NBC yaimarisha uwekezaji, yazindua mifuko mitatu mipya
3 mins read

NBC yaimarisha uwekezaji, yazindua mifuko mitatu mipya

Dar es Salaam. Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeimarisha nafasi yake katika masoko ya mitaji nchini kwa kushiriki katika uzinduzi wa mifuko mitatu mipya ya uwekezaji inayolenga sekta za huduma za kifedha, madini, mawasiliano na teknolojia barani Afrika.

NBC imeteuliwa kuwa mdhamini na mtunzaji wa mali za uwekezaji (trustee and custodian) za mifuko hiyo iliyoanzishwa na kampuni ya iTrust Finance, inayolenga kuwawezesha wawekezaji kupata fursa za kuwekeza katika kampuni zilizoorodheshwa katika masoko ya hisa ya Afrika kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Mifuko hiyo ni iAfrica Financials ETF, iAfrica Mining ETF na iAfrica Telco and Tech ETF.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika Dar es Salaam, mapema wiki hii, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, alisema taasisi imara za kifedha zina nafasi muhimu katika kulinda mali za wawekezaji na kukuza masoko ya mitaji.

“Kadiri masoko ya mitaji barani Afrika yanavyozidi kuunganishwa, wawekezaji wanahitaji taasisi imara na zinazoaminika za kifedha zinazoweza kulinda mali zao na kuwezesha miamala ya kuvuka mipaka kuwa yenye ufanisi, usalama na gharama nafuu,” alisema Sabi.

Ushirikiano wa NBC na iTrust Finance tayari umewezesha uanzishaji wa bidhaa nyingine za uwekezaji, ikiwemo Mfuko wa Uwekezaji wa Hisa za Kampuni Kubwa za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Large Cap ETF).

Wakati wa uuzaji wa awali wa vipande vya mfuko huo, uliweza kuvutia uwekezaji wa Sh54.03 bilioni, dhidi ya lengo la Sh10 bilioni.

Sabi alisema mifuko hiyo mipya inalenga kuwapa wawekezaji fursa ya kushiriki katika sekta muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa Afrika, ikiwemo huduma za kifedha, uchimbaji wa madini na maendeleo ya teknolojia.

Alisema kipindi cha uuzaji wa awali wa vipande vya mifuko hiyo kilianza Oktoba 26 na kinatarajiwa kufungwa Novemba 27, 2026.

Wawekezaji wanaweza kupata msaada wa kujiunga kupitia matawi ya NBC nchini kote na njia za huduma za kibenki za kidijitali, ikiwemo programu ya simu.

Hata hivyo, Sabi aliwahimiza wawekezaji kusoma nyaraka za ofa, kuelewa malengo ya mifuko hiyo na kutathmini hatari zinazohusiana na uwekezaji kabla ya kufanya maamuzi.

Uzinduzi huo uliongozwa na Exaut Julius, Mkurugenzi wa Usimamizi na Uchunguzi wa Masoko wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), aliyemwakilisha Mtendaji Mkuu wa mamlaka hiyo, CPA Nicodemus Mkama.

Julius alisema ushirikiano kati ya wasimamizi wa sekta, kampuni za uwekezaji, wadhamini na watunzaji wa mali ni muhimu katika kujenga imani ya wawekezaji, kuimarisha uwazi na kupanua fursa za uwekezaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa iTrust Finance, Aunali Rajabali, alisema idadi kubwa ya vijana barani Afrika, rasilimali za asili na kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia ni miongoni mwa mambo yanayochochea fursa za uwekezaji.

Rajabali, mwenye uzoefu wa miaka 25 katika uwekezaji kwenye masoko ya hisa ya Afrika Mashariki, alisisitiza umuhimu wa nidhamu na mtazamo wa muda mrefu katika uwekezaji.

Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki kwa Biashara wa NBC, Elvis Ndunguru, alisema ushirikiano huo unaendeleza bidhaa zinazowaunganisha wawekezaji na fursa za masoko ya mitaji barani Afrika.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *