili liwe tayari ili wamachinga waweze kuhamia na kufanya biashara zao kwa amani,” alisema.
Shemdoe alisema ujenzi wa soko hilo utagharamiwa kwa asilimia tano ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Ilala, baada ya Rais Samia kutoa idhini ya kutumia fedha hizo kuimarisha miundombinu ya biashara, ikiwemo ujenzi wa masoko.
Alisema wakati ujenzi ukiendelea, Serikali itaendelea kupanga wamachinga waliopo Kariakoo ili kuhakikisha barabara zinapitika na shughuli za biashara zinafanyika katika maeneo yaliyopangwa.

