Saccos zahimizwa kuwekeza katika Tehama
2 mins read

Saccos zahimizwa kuwekeza katika Tehama

Arusha. Vyama vya kuweka na kukopa (Saccos) vimetakiwa kuwekeza na kuendeleza matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) ili kurahisisha huduma kwa wanachama na kuchochea ukuaji wa mitaji.

Wito huo umetolewa Oktoba 24, 2026 na Naibu Mkurugenzi Mtendaji (Uzalishaji) wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi Anthony Mbushi, wakati akizungumza katika mkutano mkuu wa 58 wa mwaka wa Tanesco Saccos uliofanyika jijini Arusha.

Mbushi amesema mifumo ya kidijitali inaweza kusaidia vyama hivyo kuongeza ufanisi wa huduma, kupunguza usumbufu kwa wanachama na kuimarisha usalama wa mali zao.

Amesema Tanesco Saccos imepiga hatua katika ukuaji wa mtaji huku ikiendelea kuboresha huduma zake kwa kutumia mifumo ya kidijitali.

“Kwa mfano, mtu anapotaka kukopa, mambo yote yanafanyika kidijitali. Hii inarahisisha huduma kwa wanachama na kuonyesha namna ambavyo chama kinaendelea kuboresha utendaji wake,” amesema.

Mbushi amesema Saccos zina nafasi muhimu katika maendeleo ya mtu mmoja mmoja na uchumi wa Taifa kwa ujumla, kwa kuwa zinawawezesha wanachama kupata mitaji ya uwekezaji kupitia mikopo yenye riba nafuu na inayomudu kulipwa.

Amesisitiza umuhimu wa vyama hivyo kuwa na mipango mkakati ya muda mrefu itakayoviongoza kutekeleza malengo yake na kuhakikisha vinaendelea kutoa huduma zenye tija kwa wanachama.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco Saccos, Omari Shabani, amesema chama hicho kinaendelea kukua, huku thamani ya mali zake ikifikia Sh86 bilioni na mtaji kufikia Sh7.5 bilioni.

Amesema akiba za wanachama pia zimeongezeka kutoka Sh62 bilioni hadi Sh72 bilioni kufikia Septemba mwaka huu.

Shabani amesema matumizi ya mifumo ya Tehama ni miongoni mwa vichocheo vya ukuaji wa chama hicho na uboreshaji wa huduma zake.

Amesema kupitia mifumo hiyo, wanachama wanaweza kuhamisha fedha kutoka akaunti zao za Saccos kwenda akaunti zao binafsi na kupata huduma za mikopo kwa kutumia simu za mkononi bila kulazimika kufika ofisini.

“Wanachama wetu wanapata huduma kupitia simu zao za mkononi. Wanaweza kuhamisha fedha kwenda kwenye akaunti zao binafsi na kupata huduma za mikopo kwa njia ya simu kupitia mfumo bila kufika ofisini,” amesema.

Amewataka viongozi wa vyama vingine vya ushirika kutokata tamaa ya kuwekeza katika mifumo ya kidijitali, akisema licha ya changamoto zinazoweza kujitokeza, teknolojia ina mchango mkubwa katika kurahisisha miamala na kuboresha huduma.

Akizungumzia manufaa ya chama hicho, mwanachama wa Tanesco Saccos, Harold Ramsey, kutoka Kituo cha Kufua Umeme cha Mafia, amesema amekuwa akinufaika na huduma za chama hicho na kupata fursa ya kukua kiuchumi.

Amesema matumizi ya Tehama yamerahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha, hivyo kumwezesha mwanachama kuhudumiwa bila usumbufu.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *