UDSM yaadhimisha miaka 65 kwa elimu, tafiti, uhifadhi mazingira
Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeadhimisha miaka 65 tangu kuanzishwa kwake, kikijivunia mchango wake katika elimu ya juu, tafiti na kuandaa viongozi, huku kikiweka mbele umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kampasi kuu ya chuo hicho jijini Dar es Salaam, leo Jumapili, Oktoba 25, 2026, upandaji miti ulikuwa miongoni mwa shughuli zilizotumika kuenzi safari ya chuo hicho na kuashiria mwanzo wa miaka mingine 65 ya kutoa huduma kwa wananchi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye, amesema chuo hicho kilichoanzia Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam kimepanua wigo wa shughuli zake hadi maeneo mbalimbali nchini.
“Tupo Zanzibar, Nzega, Dodoma, Mbeya na sasa tunakwenda Kagera na Lindi. Chuo hiki kilianzishwa kwa michango ya Watanzania ili kuwasaidia watoto wa Kitanzania kupata elimu,” amesema.
Amesema mafanikio ya chuo hicho yametokana pia na mchango wa viongozi wa Taifa, kuanzia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hadi Rais Samia Suluhu Hassan.
“Tuna kila sababu ya kutoa shukrani kwa waasisi wa Taifa letu, kuanzia Mwalimu Nyerere hadi Samia, wote wametushika mkono kuhakikisha UDSM tunafikia hapa tulipo,” amesema.
Profesa Anangisye amesema chuo hicho kinajivunia wahitimu waliofikia nafasi za juu katika uongozi, wakiwamo marais na mawaziri wakuu. Alimtaja Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, miongoni mwa waliowahi kusoma UDSM, huku akiwataka watumishi kutafakari safari ya chuo hicho, kilikotoka na kinakoelekea.
“Na leo tunapanda miti kama sehemu ya kumbukumbu ya kutimiza miaka 65, ikiwa mwanzo wa miaka 65 mingine. UDSM tupo kwa ajili ya wananchi,” amesema.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa William Anangisye, akipanda mti katika hafla ya maadhimisho ya miaka 65 ya kuanzishwa kwa Chuo hicho Oktoba 25, 2026, Katika kampasi kuu ya Chuo hicho jijini Dar es Salaam.
Upandaji miti kuimarisha uhifadhi
Akizungumzia upandaji miti katika maadhimisho hayo, Profesa Samora Andrew wa Idara ya Mimea amesema shughuli hiyo inalenga kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kuendeleza utamaduni wa kuhifadhi miti.
Amesema miti ina mchango muhimu katika upatikanaji wa oksijeni na hutoa rasilimali zinazotumika katika shughuli mbalimbali, zikiwamo kuni, mkaa na mbao.
Amewashauri Watanzania kuzingatia upandaji wa miti ya asili kutokana na mchango wake katika kuhifadhi mazingira na kusaidia wadudu pamoja na viumbe wengine.
“Tunawashauri wataalamu wanapopanda miti watumie miti ya asili, kwani miti hiyo ni rafiki wa wadudu na viumbe wengine,” amesema.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anayeshughulikia Utafiti, Profesa Nelson Boniface, akipanda mti katika hafla ya maadhimisho ya miaka 65 ya kuanzishwa kwa Chuo hicho, Oktoba 25, 2026 katika kampasi kuu ya Chuo hicho jijini Dar es Salaam.
Chuo chajivunia tafiti na uoto wa asili
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Utafiti, Profesa Nelson Boniface, amesema UDSM inajivunia juhudi za kulinda miti na kuhifadhi uoto wa asili, unaosaidia pia kutunza makazi ya viumbe mbalimbali, wakiwamo wanyama.
Amesema chuo hicho kina zaidi ya wanafunzi 42,000 na kwamba kila mwanafunzi akipanda mti mmoja, hatua hiyo inaweza kuongeza idadi kubwa ya miti.
Ameongeza kuwa tafiti zinazofanywa na chuo hicho zimekuwa na mchango kwa jamii katika maeneo mbalimbali, yakiwamo biashara na ujasiriamali.
Wanafunzi wa Shule ya Sheria, wajivunia mafanikio
Akizungumzia mafanikio ya Shule Kuu ya Sheria ya UDSM (UDSoL), Mratibu wa shahada za awali wa shule hiyo, Sesilia Ngaiza, amesema taasisi hiyo inajivunia safari yake na matarajio ya kuendelea kukua.
Amesema upandaji miti katika maadhimisho hayo ni ishara ya maendeleo na matarajio ya kuimarika kwa chuo hicho katika miaka ijayo.
“Matarajio yetu Shule Kuu ya Sheria ni kuendelea kukua kama mti uliopandwa unaoendelea kukua. Hivyo upandaji miti huu ni ishara ya maendeleo ya chuo chetu na kuanza ukurasa mpya wa miaka 65 mingine,” amesema.
Kwa upande wa wanafunzi, Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa UDSM (Daruso), Mwakigowe Steven, amewataka kujivunia mafanikio ya chuo hicho na kutumia maarifa wanayopata kuchangia maendeleo ya jamii.
Amesema elimu inayotolewa na chuo hicho imekuwawezesha wahitimu kushika nafasi mbalimbali katika jamii na kupata fursa za ajira.
“Chuo kilianzishwa na wanafunzi 11 pekee lakini leo tupo zaidi ya 40,000. Haya ni mafanikio makubwa,” amesema.

