Nyumba 400 zabomoka, mmoja afariki mvua zinazoendelea kunyesha Mara
2 mins read

Nyumba 400 zabomoka, mmoja afariki mvua zinazoendelea kunyesha Mara

Musoma. Mtoto mmoja amefariki dunia huku nyumba zaidi ya 400 zikibomolewa katika wilaya za Bunda na Rorya mkoani Mara kufuatia mvua za El- Nino zinazoendelea kunyesha nchini.

Taarifa hiyo imetolewa mjini Musoma leo Jumamosi Oktoba 31, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi wakati akitoa salaam za rambirambi katika mazishi ya baba mzazi wa Mkuu wa Polisi nchini (IGP), Camilius Wambura, Deusdedit Wambura (100).

“Kwa bahati mbaya sana tumempoteza mtoto mmoja kule Rorya huku nyumba zaidi ya 400 zikipata madhara mbalimbali kwa viwango tofauti katika wilaya za Rorya na Bunda hadi sasa,” amesema.

Amewataka wakazi wa mkoa huo kuendelea kuchukua tahadhari huku akikemea tabia ya baadhi ya watu kubeza utabiri wa hali ya hewa kuhusu mvua za El-Nino.

Amesema mvua hizo zipo na zimeanza kunyesha na madhara yameanza kutokea ambapo ameaagiza wale wote wanaoishi mabondeni na maeneo hatarishi kuhama mara moja ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.

“Niwaambie tu kuwa El- Nino ipo na imeanza,juzi nimepokea simu kutoka Bunda mwananchi anasema ile sio mvua ni gharika maana maji yalikuwa yanamwagika kama yanatokea kwenye tenki,niwatake wote kwa pamoja tuendelee kuchukua tahadhari kuna madhara yanaweza kuepukika tukichukua tahadhari,” amesema.

Mtambi amesema tahadhari hizo mbali na kuhama katika maeneo hatarishi pia ni pamoja na kutokuruhusu wanafunzi kwenda shule endapo kutakuwa na viashiria hatarishi ili kuepuka majanga yanayoweza kutokea.

Amewataka wakazi wa mkoa huo kuendelea na shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo cha mazao yanayohimili mvua nyingi hatua ambayo amesema itasaidia kuimarisha hali ya usalama wa chakula pamoja na uchumi wa wakulima na wananchi kwa ujumla.

Oktoba 24, 2026, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Halfan Haule alisema nyumba zaidi ya 360 zimepata madhara mbalimbali ikiwepo kubomoka kufuatia mvua za El-Nino zilizoambatana na upepo zilizonyesha wilayani Bunda mkoani Mara.

Alisema kutokana na hali hiyo baadhi ya familia zimelazimika kupata hifadhi kwa ndugu, jamaa na marafiki huku Serikali ikitoa msaada wa chakula kwa familia hizo huku akisema tathmini ya athari ya mvua hizo inaendelea.

Baadhi ya nyumba zilizobomolewa na mvua za El- nino wilayani Bunda.

Alifafanua kuwa kati ya nyumba hizo, 50 zimebomoka kabisa na hazifai kwa matumizi tena na hadi sasa kata tatu wilayani humo ndizo zilizoathiriwa na mvua hizo.

Ameeleza kuwa mvua hizo zilizonyesha Oktoba 21 na 22 mwaka huu ambapo kata zilizoathirika ni Kabasa, Hunyari na Mcharo zote za halmashauri ya Mji wa Bunda.

Alitoa wito kwa wadau kuchangia vifaa vya ujenzi ili kuwezesha wamiliki wa nyumba hizo kurejesha makazi yao katika hali ya kawaida na kuendelea na shughuli zao za kila siku.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *