Same yatenga siku saba kudhibiti tembo
Same. Serikali ya Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, inatarajia kuanza operesheni ya siku saba ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu, hususan tembo wanaovamia makazi na mashamba ya wananchi na kusababisha majeraha pamoja na uharibifu wa mazao.
Operesheni hiyo inatarajiwa kuanza kesho, Oktoba 26, 2026, kwa ushirikiano kati ya Serikali ya wilaya na taasisi za uhifadhi, zikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Akizungumza leo kuhusu maandalizi ya operesheni hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, amesema vikosi vinne vimeundwa ili kudhibiti uvamizi wa tembo katika maeneo yaliyoathirika zaidi, yakiwemo Kisiwani, Ndungu, Makanya, Hedaru, Njoro na Ruvu.
Amesema operesheni hiyo inalenga kupunguza migongano kati ya binadamu na wanyamapori, kuimarisha usalama wa wananchi na kuwawezesha kuendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu ya kushambuliwa au kupoteza mazao.
“Changamoto hii imekuwa kubwa katika wilaya yetu, wananchi wanajeruhiwa na mazao yao yanaliwa, hivyo Serikali ni lazima itatue kero hizi ili kuwapa wananchi tabasamu, kama Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alivyotuagiza,” amesema Mgeni.
Amesema operesheni hiyo ni sehemu ya mikakati ya Serikali kwa kushirikiana na taasisi za uhifadhi kutafuta suluhisho la changamoto ya wanyamapori wanaoingia katika makazi ya watu na maeneo ya shughuli za kibinadamu.
Mgeni amewataka wananchi kushirikiana na vikosi vitakavyofika katika maeneo yao, akisema elimu kuhusu namna ya kujikinga na wanyamapori hao itatolewa ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
Droni, magari kutumika kufuatilia tembo
Kwa upande wake, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Eva Mallya, amesema vikosi vitatumia ndege zisizo na rubani (droni) pamoja na magari kuwafuatilia na kuwafukuza tembo kutoka maeneo ya wananchi.
“Kazi hii itafanyika kwa umakini mkubwa kwa kushirikiana na wananchi. Nitoe wito kwa wananchi wote kwamba watakapoona zoezi hili linafanyika, watoe ushirikiano wa kutosha,” amesema Mallya.
Naye Kamanda anayesimamia Mapori Tengefu ya Ruvu-Same, Kalimawe na Mto Umba kutoka Tawa, Lackson Mwamwezi, amesema vikosi vitasambazwa katika maeneo manne ili kurahisisha udhibiti wa wanyamapori hao.
Amesema kikosi cha kwanza kitakuwa Kata ya Maore, kikihudumia pia maeneo ya Kisiwani na Ndungu. Kikosi cha pili kitahudumia kata za Makanya na Hedaru, cha tatu kitakuwa Kata ya Njoro, huku cha nne kikielekezwa Kata ya Ruvu.
Mwamwezi amesema mafanikio ya operesheni hiyo yanategemea ushirikiano kati ya wananchi na vikosi vya uhifadhi, huku elimu itakayotolewa ikitarajiwa kuwasaidia wananchi kujikinga dhidi ya hatari zinazoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu.
Operesheni hiyo inatarajiwa kusaidia kupunguza hatari kwa wananchi na uharibifu wa mazao katika maeneo yanayokabiliwa na uvamizi wa tembo.

