Ulega: Haki si kwa matajiri, kila mwananchi anastahili
2 mins read

Ulega: Haki si kwa matajiri, kila mwananchi anastahili

Kibaha. Waziri wa Katiba na Sheria, Abdallah Ulega amesema Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Awamu ya Pili ni hatua muhimu ya kuwawezesha wananchi kupata haki bila vikwazo vya kiuchumi, akisisitiza haki haipaswi kuwa fursa ya watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha pekee.

Amesema kampeni hiyo ni daraja kwa wananchi wenye changamoto za kisheria, hususani wasiokuwa na uelewa wa mahali pa kwenda kupata msaada wa kisheria.

Waziri Ulega ameyasema hayo Oktoba 28, 2026, wakati akifungua utekelezaji wa kampeni hiyo katika Mkoa wa Pwani, kwenye Viwanja vya Stendi ya Zamani ya Maili Moja, Kibaha.

“Kampeni hii ya Mama Samia Legal Aid ni daraja, ni ukombozi kwa wananchi wengi wa hali ya chini, wasiojua wapi pa kwenda na hatua gani ya kuchukua,” amesisitiza Waziri Ulega.

Ameeleza kuwa kampeni hiyo inalenga pia kuwafikia wajane, yatima, watu wenye ulemavu na wananchi wanaoishi maeneo ya pembezoni, ili kuwawezesha kupata elimu na huduma za kisheria kwa ajili ya kulinda haki zao.

Aidha, amewahimiza wananchi wa Mkoa wa Pwani kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo ya siku 10, akiwataka kuwa mabalozi wa kampeni kwa kuwahamasisha wengine wenye changamoto za kisheria kupata huduma hizo.

Pia, amewapongeza viongozi wa dini na wataalamu wa sheria kwa mchango wao katika kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo amewataka wananchi kujitokeza kupata msaada wa kisheria, hususan kuhusu migogoro ya ardhi, mirathi na ukatili wa kijinsia.

Amesema kampeni hiyo inatoa fursa kwa wananchi wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za huduma za kisheria kupata haki zao, akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kuimarisha upatikanaji wa haki nchini.

Waziri wa Katiba naSheria Abdalah Ulega akiwa na viongozi wengine kwenye uwanja wa Mailimija Kibaha Pwani. Picha na Sanjito Msafiri

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dk Seif Abdallah Shekalaghe, amesema kampeni hiyo itatekelezwa kuanzia mwaka 2026 hadi 2030 ili kuhakikisha umaskini hauwi kikwazo cha kupata haki.

Ameongeza kuwa kampeni hiyo inaunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 kupitia uimarishaji wa utawala bora, haki za binadamu na utawala wa sheria.

Kampeni hiyo katika Mkoa wa Pwani itatekelezwa kwa siku 10, kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 7, 2026, katika halmashauri zote za mkoa huo.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *