Ngoma ngumu uchaguzi Israel, Netanyahu, Eisenkot wahaha
3 mins read

Ngoma ngumu uchaguzi Israel, Netanyahu, Eisenkot wahaha

Israel. Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ameshindwa kupata wingi wa viti unaohitajika kuunda Serikali baada ya matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu kuonyesha kambi yake ikipungukiwa na viti vinane kufikia idadi inayotakiwa.

Hadi asilimia 90 ya kura zilipokuwa zimehesabiwa, kambi ya mrengo wa kulia inayoongozwa na Netanyahu ilikuwa imepata viti 53 kati ya 120 vya Bunge la Israel, Knesset, huku muungano wa upinzani unaoongozwa na Gadi Eisenkot ukitarajiwa kupata viti 48. Ili kuunda Serikali, kambi inahitaji angalau viti 61.

Kwa mujibu wa taarifa ya Al Jazeera ya Oktoba 29, 2026, zaidi ya kura 500,000 maalumu zilikuwa bado hazijahesabiwa, zikiwamo za wanajeshi, wanadiplomasia na wapigakura waliopiga kura nje ya vituo walivyosajiliwa.

Hali hiyo imeacha ushindani ukiwa wazi, huku mazungumzo ya kuunda Serikali yakitarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuamua hatima ya uongozi wa nchi hiyo.

Uchaguzi huo ni wa kwanza tangu mashambulizi yaliyoongozwa na Hamas dhidi ya Israel Oktoba 7, 2023, na vita vilivyofuata katika Ukanda wa Gaza. Pia umechukuliwa kama kipimo cha uungwaji mkono kwa uongozi wa Netanyahu, mwenye umri wa miaka 77.

Vyama vya Waarabu vyapata nafasi

Matokeo ya awali yanaonyesha vyama vya Waarabu, Joint List na Ra’am, vinaweza kupata jumla ya viti 19, idadi inayoweza kuvipa nafasi muhimu katika mazungumzo ya kuunda Serikali.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu, muungano wa Joint List umesema ushiriki mkubwa wa wapigakura Waarabu umechangia kuifanya kambi ya Netanyahu ishindwe kupata wingi wa viti bungeni.

Muungano huo umesema wapigakura wamepinga sera za ubaguzi wa rangi, ubomoaji wa nyumba za Wapalestina na vita.

Kiongozi wa Joint List, Yousef Jabareen, amesema muungano huo uko tayari kuunga mkono Serikali itakayoundwa bila Netanyahu, lakini hautajiunga moja kwa moja na Serikali hiyo.

Kwa upande mwingine, chama cha Likud kinachoongozwa na Netanyahu kimevituhumu vyama vya Waarabu kwa kuiba uchaguzi, kikidai kulikuwa na rushwa, vitisho, vurugu na matumizi ya programu zilizopigwa marufuku katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.

Likud imesema inawasilisha ushahidi kwa polisi, Shirika la Usalama wa Ndani la Israel na Tume Kuu ya Uchaguzi. Hata hivyo, madai hayo ni ya chama hicho na hayajathibitishwa kuwa ukweli.

Hatima ya Serikali bado haijajulikana

Licha ya kukosa wingi wa viti, Netanyahu bado ana nafasi ya kuunda Serikali kupitia mazungumzo na vyama vingine.

Baadhi ya wachambuzi wanaona uwezekano wa Serikali ya umoja, ingawa makubaliano hayo yanaweza kuwa magumu kutokana na tofauti za kisiasa kati ya kambi hizo.

Eisenkot amesema muungano wake umejikita katika kutafuta mabadiliko ya kisiasa na kuunda Serikali mbadala.

Rais wa Israel, Isaac Herzog, anatarajiwa kuanza mashauriano na viongozi wa vyama baada ya matokeo rasmi kutangazwa ili kubaini nani ana nafasi kubwa ya kuunda Serikali.

Wakati huo, Netanyahu ataendelea kuwa waziri mkuu wa mpito hadi Serikali mpya itakapoundwa.

Uchaguzi huo umefanyika wakati Israel ikiendelea kukabiliwa na athari za vita vya Gaza na mijadala kuhusu usalama, mustakabali wa Wapalestina na mwelekeo wa kisiasa wa nchi hiyo.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *