Tanzania, Kenya zilivyojipanga kuimarisha ulinzi wa mpaka Horohoro
Mkinga. Polisi wa Tanzania na Kenya wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiusalama katika mpaka wa Horohoro, Wilaya ya Mkinga, mkoani Tanga, ili kudhibiti wahalifu wanaovuka mipaka kujificha baada ya kutenda uhalifu na kuzuia biashara haramu ya mirungi.
Hatua hiyo inalenga kukabiliana na changamoto ya watu wanaotenda uhalifu nchini Tanzania na kukimbilia Kenya, pamoja na wanaofanya uhalifu Kenya na kuingia Tanzania kupitia njia zisizo rasmi za mpakani.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kilichowakutanisha maofisa wa vyombo vya usalama kutoka nchi hizo mbili, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Gilbert Kalima, na Mkuu wa Wilaya ya Lunga Lunga nchini Kenya, Christopher Siale, kwa lengo la kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto za kiusalama zinazovuka mipaka.
Akizungumza katika kikao hicho, leo Jumapili, OKtoba 24, 2026, Siale amesema ni muhimu viongozi wa maeneo yanayopakana na maofisa wa usalama kufanya vikao vya pamoja mara kwa mara ili kutatua changamoto zinazohusu usalama, uhamiaji na uvuvi, ambazo zinaathiri jamii za pande zote mbili.
Kwa upande wake, Kalima amesema mojawapo ya changamoto zilizopo ni baadhi ya waendesha pikipiki kuvuka kwenda Kenya bila kuzingatia masharti ya nchi hiyo, hali inayowafanya kuchukuliwa hatua za kisheria na baadaye kulalamika.
“Ni kweli sisi ni ndugu na jamii tunazoishi pamoja, lakini vigezo na masharti lazima yazingatiwe. Kenya wana sheria zao na Tanzania tuna sheria zetu,” amesema Kalima.
Amesema biashara na matumizi ya mirungi ni miongoni mwa changamoto zinazohitaji kushughulikiwa kwa ushirikiano wa nchi hizo mbili, akieleza kuwa matumizi ya dawa za kulevya yanaweza kuchangia kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu katika jamii.
Mkuu wa Wilaya ya Lunga Lunga nchini Kenya, Christopher Siale, akizungumza katika kikao cha pamoja cha viongozi na maofisa wa usalama wa Tanzania na Kenya kuhusu mikakati ya kukabiliana na uhalifu na biashara haramu. Picha na Mbonea Herman.
Amewataka maofisa wa usalama wa Kenya kushirikiana na wenzao wa Tanzania kuwabaini na kuwachukulia hatua watu wanaotumia pikipiki kuvuka mipaka kwa lengo la kusafirisha mirungi kinyume cha sheria.
Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Lunga Lunga, Danson Mwakundia, amesema ushirikiano wa polisi wa nchi hizo mbili ni muhimu kwa kuwa baadhi ya watu wanaotenda uhalifu upande mmoja huvuka mpaka na kujificha upande mwingine ili kukwepa kukamatwa.
Amesema vyombo vya usalama vinaendelea kushirikiana kudhibiti vitendo hivyo, huku akiwataka wananchi wanaoishi maeneo ya mpakani kuzingatia sheria za nchi wanayotembelea na kutumia njia rasmi wanapovuka mpaka.
Mwakundia amesisitiza kuwa ujirani mwema haupaswi kutumiwa kama kisingizio cha kuvunja sheria. Amesema watu wanaovuka mpaka kwa shughuli za biashara au zinazohusisha mirungi wanapaswa kuzingatia sheria za nchi husika na kuwajibika wanapokiuka masharti yaliyowekwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema kupitia mradi wa Nyumba Yangu, Hakuna Uhalifu, jamii inapaswa kushirikiana na polisi kuhakikisha wahalifu hawapati nafasi ya kujificha katika maeneo yao.
Amewataka wananchi kutoa taarifa za uhalifu kwa vyombo vya usalama, akiahidi kuwa taarifa hizo zitahifadhiwa kwa siri.
Mchunguzi pia amesisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kuwapatia watoto malezi bora na kuwafundisha kuzingatia sheria. Amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani ili shughuli za maendeleo ziweze kufanyika bila vikwazo.
Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Mkinga wamesema ushirikiano huo unaweza kusaidia kupunguza biashara haramu ya mirungi inayowahusisha baadhi ya vijana, ambao wanahatarisha maisha yao kwa kutumia njia zisizo rasmi na kusafiri nyakati za usiku wakiwa na mizigo hiyo.
Mkazi wa eneo hilo, Yusuph Ally, amesema baadhi ya vijana hutumia njia zisizo rasmi katika eneo la Jasini kusafirisha mirungi kwa pikipiki, mara nyingi nyakati za usiku. Alisema hali hiyo inahitaji hatua za pamoja za vyombo vya usalama ili kukomesha biashara hiyo.
Ameongeza kuwa kuimarishwa kwa doria, ubadilishanaji wa taarifa na ufuatiliaji wa njia zisizo rasmi za mpakani kutasaidia kudhibiti vitendo hivyo na kuwakinga vijana dhidi ya hatari wanazokumbana nazo wanapojihusisha na usafirishaji haramu wa mirungi.

