Tshisekedi aomba kuungwa mkono kumkabili Kabila
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix Tshisekedi, ametoa wito kwa wananchi wa nchi hiyo, vyama vya upinzani washirika na mataifa ya nje kumuunga mkono katika kukabiliana na Rais mstaafu, Joseph Kabila, akieleza wasiwasi wake kuhusu mpango wa mtangulizi wake kuongoza vuguvugu la kisiasa na kijeshi.
Tshisekedi ametoa kauli hiyo baada ya kukaa muda mrefu bila kumzungumzia Kabila, ambaye anaongoza vuguvugu la kisiasa na kijeshi linalojulikana kama Front pour la refondation de la nation (FRN), linaloshirikiana na waasi wa M23.
Muungano huo mpya ulitangazwa rasmi Oktoba 12, 2026, katika mkutano uliofanyika mjini Goma, mashariki mwa DRC, ukiwa na lengo la kuratibu vikosi vya upinzani ili kuiondoa madarakani serikali ya Tshisekedi.
Kabila, aliyeiongoza DRC kuanzia mwaka 2001 hadi 2019, anatarajiwa kuongoza muungano huo, ambao umetangaza kuwa utatumia njia zote, ikiwemo nguvu, kufanikisha malengo yake hatua inayoleta wasiwasi kuhusu mustakabali wa usalama na amani nchini humo.
Hali hiyo imekuja wakati baadhi ya washirika wa vuguvugu hilo wakianza kujitenga na msimamo wa kutumia silaha, jambo linaloashiria kutokuwapo kwa mwafaka miongoni mwao kuhusu njia za kufanikisha malengo yao ya kisiasa.
Kwa mujibu wa RFI Swahili, katika mkutano wake wa kwanza rasmi wa kisiasa uliofanyika mjini Kinshasa juzi, Tshisekedi alimshambulia mtangulizi wake huyo na kuwahamasisha wanasiasa wanaounda muungano wake kuungana katika kukabiliana na uasi huo mpya.
“Natoa wito kwa wananchi, vyama vya upinzani washirika na mataifa ya nje tunayoshirikiana nayo kutuunga mkono katika kukabiliana na Kabila pamoja na muungano wake wote,” alisema Tshisekedi.
Katika mkutano huo, Tshisekedi alikutana na wabunge na maseneta wa muungano wake wa Union sacrée mjini Kinshasa, siku chache baada ya Kabila kuchukua rasmi uongozi wa FRN.
Tshisekedi alimlaumu Kabila kufuatia hatua yake ya kuongoza muungano huo, akimtaja hadharani kuwa ni mwoga na kudai kuwa ameamua kutumia silaha baada ya kuiongoza nchi hiyo kwa miaka 18.
Aidha, aliwahakikishia wanachama wa Union sacrée kuwa hali ya usalama inadhibitiwa na Jeshi la DRC (FARDC) linaendelea kufanya vizuri katika uwanja wa vita licha ya changamoto zinazolikabili.
Wito wa kujibana kiuchumi
Katika hotuba yake, Tshisekedi aliwataka viongozi na wananchi kupunguza matumizi ili kusaidia kugharamia vita vinavyoendelea mashariki mwa nchi hiyo, pamoja na kutekeleza miradi ya maendeleo katika muhula wake wa uongozi.
Akizungumzia suala la katiba, ambalo limeibua mjadala kuhusu uwezekano wa kutaka kuongeza muda wake wa uongozi, Tshisekedi alidai hana nia ya kujiongezea madaraka kinyume na matakwa ya wananchi, huku akisisitiza dhamira yake ya kurejesha amani ya kudumu nchini humo.
Pia, aliwahamasisha wabunge wanaomuunga mkono kujiandaa kwa mazungumzo ya kitaifa yanayotarajiwa kufanyika, akijibu wasiwasi uliojitokeza kufuatia mabadiliko ya kisiasa na kiusalama nchini humo.
Wananchi wasema ni propaganda
Akizungumza na Mwananchi, mwandishi wa habari wa DRC, Chube Ngorombi, amesema licha ya hotuba ya Tshisekedi, wananchi wanaichukulia kama propaganda kwa kuwa hawaoni hatua za kutosha zinazochukuliwa kurejesha amani nchini humo.
Amesema viongozi hao wawili wamekuwa wakitoa kauli kwa nyakati tofauti wakitaka kuungwa mkono, huku akibainisha kuwa Kabila tayari amewekewa vikwazo na jumuiya ya kimataifa.
“Wananchi wa DRC, hasa wa mashariki mwa nchi, wanapitia wakati mgumu. Hakuna amani, na kila machafuko yanapoanza, wananchi ndio wanaopata shida. Wananchi wanataka kiongozi atakayerudisha amani, awe Kabila au Tshisekedi,” amesema Ngorombi.
Ameongeza kuwa mapigano yanapoanza, viongozi wanaohusika hawapati madhara makubwa kama wananchi wa kawaida, ambao hujikuta katika mazingira magumu ya maisha.
Amesema hali inayoendelea mashariki mwa DRC imewaacha wananchi katika mazingira ya njaa, kushindwa kufanya kazi na kukosa amani, huku wakikabiliwa na changamoto za maisha zinazochochewa na mapigano yanayoendelea katika maeneo hayo.

