Mkuna: Kwa nini biashara ndogondogo hukua taratibu?
Katika mitaa ya Tanzania, kufanya biashara ndogo ndogo ni sehemu muhimu ya maisha ya kila siku. Kuanzia mama lishe, wauza mboga, maduka ya rejareja, saluni, mafundi, wachuuzi, wasafirishaji hadi wafanyabiashara wa bidhaa mtandaoni, maelfu ya Watanzania hutegemea biashara hizi kama chanzo cha kipato.
Hata hivyo, pamoja na idadi kubwa ya biashara hizi, swali muhimu linabaki: kwa nini biashara nyingi hukaa katika kiwango kilekile kwa miaka mingi bila kuwa biashara kubwa?
Jibu si kwamba wafanyabiashara hawafanyi kazi kwa bidii bali wengi huamka mapema na kufunga biashara zao usiku. Tatizo mara nyingi liko katika namna biashara inavyoendeshwa.
Kwanza, kutenganisha fedha za biashara na fedha za familia ni changamoto kubwa.
Mfanyabiashara anaweza kupata mauzo ya shilingi 100,000 kwa siku na kudhani amepata faida hiyo yote. Sehemu ya fedha hizo hutumika kununua chakula, kulipa kodi, ada za watoto au mahitaji mengine ya nyumbani. Mwishowe, mtaji unapungua bila mfanyabiashara kutambua. Biashara haiwezi kukua ikiwa faida hairejeshwi kwa kiwango cha kutosha katika biashara.
Pili, biashara nyingi zinaendeshwa bila kumbukumbu sahihi za mapato na matumizi. Baadhi ya wafanyabiashara hawajui bidhaa gani inaleta faida kubwa, ni kiasi gani wanadaiwa na wateja, wala gharama halisi za uendeshaji. Bila taarifa hizi, maamuzi yanafanywa kwa hisia badala ya ushahidi.
Tatu, kutegemea wateja wale wale kunaweza kuzuia ukuaji. Mfanyabiashara anayesubiri wateja wapite mbele ya duka pekee anaweza kupoteza fursa kubwa zinazopatikana kupitia simu na mitandao ya kijamii.
Teknolojia imebadilisha namna watu wanavyotafuta, kulinganisha na kununua bidhaa. Biashara ndogo inayotumia WhatsApp, Facebook, Instagram, TikTok au majukwaa mengine inaweza kufikia soko kubwa zaidi kuliko eneo lake la biashara.
Nne, baadhi ya wafanyabiashara wanaogopa kuwekeza katika ubora na ubunifu. Wanataka kuuza bidhaa ileile kwa bei ileile kwa miaka mingi. Lakini soko hubadilika. Wateja wanataka ubora, huduma nzuri, urahisi na thamani zaidi.
Biashara inayokataa kubadilika inaweza kuendelea kuwapo lakini ikashindwa kukua.
Pia kuna changamoto ya upatikanaji wa mtaji. Biashara nyingi zinahitaji fedha kwa ajili ya kuongeza bidhaa, mashine, teknolojia au kufungua matawi mapya.
Hata hivyo, kutegemea mikopo pekee si suluhisho. Mfanyabiashara anahitaji kwanza kujenga mfumo mzuri wa biashara unaoonyesha uwezo wa kuzalisha na kurejesha mtaji.
Jambo jingine ni ujuzi wa usimamizi. Kuwa na bidhaa nzuri hakutoshi. Mfanyabiashara anahitaji kujua kupanga, kuweka bei, kusimamia hesabu, kutunza wateja, kudhibiti gharama na kutathmini faida. Biashara inapokua, mmiliki pia anatakiwa kujifunza kugawa majukumu badala ya kufanya kila kitu mwenyewe.
Biashara nyingi hukua polepole kwa sababu hazina malengo yanayopimika. “Nataka biashara yangu ikue” si mpango. Mfanyabiashara anapaswa kujiuliza: Nataka mauzo yafikie kiasi gani ndani ya miezi sita? Nataka kuongeza wateja wangapi? Nataka kufungua tawi lini? Ni kiasi gani cha faida nitarejesha kwenye biashara?
Tanzania inahitaji biashara ndogo zinazoweza kukua na kuwa biashara za kati na kubwa, kwa sababu ukuaji huo unamaanisha ajira zaidi, mapato zaidi na uzalishaji mkubwa. Changamoto si kuwa na biashara ndogo; changamoto ni kubaki ndogo kwa sababu ya mifumo mibovu ya uendeshaji.
