Teknolojia ya jua yaja kuokoa misitu, kuongeza ubora wa tumbaku
Arusha. Ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazochangiwa na ukataji wa miti na matumizi ya kuni katika ukaushaji wa tumbaku, teknolojia ya kutumia nishati ya jua imebuniwa kama suluhisho la kukabiliana na ukataji miti na misitu.
Teknolojia hiyo inalenga kupunguza utegemezi wa kuni katika ukaushaji wa tumbaku, huku ikiwezesha zao hilo kukaushwa kwa muda mfupi na kwa ubora unaoweza kuongeza kipato cha mkulima.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Oktoba 26,2026 Mhadhiri kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Dismas Kimaro, amesema tafiti zinaonyesha kuwa takriban tani milioni 1.5 za kuni hutumika kila mwaka kwa ajili ya kukausha tumbaku nchini.
Amesema hali inayochangia ukataji mkubwa wa misitu, hususani katika maeneo yanayolima zao hilo kama Tabora.
Mhadhiri huyo amesema hali hiyo imeifanya taasisi hiyo kupitia kundi lake la watafiti kuja na teknolojia inayotumia nishati ya jua kama njia mbadala ya kuni ambayo ni rafiki kwa mazingira.
Amesema katika teknolojia hiyo wameunganisha mfumo unatumia joto la jua moja kwa moja wakati jua linapokuwa linawaka.
Kimaro amesema faida ya teknolojia hii ni kupunguza muda wa ukaushaji na kuboresha ubora wa tumbaku ambapo kwa sasa hutumia hadi siku saba kukausha tumbaku ila kwa majaribio yao wameweza kukausha ndani ya saa 13.
“Pia, tumebaini kuwa teknolojia hii inaweza kusaidia kupata tumbaku yenye ubora unaotakiwa. Katika tathmini yetu, tumbaku iliyokaushwa kwa teknolojia hii ilionesha matokeo mazuri katika madaraja ya ubora ikilinganishwa na ile inayokaushwa kwa njia za kawaida,”
Mhadhiri huyo amesema kwa sasa wameanza na mtambo wa majaribio ambao ulikuwa na uwezo wa kukausha kilo 20 za tumbaku kwa wakati mmoja na kwa sasa wamepiga hatua na kujenga mtambo mkubwa zaidi mkoani Tabora, ambao una uwezo wa kukausha zaidi ya kilo 500 za tumbaku kwa wakati mmoja.
Akizungumzia gharama za teknolojia hiyo amesema ipo juu kidogo ila wanafikiria kutumia mfumo wa vituo maalumu vya kukaushia tumbaku badala ya kila mkulima kulazimika kujenga mtambo wake.
Kwa upande wake mkulima wa tumbaku kutoka Chama cha Ushirika cha Msingi cha Malumba (Malumba Amcos), Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Kisiriga Swalehe, amesema matumizi ya teknolojia ya kukaushia tumbaku kwa kutumia nishati ya jua yatasaidia kupunguza ukataji wa miti, kulinda mazingira na kuboresha ubora wa zao hilo.
Amesema akiwa na uzoefu wa miaka 10 ya kilimo hicho, changamoto nyingine inayowakabili wakulima ni mabadiliko ya tabianchi, hasa wakati wa mvua nyingi, ambapo unyevunyevu unaweza kuathiri mchakato wa ukaushaji na kusababisha tumbaku kupoteza rangi na ubora wake.
“Isipokauka katika mazingira yanayotakiwa, inaweza kupoteza rangi na ubora wake,” amesema.
Amesisitiza kuwa Serikali na wadau wa sekta ya tumbaku wanapaswa kuwekeza katika teknolojia na kuhakikisha inawafikia wakulima wengi zaidi, akishauri ianze kuoneshwa kwa vitendo katika vyama vya msingi vya ushirika ili wakulima waweze kujifunza na kuona manufaa yake.
