Pambalu naye kortini uhaini | Mwananchi
Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mafunzo, Oganaizesheni na Uchaguzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Pambalu amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, akikabiliwa na shtaka la uhaini.
Pambalu, ambaye pia ni mjumbe wa Sekretarieti ya Taifa, Kamati Kuu na Baraza Kuu la Chadema, amesomewa shtaka hilo leo Jumatano, Oktoba 21, 2026, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Salome Mshasha.
Katika kesi hiyo, Pambalu anakabiliwa na shtaka moja linalodaiwa kuwa kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Toleo la Marekebisho la mwaka 2023.
Wakili wa Serikali, Titus Aron, ndiye aliyemsomea shtaka hilo, bila wakili wa Pambalu kuwepo mahakamani.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka ambayo Mwananchi imeiona na kuthibitishwa na mmoja wa mawakili wa Chadema, Hekima Mwasipu, Pambalu anadaiwa kutenda kosa hilo katika nyakati tofauti, Septemba mosi na Oktoba 29, 2025, katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Hati hiyo inadai kuwa Pambalu, akiwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alionyesha nia ya kushawishi umma kusababisha kuzuiwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Anadaiwa kuonyesha nia hiyo kwa kuendesha maandamano yasiyo na ukomo nchini, kwa kusudi la kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kabla ya kufikishwa mahakamani na kusomewa shtaka hilo, Pambalu alikamatwa jijini Arusha Oktoba 14, 2026, kisha akasafirishwa hadi Dar es Salaam, ambako alihojiwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Pambalu ni kiongozi wa pili wa Chadema kukabiliwa na kesi ya uhaini inayohusishwa na madai ya kujaribu kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, akitanguliwa na mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu huku Katibu wa Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami na wenzake 16 wakishtakiwa kwa kupanga na kula njama kufanya vitendo vya ugaidi.
Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025, wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma, na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambako alisomewa shtaka la uhaini Aprili 10, mwaka huo.
Kwa sasa, Lissu anasubiri kusomewa hukumu katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, Novemba 6, 2026, baada ya kukamilika kwa usikilizaji wa kesi yake.

