Mwigulu ashawishi wawekezaji Marekani kwenye kilimo
Dar es Salaam. Tanzania imewakaribisha wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika sekta ya kilimo, ikitumia fursa ya soko la watu milioni 170 katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amesema uwekezaji katika sekta hiyo unaweza kuongeza uzalishaji wa chakula, kuboresha lishe na kutengeneza fursa za kiuchumi.
“Uwekezaji unaweza kuchangia kutoa huduma za chakula na lishe na wakati huohuo ukatengeneza fursa za kiuchumi zinazoonekana. Kwa hiyo, tunawakaribisha nyote kuwekeza nchini Tanzania kwani mnapowekeza Tanzania kwa maana pana, mnawekeza pia katika soko la ukanda mzima,” alisema.
Dk Mwigulu aliyasema hayo jana Jumanne, Oktoba 20, 2026, alipoongoza mjadala kuhusu uwekezaji katika kilimo biashara, uliohusisha viongozi wa kampuni za utafiti wa kilimo, teknolojia za kilimo, uzalishaji wa bidhaa za kilimo, mbegu na dawa za wadudu wa mazao.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mjadala kuhusu uwekezaji katika kilimo-biashara, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Iowa, jijini Des Moines, nchini Marekani, Oktoba 20, 2026. Mjadala huo ulifanyika kando ya Mkutano wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug.
Mjadala huo ulifanyika kando ya mkutano wa kimataifa wa Norman E. Borlaug, jijini Des Moines, Jimbo la Iowa, Marekani.
Akieleza fursa za uwekezaji zilizopo nchini, Waziri Mkuu alitaja usindikaji na ufungashaji wa mazao, ujenzi wa maghala, miundombinu ya kuhifadhi bidhaa katika ubaridi, usafirishaji, huduma za kidijitali na huduma za kifedha kwa wakulima na wafanyabiashara.
Alisema Tanzania ina hekta milioni 44 za ardhi zinazofaa kwa kilimo, lakini zinazotumika kwa shughuli hizo ni hekta milioni 10.8 pekee.
Kuhusu kilimo cha umwagiliaji, alisema nchi ina uwezo wa kumwagilia hekta milioni 29.4, lakini eneo linalotumika kwa sasa ni hekta 727,280, hali inayotoa nafasi kwa wawekezaji kushiriki katika kupanua uzalishaji.
Dk Mwigulu alisema Serikali imewekeza katika skimu za umwagiliaji, uzalishaji wa mbegu na programu zinazolenga kuwawezesha vijana kushiriki katika kilimo, mifugo na uvuvi.
Aliongeza Serikali imeweka vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi kwa wawekezaji ili kuchochea uwekezaji katika sekta hiyo.
Waziri Mkuu alisisitiza kuwa sekta binafsi ni mshirika muhimu katika kuongeza thamani ya mazao, kupanua masoko, kutengeneza ajira zenye staha na kuimarisha usalama wa chakula na lishe.
Katika mjadala huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Utafiti na Viwanda wa Microsoft, Dk Ranveer Chandra, alieleza namna teknolojia ya Akili Unde (AI) inavyoweza kutumika kuongeza tija ya uzalishaji na kuboresha maisha ya wakulima.
Alisema alianza programu ya kilimo ndani ya Microsoft miaka 10 iliyopita na tangu wakati huo kampuni hiyo imetekeleza shughuli mbalimbali nchini Tanzania.
Baadhi ya washiriki wakimsikiliza Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba (kulia, aliyeipa kamera mgongo), wakati wa mjadala kuhusu uwekezaji katika kilimo-biashara, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Iowa, jijini Des Moines, nchini Marekani, Oktoba 20, 2026.
“Miongoni mwa shughuli hizo ni ushirikiano wetu na Made Alliance, ambao ulilenga kusaidia matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali kwa wakulima 50,000 wa alizeti nchini Tanzania. Pia tulishirikiana na kampuni ya Mawingu kupanua upatikanaji wa huduma za mawasiliano na intaneti katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania,” alisema.
Kuhusu kuongeza ujuzi wa AI, Dk Chandra alisema Microsoft imeshirikiana na ABSA Tanzania pamoja na Women in Tech kutekeleza mpango unaolenga kuwapatia wanawake 5,000 mafunzo kuhusu teknolojia hiyo.
Alisema Akili Unde inaweza kusaidia kuongeza kipato cha wakulima, kuboresha tija ya uzalishaji na kupunguza upotevu wa mazao.
“Ndani ya Microsoft, tumekuwa tukichunguza namna Akili Unde inavyoweza kutumika kufanikisha malengo hayo. Tunashirikiana na nchi mbalimbali, maeneo tofauti na taasisi nyingi katika kuendeleza teknolojia hii,” alisema.
Dk Chandra alisisitiza kuwa Akili Unde haipaswi kuchukuliwa kama mbadala wa mkulima, bali ni nyenzo inayoweza kuongeza maarifa na kumsaidia kufanya maamuzi sahihi.
Alisema wakulima hufanya maamuzi mengi kila siku, yakiwamo ya wakati wa kupanda, kuvuna na kumwagilia mazao, ambayo wakati mwingine hufanywa kwa kutegemea makisio au uzoefu binafsi bila kuwa na taarifa zote zinazohitajika.
“Kwa kutumia Akili Unde, tunaweza kupunguza utegemezi wa makisio na kuwawezesha wakulima kufanya maamuzi yanayotegemea taarifa sahihi zaidi. Changamoto moja muhimu tunayojaribu kutatua ni namna ya kufanya teknolojia hii iwe nafuu na iweze kufikiwa na wakulima wengi,” alisema.
Alisema Tanzania ina nafasi ya kuwa kituo cha kikanda cha matumizi ya Akili Unde katika kilimo kutokana na nafasi yake ya kimkakati ya kuunganisha masoko ya ukanda huu.
“Tanzania inaweza kuwa mfano wa kituo cha kikanda cha Akili Unde kwa ajili ya kilimo, ambacho nchi nyingine katika ukanda huu zinaweza kujifunza kutoka kwake. Tunapozungumzia kituo cha kikanda cha Akili Unde kwa ajili ya kilimo, hatumaanishi tu mfumo unaoweza kujibu maswali, bali tunahitaji mifumo inayoweza kutoa majibu sahihi na yanayofaa kwa mazingira ya Tanzania,” alisema.
Katika hatua nyingine, mwanzilishi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya CeluNova kutoka Mexico, Adolfo Vidal Ruiz, alisema kampuni yake inazalisha nyuzi kutoka kwenye majani ya nanasi na kuzitumia kama malighafi katika utengenezaji wa karatasi za chooni na taulo za karatasi za jikoni.
“Karatasi hizi zina uwezo mkubwa wa kufyonza maji na ni imara zaidi, yaani zinastahimili kuvutwa na hazichaniki haraka ikilinganishwa na karatasi nyingine za chooni,” alisema.

